Idadi ya vifo yafikia watu 20 vurugu za New Delhi

Idadi ya vifo kutokana na maandamano ya kupinga sheria mpya ya uraia mjini New Delhi, imepanda hadi watu 20.

Ghasia hizo ambazo ndizo mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika mji huo mkuu wa India katika miongo mingi, zilianza Jumapili jioni lakini zikaongezeka Jumatatu wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipowasili New Delhi kufanya mazungumzo na viongozi wa India.

Hospitali kuu ya mjini humo imethibitisha idadi hiyo ya vifo ikisema kuwa iliwapokea watu 189 waliopata majeraha. Polisi 40 ni miongoni mwa waliojeruhiwa.

Sheria hiyo mpya inarahisisha mchakato wa kutoa vibali vya uraia kwa jamii za kidini za walio wachache kutoka nchi jirani zenye raia wengi Waislamu, lakini orodha hiyo inawatenga Waislamu.

Wakosoaji wa sheria hiyo wanasema inawabagua Waislamu wa India walio wachache. Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ametoa wito wa kurejeshwa utulivu akisema kuwa amani na maelewano ndio utamaduni wa nchi hiyo.

0 Comments