Faida za kunywa maji kabla ya kula chochote

Ni wazi kuwa sote tumeshapata kusikia msemo unaosema ‘maji ni uhai.’ Msemo huu ni sahihi kabisa kwani viumbe vyote vilivyo hai vinahitaji maji katika kuendesha shughuli zote zinazopelekea kuwepo kwa uhai.
Mbali na kuwa maji ni uhai, lakini pia maji yanaweza kuwa tiba nzuri ya kujikinga na baadhi ya maradhi ikiwa yatatumiwa katika utaratibu maalumu.
Mpenzi msomaji, fahamu kwamba miili yetu inaundwa na zaidi ya asilimia 70 ya maji, hivyo ni muhimu kunywa maji ya kutosha ili kuufanya mwili kufanya kazi vyema. Iwapo mwili wako hautapata maji ya kutosha, unaweza ukapata madhara mbalimbali ya muda mfupi na muda mrefu kama vile magonjwa ya shinikizo la damu, saratani pamoja na magonjwa ya figo. Ndugu msomaji, katika makala ya leo tutaangazia kwa undani faida mbalimbali zinazopatikana pale mtu anapokunywa maji kabla ya kula kitu chochote, yaani pale unapoamka asubuhi.

Faida za kunywa maji kabla chochote

Huondoa sumu mwilini

Unywaji wa maji mengi husaidia kuondoa sumu mwilini kwani huwezesha viungo kama vile figo kufanya kazi yake vyema. Unapokunywa maji kabla ya kula chochote asubuhi utauwezesha mwili wako pia kujenga misuli na kuzalisha seli mpya za damu.

Huboresha metaboli

Metaboli ni mchakato ambao mwilli hutumia vyakula (wanga, protini na mafuta) ili kupata nguvu na kujijenga. Hivyo basi, unywaji wa maji huwezesha mchakato huu kwenda vyema na kuufanya mwili kuwa na afya njema. Kunywa maji kabla ya kula chochote unapoamka huufanya utumbo kuwa tayari kufyonza virutubisho.

Husaidia kupunguza uzito

Wapo watu wanaopenda kupunguza uzito wa miili yao kwani uzito mkubwa si jambo zuri kiafya. Ikiwa unakusudia kupunguza uzito, basi ni vizuri zaidi kutumia maji kuliko vinywaji vingine.
Elewa kuwa. Unapotumia vinywaji kama vile soda na juisi (sharubati) asubuhi vitachangia sana kuongeza uzito wako wa mwili kwani sukari iliyomo hugeuzwa mafuta na kusababisha kuongezeka uzito.

Huondoa kiungulia

Kunywa maji kutakusaidia kuzimua asidi inayopatikana tumboni ambayo ndiyo hupelekea tatizo la kiungulia. Sanjari na hayo unywaji wa maji hurahisisha na kuhimiza mchakato mzima wa umeng’enywaji wa chakula na kupelekea zoezi hili kutendeka kwa ufanisi wa hali ya juu.

Huboresha na kuimarisha ngozi

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kunywa maji takriban nusu lita kunarahisisha mzunguko mzuri wa damu katika ngozi. Hivyo basi, hali hii hupelekea kuondoa sumu mbalimbali katika ngozi na kuiacha ngozi yako katika hali nzuri kiafya.

Huhamasisha ukuaji wa nywele bora zenye afya

Upungufu wa maji mwilini una madhara makubwa sana kwa afya yako. Ni ukweli kabisa kuwa takriban robo ya uzito wa nywele zetu ni maji. Hivyo kutokunywa maji ya kutosha kutasababisha ukuaji duni wa nywele na pia kutafanya nywele hizo kuwa dhaifu na nyepesi na hivyo kupelekea kunyonyoka au kukatika kirahisi.

0 Comments