Waziri Mkuu wa Pakistan akosoa vikali muswada wenye utata wa serikali ya India dhidi ya Waislamu

Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan amesema kuwa kupasishwa muswada nchini India ambao unawapa uraia watu wasiokuwa Waislamu, ni ukiukaji wa haki za binaadamu.
Imran Khan ameyasema hayo wakati akikosoa vikali siasa za serikali ya New Delhi kuwalenga Waislamu nchini India na kubainisha kwamba kupasishwa muswada huo, kuna maana ya kuwafukuza Waislamu na kuiunga mkono jamii ya Wahindu wenye misimamo ya kuchupa mipaka katika jamii ya nchi hiyo. Hivi karibuni serikali ya India iliwasilisha muswada wenye utata katika bunge la nchi hiyo ambao kwa mujibu wake, wahajiri wanaotoka nchi jirani na ambao sio Waislamu, watastahiki kupewa uraia. Serikali ya New Delhi imetangaza kwamba itawapa hifadhi watu wasiokuwa Waislamu wanaokimbia kutoka nchi jirani kama vile Pakistan, Bangladesh na Afghanistan kuelekea nchi hiyo. Sheria hiyo tayari imepasishwa na bunge hilo.

Vyama vya upinzani vinasema kuwa muswada huo ni sehemu ya siasa za chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) kinachoongozwa na Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India kwa ajili ya kuwafukuza Waislamu kutoka nchi hiyo. Kabla ya hapo, serikali ya Modi iliwasilisha muswada huo bungeni dhidi ya Waislamu mwaka 2016, hata hivyo ulifutwa kutokana na upinzani mkali wa mikoa ya kaskazini mashariki mwa India ambayo inaundwa na jamii za makabila na dini tofauti. Kwa mujibu wa sheria ya India, ni marufuku kuwapa uraia wahajiri haramu.

0 Comments