Watu wengine watatu wauawa India katika maandamno ya kupinga sheria tata dhidi ya Waislamu

Watu wengine watatu wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika maandamano ya kupinga sheria iliyo dhidi ya Waislamu nchini India, huku taasisi za kimataifa, nchi na shakhsia mbalimbali duniani wakiendelea kukosoa hatua ya kupasishwa sheria hiyo tata.
Aidha maelfu ya watu wanaripotiwa kutiwa mbaroni na vikosi vya usalama vya nchi hiyo katika maandamano yanayoongezeka kila siku nchini India ya kupinga sheria hiyo. Mauaji hayo yanatokea siku chache tu baada ya raia wengine wasiopungua sita kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika maandamano hayo.
Maandamano hayo yanayowashirikisha ya raia nchini India yamepigwa marufuku katika sehemu mbalimbali za mji mkuu wa nchi hiyo New Delhi na katika majimbo ya Uttar Pradesh na Karnataka.
Huduma zote za simu zilisitishwa katika baadhi ya maeneo ya mji mkuu New Delhi, karibu na eneo ambalo maandamano hayo yalikuwa yakifanyika. Kumekuwa na mfululizo wa maandamano kwa siku kadhaa sasa nchini India, huku siku zingine zikijawa na vurugu kali.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, taharuki imetanda nchini India hususan katika majimbo ya kaskazini mwa nchi hiyo, huku maandamano ya kupinga sheria hiyo ya kibaguzi iliyopasishwa hivi karibuni na Bunge la nchi hiyo yakishtadi.
Sheria hiyo inaruhusu kupatiwa uraia wahajiri wa jamii za Wahindu, Mabudha na hata Wakristo wanaotokea kkatika nchi jirani za Pakistan, Bangladesh na Afghanistan, huku ikizuia kupewa uraia Waislamu wanaotoka katika nchi hizo.

0 Comments