Wanazuoni waandamizi watoa neno Misk ya Roho

Wanazuoni kadhaa waandamizi wamesifu Kongamano la Tatu la Misk ya Roho na kutaka juhudi kama hizi ziendelezwe na kuigwa.
Mmoja wa Wanazuoni hao ni Sheikh Suleiman Amran Kilemile, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hayat) ambaye alisema kongamano la mwaka huu lilifanikiwa. Sheikh Kilemile alitaja nukta mbili zinazothibitisha mafanikio hayo kuwa ni kitendo cha kukusanya Waislamu zaidi ya 5,000 na kuwafikishia maudhui mazuri yanayohusu Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Hata hivyo, Sheikh Kilemile alisema ingefaa kongamano hilo liende na mikoani au wengine waige ili kusambaza faida zinazopatikana.
Naye, Sheikh Othman Kaporo alisema makongamano ya aina ya Misk ya Roho yanahitaji kufufua imani za watu, kutengeneza vema itikadi na kujenga hamasa za kidini.
Sheikh Kaporo alisema, makongamano kama haya yafaa yawe mengi katika mwaka na kwamba yatasaidia kupeleka Uislamu wetu mbele.
Kwa upande wake, Sheikh Abdul-Qadir Al–Ahdal, Rais wa Taasisi ya Al– hikma Foundation alisema kongamano la Misk ya Roho ni zuri kwa sababu inaongelewa Qur’an.
Alisema, Waislamu waliohudhuria wamepata faida kubwa. Sheikh Al–Ahdal aliwataka Waislamu warudi katika Qur’an na kuifuata ili wawe na tabia za Qur’an, kama ilivyokuwa kwa kiigizo chetu Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).
Ukiacha wanazuoni hao, mmoja wa wasomi wa Kiislamu, Pazi Mwinyimvua alisema yeye kama muhudhuriaji amepata faida kubwa.
Pazi alisema: “Tumepata faida nyingi… tumekutana tumekumbushana. Yale mawaidha kwa kweli yamesaidia kutuongezea uhai katika nafsi zetu kwa kuwa tunajua katika haya maisha ya Duniani tunashindana na Iblisi anayetaka kututoa katika njia iliyonyooka.”
Katika waliohudhuria kongamano hilo alikuwepo pia Sheikh Hassan Abasi Semkuya Shemashilu, Imamu wa Msikiti wa Ijumaa Gongo la mboto mwisho na Amiri wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam, ambaye alisifu mada kuu ya kongamano hilo.
Aidha, aliisifu na kuishukuru Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) kwa juhudi zake za miaka mitatu mfululizo ya kuandaa makongamano makubwa ya Afrika Mashariki.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na watu takriban 5,000 wanaume kwa wanawake, huku walemavu wakipewa upendeleo maalumu kwa kukaa mbele eneo la VIP. Baadhi ya washiriki waliambatana na familia zao.

0 Comments