02-Swalaah - Kuwajibika Na Fadhila Zake: Kusisitizwa Kwake na Malipo yake

Swalaah – Kuwajibika Na Fadhila Zake

02- Kusisitizwa Kwake na Malipo yakeHakika Swalaah ‘ibaadah muhimu na tukufu katika Uislamu kwa dalili zifuatazo: 

Swalaah Ni Nguzo Ya Dini:


عن معاذِ بن جبلٍ رضي الله عنه (( ...ألا أُخْبِرُكَ بِرَأسِ الأمْرِ وَعَمودِهِ وَذِرْوَةِ سَنَامِهِ؟)) قلتُ: بَلىَ يا رسول الله. قال:  رَأْسُ الأمْرِ الإسلامُ، وعَمُودُهُ الصَّلاةُ، وَذِرْوَةُ سَنَامِهِ الجِهادُ))
رَوَاهُ التِّرْمِذِيُّ وَقَالَ: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ  ٌ
Kutoka kwa Mu'aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhu) ((…Tena akasema: Je, nikwambie kilele cha hilo jambo; nguzo yake na sehemu yake ya juu kabisa?))  Nikasema: Ndio ee Rasuli wa Allaah.  Akasema:  ((Kilele chake ni Uislamu, nguzo yake ni Swalaah na sehemu yake ya juu kabisa ni Jihaad)) [At-Tirmidhiy na Hadiyth Hasan Swahiyh]

Hivyo inapoanguka nguzo huanguka kile kilichojengewa nacho nayo ina maana ni Dini yake mtu kwani bila ya kuswali ni kama kafiri kutokana na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) itakayotajwa katika hukmu ya mwenye kuacha Swalaah.
   

Swalaah Ni Jambo La Kwanza Kuulizwa Na Kuhesabiwa Siku Ya Qiyaamah:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ َقَالَ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ ((إِنَّ أَوَّلَ مَا يُحَاسَبُ بِهِ الْعَبْدُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنْ عَمَلِهِ صَلاتُهُ فَإِنْ صَلُحَتْ فَقَدْ أَفْلَحَ وَأَنْجَحَ وَإِنْ فَسَدَتْ فَقَدْ خَابَ وَخَسِرَ فَإِنْ انْتَقَصَ مِنْ فَرِيضَتِهِ شَيْءٌ قَالَ الرَّبُّ عَزَّ وَجَلَّ انْظُرُوا هَلْ لِعَبْدِي مِنْ تَطَوُّعٍ فَيُكَمَّلَ بِهَا مَا انْتَقَصَ مِنْ الْفَرِيضَةِ ثُمَّ يَكُونُ سَائِرُ عَمَلِهِ عَلَى ذَلِكَ)) الترمذي و أبوا داود والنسائي وابن ماجه وأحمد

Imepokelewa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah  wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kitu cha kwanza kinachohesabiwa katika ‘amali za mja wa Allaah Siku ya Qiyaamah ni Swalaah zake. Zikiwa zimetimia, hapo tena atakuwa kaneemeka na kafuzu, na zikiwa zina kasoro atakuwa kaanguka na kala khasara. Ikiwa pana upungufu katika Swalaah zake za fardhi Allaah ‘Azza wa Jalla Atasema: “Tazama ikiwa mja wangu ana Swalaah zozote za Sunnah ambazo zinaweza kufidia zile zilizopungua, hapo tena ‘amali yake iliyobaki itaangaliwa hivyo hivyo)). [At-Tirmidhiy, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Ahmad]

Kwa hiyo kuacha Swalaah iwe ni   jambo la kumtia khofu kubwa Muislamu kwa kuwa ni kupata hasara siku ya Qiyaamah kwa kuacha kuswali.


Maswali ya kujiuliza kuhusu Swalaah:

 • Unaswali?
 • Unaziswali Swalaah zote kwa wakati wake?
 • Unaziswali kwa twahara iliyokamilika na wudhuu uliotekelezeka vizuri?
 • Unaelekea Qiblah? Unaweka Sutrah mbele yako?
 • Nguo na sehemu unazoswalia ni safi hakuna najisi yoyote wala si isbaal; hazibururi kwa kuvuka mafundo ya miguu?
 • Unaswali mahali au nyumba isiyotundikwa picha za viumbe?
 • Unaswali Jamaa’ah Msikitini? (Swalaah kwa wanaume).
 • Unaswali kwa kutimizia kila kitendo cha Swalaah ipasavyo?
 • Unasoma Qur-aan kwa kuzingatia maana yake?
 • Unaswali kwa khushuu’ (unyenyekevu) na twumaaninah (utulivu)?
 • Unaswali Swalaah za Nawaafil na Sunnah; Sunnah zilosisitizwa na zisositizwa, dhwuhaa, witr’ kwa ujumla Qiyaamul-Layl?  

Wasiya Wa Mwisho Wa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Ummah Wake:

Katika khutbah zake za mwisho aliwausia sana Swalaah akisema:

((...الصلاة الصلاة و ما ملكت أيمانكم))    أحمد وصححه الألباني

((…Swalaah, Swalaah na waliomiliki mikono yenu ya kuume)) [Ahmad na ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]


'Ibaadah Pekee Iliyofaradhiwa Katika Mbingu Ya Saba:

Swalaah ni nguzo pekee aliyoipokea Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mbingu ya saba katika tukio la Israa Wal-Mi'raaj. Na zilikuwa asili yake ni Swalaah khamsini kisha zikapunguzwa hadi zikafika tano. Hivyo thawabu zake ni khamsiyn katika mizani ingawa ni tano katika kuzitekeleza.

Sifa Ya Mwanzo Na Ya Mwisho Ya Waja Watakaofuzu:

Kwa jinsi Swalaah ilivyokuwa ni muhimu na tukufu mno, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ameanza kutaja Swalaah kwa waja Wake watakaofuzu na kupata Jannah ya Firdaws kwa kutekeleza na kudumisha Swalaah.
قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾
Kwa yakini wamefaulu Waumini.

الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾
Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea.

وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾
Na ambao wanajiepusha na mambo ya upuuzi.

وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿٤﴾
Na ambao wanatoa Zakaah.

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾
Na ambao wanazihifadhi tupu zao.

إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾
Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume basi hao hawalaumiwi.

فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾
Lakini atakayetaka kinyume ya hayo; basi hao ndio wapindukao mipaka.

وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٨﴾
Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga.

وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٩﴾
Na ambao wanazihifadhi Swalaah zao.

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾
Hao ndio warithi.

الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾
Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu. [Al-Muuminuwn: 1-11]


Kwa hiyo, nani basi miongoni mwa Muumini asiyetaka kuipata Jannah ya Al-Firdaws iliyo juu kabisa karibu na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu tu ya kuacha Swalaah? Ibaadah ambayo haimchukui mtu muda mwingi  kuitekeleza?

0 Comments