Kulingamana Sawa 'Istiqaamah' (Riyaadhus Swaalihiyn)

Kutoka Katika Kitabu ‘Riyaadhus Swaalihiyn

Imekusanywa na ‘Abdallaah Mu’aawiyah


1-   KULINGAMANA SAWA 'ISTIQAAMAH'"Istiqaamah" ni mtu kuthibiti juu ya Shari’ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama Alivyoamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kumtakasia nia Allaah:

« فاستقم كما «أمرت »
« Basi simama sawasawa kama ulivyoamrishwa »

Anayesemeshwa hapa ni Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na kauli inayoelekezwa kwa Mtume hukusudiwa yeye na umma wake isipokuwa kama kutakuwepo dalili inayoonyesha kuwa kauli hiyo inamhusu yeye tu. Na kama hakuna dalili, basi kauli hiyo itakuwa ni yake na ya umma wake.

Kila mmoja ni lazima asimame sawa kama alivyoamriwa. Asibadili chochote katika Dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na wala asizidishe kitu wala asipunguze. Na kwa ajili hiyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema katika Aayah nyingine:

« واستقم كما أمرت ولا تتبع أهواءهم »
» Na simama sawasawa na wala usifuate matamanio yao «

« إن الذين قالوا ربنا الله ثم استقاموا تتنزل عليهم الملائكة ألا تخافوا ولا تحزنوا وأبشروا بالجنة التي كنتم توعدون ۞ نحن أولياؤكم في الحياة  الدنيا وفي الآخرة ولكم فيها ما تشتهى أنفسكم ولكم فيها ما تدعون ۞ نزلا من غفور رحيم ».

»Hakika waliosema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika (wakawaambia): Msiogope wala msihuzunike, nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa ۞ Sisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na Akhera, na humo mtapata kinachotamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyovitaka ۞ Ni takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwingi wa kurehemu «

« ربنا الله »
Muumbaji wetu, Mmiliki wetu na Mwendeshaji mambo yetu. Nasi tunamtakasia.
« ثم استقاموا »
Juu ya hilo, yaani neno lao: Mola wetu ni Allaah na wakaitekeleza shari’ah Yake.

Hawa waliosifika kwa sifa hizi mbili:
« تتنزل عليهم الملائكة »
Malaika baada ya Malaika
« ألا تخافوا ولا تحزنوا »
Yaani Malaika wanawateremkia kwa amri ya Allaah katika kila sehemu inayoogopesha na hususan wakati wa kufa wakiwaambia:
« ألا تخافوا ولا تحزنوا »
Msiogope katika mambo yenu mnayoyaelekea, wala msihuzunike kwa mambo yenu yaliwowapita.
« وأبشروا بالجنة التي كنتم توعدون »
Bishara ni kuelezea jambo lenye kufurahisha. Na hakuna shaka kuwa mwanadamu kunamfurahisha yeye kuwa ni katika watu wa peponi. Na kila mwenye kusema: "Mola wangu ni Allaah kisha akalingamana sawa juu ya Dini ya Allaah, basi huyo ni katika watu wa peponi.
« نحن أولياءكم في الحياة الدنيا والأخرة »
Malaika ndio walinzi wa wale waliosema: "Mola wetu ni Allaah", kisha wakalingamana sawa katika maisha ya duniani; huwaweka sawa, huwaongoza ya haki na huwasaidia. Pia vile vile huko Akhera, Malaika watawapokea siku ya kufufuliwa na kuhesabiwa wawaambie:
« هذا يومكم الذي كنتم توعدون »
« ولكم فيها ما تشتهي أنفسكم ولكم فيها ما تدعون »

« لكم فيها »
Yaani Akhera
« ما تشتهي أنفسكم »
Na hii ni katika neema za peponi, kwa vile peponi kuna vile ambavyo nafsi inavitamani na macho kuburudika.
« ولكم فيها ما تدعون »

Yaani mnavyovitaka, bali watapata zaidi ya hivyo.
« لهم ما يشاءون فيها ولدينا مزيد »
Yaani watapata zaidi ya wanavyovitaka na kuvitamani.
« نزلا من غفور رحيم »
Yaani peponi ndio mashukio yao na makaribisho toka kwa Mwingi wa kughufiria daima na Mwingi wa kurehemu daima.

