Waislamu wa Rohingya: Dunia isikubali utetezi wa San Suu Kyi katika mahkama ya Uholanzi

Waislamu wa jamii ya Rohingya wameitaka jamii ya kimataifa isikubali matamshi ya Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala nchini Myanmar aliyoyatoa katika Mahkama ya Kimataifa ya Uadilifu ICJ.
Hii ni baada ya Jumatano ya jana Suu Kyi kujitetea katika mahkama hiyo huko Uholanzi kutokana na hujuma za serikali yake kuwalenga Waislamu wa jamii hiyo nchini Myanmar. Katika utetezi wake Suu Kyi alipinga kujiri aina yoyote ya mauaji dhidi ya Waislamu nchini kwake na kudai kuwa sababu ya mamia ya Waislamu hao kuondoka Myanmar na kuelekea nchi nyingine ilitokana na vita dhidi ya waasi. Aung San Suu Kyi ametoa kauli hiyo katika hali ambayo mwaka 2017 jeshi la nchi hiyo lilifanya mauaji makubwa ya umati kuwalenga Waislamu wa jamii ya Rohingya, kufanya vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia na pia kuteketeza kwa moto nyumba zao.
Jamii ya Waislamu wa Rohingya inayokandamizwa zaidi nchini Myanmar kutokana na imani yao
Mahkama ya Kimataifa ya Uadilifu nchini Uholanzi ilianza kuchunguza faili la mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Rohingya kuanzia siku ya Jumanne, baada ya serikali ya Gambia ikiziwakilisha nchi 57 za Kiislamu kuifungulia mashtaka Myanmar. Itakumbukwa kuwa wimbi jipya la mauaji, mashambulizi na ubakaji wa jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu wa Rohingya, lilianza tarehe 25 Agosti mwaka 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa. Aidha zaidi ya Waislamu wengine milioni moja wa jamii hiyo walilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh. Hujuma za jeshi la Myanmar kwa kushirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kigaidi katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu hao zilianza tangu mwaka 2012.

0 Comments