Corona ilivyoathiri misafara ya Umrah, yatishia Hijja

Wakati Saudi Arabia ikitangaza kusimamisha kupokea wageni wa Mwenyezi Mungu wanaoingia nchini humo kwa ajili ya ibada ya Umrah kwa sababu ya ugonjwa wa corona, wasiwasi umeenea juu ya uwezekano wa marufuku hiyo ikaendelea hadi kipindi cha Hijja pia na mwezi wa Ramadhan.
Hata hivyo, ukweli kwamba kuna miezi takriban mitano kabla ya kufika mwezi wa Dhul-Hijja, unafanya watu wawe na matumaini kuwa ifikapo kipindi upepo wa homa ya corona utakuwa umepita.
Tayari katika nchi kadhaa watu wameshaanza kujiandikisha kwa ajili ya Hijja ya mwaka huu.
Wakati mahujaji watarajiwa wakijipa matumaini kuwa muda bado ni mrefu na kuna uwezekano mkubwa wa corona kudhibitiwa, ni Waislamu ambao walipanga kwenda Umrah mwezi wa Ramadhan ndio wapo hatarini zaidi kukosa safari hiyo.
Chini ya miezi miwili imebaki kabla ya Ramadhan kuingia, mwezi ambao thawabu za kufanya Umrah ndani yake zimefananishwa na fadhila za Hijja.

Misafara ya Umrah iliyokwama

Tayari Waislamu, hususan wale ambao tayari walishalipa fedha zao na kujiandaa kwenda Makka kwa ajili ya Umrah duniani kote katika kipindi hiki wameanza kupata machungu ya marufuku hiyo iliyoletwa na ugonjwa wa corona, ambayo pia imeathiri watalii waliopanga kwenda nchini humo kutoka katika nchi zilizoathirika.
Marufuku ya safari ya Umrah inakadiriwa kuwa italazimisha mamilioni ya Waislamu na watalii kuahirisha safari zao za Umrah mpaka ugonjwa wa corona utakapodhibitiwa.
Kuanzia Pakistan, hadi india, Indonesia, Malaysia, Ulaya na Afrika – kuna simulizi nyingi za watu wali hifadhi fedha kwa muda mrefu wakijipanga kwa safari hii ambao wamejikuta wakishindwa kusafiri.
Uamuzi wa kuweka marufuku ya kupokea wageni inakadiriwa kuwa itaathiri mamilioni ya Waislamu kutoka pande zote za dunia.
Mkazi mmoja wa Palestina, Ibrahim al-Dabba amesema amekuwa akitunza fedha kwa ajili ya safari hii muhimu ambayo ingempa fursa walau ya kutoka katika maeneo ya Ukanda wa Gaza yenye maisha magumu kutokana na ukaliaji wa kimabavu wa Israel.
Jijini Kano, Nigeria mamia ya abiria waliokuwa tayari Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mallam Aminu wakielekea Saudi Arabia walijikuta safari yao inaishia hapohapo baada ya kutangaziwa kufutwa kwa safari hiyo kutokana na marufuku hiyo. Hali kama hiyo imewatokea pia abiria wengi katika nchi mbalimbali wakiwamo Waislamu 40 kutoka wilaya ya Mahisagar ambao walifika katika jiji la Ahmedabad kupanda ndege ya kuelekea Jeddah, lakini wakaambiwa hakuna safari, walau kwa sasa.

Tahadhari Tanzania

Wakati hayo yakiendelea, hapa nchini Mkurugenzi wa taasisi ya kusafirisha mahujaji na waendao Umrah, Peace Travel & Khidmat Islamiya, Sidik Osman amewatahadharisha Waislamu kuacha kufanya miamala yoyote kwa sasa inayohusu safari za Umra badala yake wasubiri mpaka hapo taarifa mpya itakapotoka.
Lakini amewashauri Waislamu kuendelea kujisajili kwa safari za Hijja kwani ibada hiyo bado iko mbali na huenda mambo yakawa mazuri na watu wakaruhusiwa kwenda kufanya ibada hiyo muhimu huko Makka.
Osman alisema, ameamua kutoa rai hiyo ili kuwatahadharisha Waislamu dhidi ya watu wenye nia mbaya wanaoweza kuchukua amana za watu na kutumia katika mambo mengine.

“Kwa sasa hivi huwezi kwenda Umrah mpaka taarifa mpya itakapotoka. Mifumo yote ya visa imefungwa, hata huko ubalozini nako visa hazitolewi. Sasa wanapopokea fedha za mahujaji atapata wapi visa ya kumpeleka huyo hujaji?” alihoji Osman.
Tangu kutokea kwa mlipuko wa virusi vya Corona mwezi Desemba 2019, zaidi ya watu 92,819 duniani, kutoka katika mataifa takribani 80 tayari wameshaambukizwa virusi hivyo huku watu 3,164 wakiwa wameshafariki Iran (ambayo imetenganishwa na Saudia kwa mkondo mwembamba wa bahari) mpaka sasa imesharipoti zaidi ya vifo 77 ambayo ni namba kubwa zaidi ya watu kwa mataifa ya nje ya Uchina.
Hata hivyo vifo hivyo vinatokana na wagonjwa 2,336, hali ambayo inawafanya madaktari wa magonjwa ya kuambukiza kuhofia kuwa nchi hiyo inaweza kuwa na wagonjwa wengi zaidi inaowaficha.
Barani Ulaya hali ni mbaya zaidi ambapo nchini Italia mpaka sasa watu zaidi ya 400 wamethibitika kuambukizwa ugonjwa huo.
Kwa Afrika ni nchi mbili mpaka sasa zimethibitisha kuingia kwa ugonjwa huo. Algeria imeripoti wagojwa watano huku Misri ikiripoti wagonjwa wawili.

0 Comments