Watu 20 wauawa India katika maandamano ya kupinga sheria ya kuwabagua Waislamu

Watu wengine 10 wameuawa katika maandamano ya kupinga sheria iliyo dhidi ya Waislamu nchini India na kufanya idadi ya waliouawa hadi sasa tangu yalipoanza maandamano hayo kufikia watu 20.
Maandamano hayo yameendelea tena leo katika maeneo mbalimbali ya India kwa siku kadhaa mtawalia licha ya ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo.
Mauaji hayo yametokea wakati baraza la mawaziri chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Narendra Modi lilitarajiwa kukutana leo kujadili hali ya usalama nchini humo kufuatia kushadidi maandamano ya kupinga sheria ya uraia.
Maandamano hayo yanayowashirikisha maelfu ya raia nchini India yamepigwa marufuku katika sehemu mbalimbali za mji mkuu wa nchi hiyo New Delhi na katika majimbo ya Uttar Pradesh na Karnataka.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, miji 11 ya India inashuuhudia maandamano hayo katika nchi hiyo yenye Waislamu milioni 200.
Maandamano hayo yameshadidi katika hali ambayo, kufikia Januari 22 mwakani, Mahakama Kuu ya India inapaswa kutangaza msimamo wake kuhusiana na sheria hiyo iliyopasishwa hivi karibuni na Bunge.
Sheria hiyo inaruhusu kupatiwa uraia wahajiri wa jamii za Wahindu, Mabudha na hata Wakristo wanaotokea katika nchi jirani za Pakistan, Bangladesh na Afghanistan, huku ikizuia kupewa uraia Waislamu wanaotoka katika nchi hizo.

0 Comments