Viongozi wa Kiislamu Ethiopia walaani hujuma dhidi ya misikiti Amhara

Viongozi wa Kiislamu nchini Ethiopia wamelaani vikali hujuma na kuteketezwa moto misikiti minne katika jimbo la Amhara ambalo liko kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Baraza Kuu la Waislamu nchini Ethiopia limelaani vikali mashambulizi hayo dhidi ya misikiti sambamba na hujuma dhidi ya kanisa katika eneo la Amhara, likisisitiza kuwa, wahusika wa mashambulizi hayo hawana azma nyingine ghairi ya kutaka kupanda mbegu za chuki na uhasama kwa misingi ya dini.
Jana Jumanne, mwanazuoni mashuhuri nchini Ethiopia, Sheikh Kamil Shemsu katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press alisema kuwa, baadhi ya wanasiasa ndio wanaotaka kuwatenganisha na kuwachonganisha Waethiopia katika misingi ya dini. Aidha amesisitiza kuwa hujuma hizo zimechochewa na wanaharakati wenye mielekeo hasi na usambazaji wa video za kichochezi kwenye mitandao ya kijamii.
Misikiti minne iliteketezwa moto na Wakristo waliokuwa na hasira katika mji wa Motta siku chache zilizopita, baada ya Kanisa la Orthodox kuteketezwa moto na watu wasiojulikana.

Makumi ya maelefu ya Waislamu wamefanya maandamano katika miji kadhaa nchini Ethiopia kulaani hujuma hizo dhidi ya misikiti katika eneo lenye Wakristo wengi la Amhara kaskazini mwa nchi hiyo.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed hivi karibuni pia alilaani hujuma hizo katika taarifa na kusema: "Njama za watu wenye misimamo ya kufurutu ada za kutaka kuvuruga historia nzuri ya maelewano na kuishi pamoja kwa amani wafuasi wa dini mbali mbali ni jambo lisilokuwa na nafasi katika Ethiopia mpya inayolenga ustawi."
Jimbo la Amhara limekuwa kitovu cha mapigano ya kikabila kwa miaka mingi sasa, ambayo hivi sasa yanaonekana kuchukua mkondo wa udini.

0 Comments