Haya ndiyo malipo ya wale waliosema: "Mola wetu ni Allaah, kisha wakalingamana sawa.”
Na katika haya, kuna dalili juu ya umuhimu wa kulingamana sawa juu ya Dini ya Allaah kwa kushikamana mtu vyema, hazidishi wala hapunguzi wala habadilishi wala hageuzi.

Ama yule anayevuka mipaka au akajiweka mbali na Dini ya Allaah, au akabadili, basi huyo si mwenye kulingamana sawa juu ya Sharia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Na kulingamana ni lazima kuwe na uwastani katika kila kitu ili mtu awe ni mwenye kulingamana sawa.

………………………………..
……………….HADIYTH

Imepokelewa toka kwa Abu 'Amri na inasemekana kuwa ni Abu 'Amrah Sufyaan bin ‘Abdillaah Allaah Amridhie akisema:

قلت: يا رسول الله قل لي فى الإسلام قولا لا أسأل عنه أحدا غيرك: قال: (( قل آمنت بالله ثم استقم))
"Nilisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niambie mimi katika Uislamu kauli ambayo simuulizi mwengine yeyote zaidi yako wewe. Akasema: ((Sema: Nimemwamini Allaah, kisha lingamana sawa)).
Imepokelewa na Muslim.


SHARH

- Neno lake:
Niambie mimi katika Uislamu kauli ambayo simuulizi mwingine yeyote zaidi yako;
Niambie mimi kauli ambayo simuulizi mwingine yeyote zaidi yako iwe ni kipambanuzi na ya mwisho isiyohitajia kumwuuliza tena yeyote. Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
"Sema: Nimemwamini Allaah, kisha lingamana sawa".

- Neno lake:
Sema nimeamini;
Makusudio si tu kusema kwa ulimi, kwani kuna watu wanaosema: "Tumemwamini Allaah na siku ya mwisho nailhali wao si wenye kuamini". Lakini makusudio ya hilo ni kutamka kwa moyo na ulimi vile vile.
Na kwa ajili hii, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema huku anawalingania watu kuingia Uislamu:
"Enyi watu! Semeni: Hapana mola mwingine ila Allaah, mtafaulu".

- Neno lake:
Nimemwamini Allaah
Inakusanya kuamini kuwepo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), Umola Wake, Majina Yake, Sifa Zake, Hukumu Zake, na yote yanayokuja kutoka Kwake. Ukiamini hivyo, basi lingamana sawa juu ya Dini ya Allaah wala usijiweke kando nayo; si kulia wala kushoto, usipunguze wala usiongeze.
Lingamana sawa juu ya shahada ya kuwa hapana mola mwengine ila Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, na hiyo ni kwa kumtakasia Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kumfuata Mtume Wake.
Lingamana sawa juu ya Swalah na juu ya Zakaah, Swawm, Hijja na juu ya shari’ah zote.

- Neno lake:
Nimemwamini Allaah kisha lingamana sawa
Ni dalili kwamba kulingamana sawa hakuwi ila baada ya kuamini na kwamba kati ya masharti ya kuswihi na kukubaliwa matendo mema, ni kuwa yawe yemejengewa juu ya imani.TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HADIYTH HII

Ni kuwa, inatakikana kwa mtu anapofanya tendo lolote, ahisi kwamba amelifanya kwa ajili ya Allaah, na kwamba yeye analifanya kwa msaada wa Allaah, na kwamba yeye analifanya kwa kufuata Shari’ah ya Allaah. Hii ni kwa vile, mtu huyu halingamani sawa juu ya Dini ya Allaah ila baada ya kumwamini Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

0 Comments