Hijabu isitiri na tabia

Moja ya amri kubwa kwa mwanamke wa Kiislamu ni kusitiri viwiliwili vyao kwa kuvaa hijabu ya kisheria. Kuvaa hijabu kwavmwanamke Muumini wa kweli si jambo la hiyari kwani ni Allah na Mtume wake ndiyo wameagiza.
Kwa upande wa pili, inawapasa wazazi na walezi kuwanunulia wake na mabinti zao mavazi muafaka ili watekeleze amri hii kila wanapotoka nje ya majumba yao. Makusudio ya amri ya kuvaa hijabu ni kuhifadhi utu na heshima ya mwanamke na kujitambulisha nafasi yake kijamii kama mja mtiifu aliye na amani. Pia hijabu inalenga kumuepusha mwanamke na kero za njiani.
Hijabu ni alama ya utakatifu na utaharifu wa jamii husika na ni moja ya silaha za kupambana na vichocheo vya uchafu wa zinaa na udhalilishaji wa kijinsia. Uovu ni moja ya sababu ya kuenea maradhi hatari, ikiwemo ukimwi.
Hata hivyo kiuzoefu, malengo ya wavaaji wa hijabu katika ulimwengu wa leo yanatofautiana. Wapo wanaovaa kwa malengo sahihi ya kutii amri ya Allah na kupata radhi zake huko akhera sambamba na kuheshimika katika jamii. Lakini kuna wanaolitumia vazi hili takatifu kwa malengo mabaya.
Baadhi wakiwa ndani ya hijabu, hujiingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani (uharamia) vikiwemo wizi, mashambulizi, utapeli na kuzua matukio mengi ya hatari. Lengo la wanawake hawa ni kuzidi kuiaminisha dunia kuwa Uislamu ni tishio na hivyo dunia haitakuwa na salama madhali Waislamu wapo. Wanawake hao wanalenga kuonesha kuwa vazi la Kiislamu limejaa balaa na ufisadi na hivyo si salama!
Pamoja na nia ovu ya kulipaka matope vazi la hijabu, wanachokiamini Waislamu wa kweli ni kile kile kilichoelezwa na Mola wao. Nacho ni kwamba, hijabu ni sitara iliyojaa hekima na ni agizo la Mjuzi wa kila kitu ambaye kabla hata ya kuwaumba, aliwajua wanadamu pamoja na mahitaji yao, ikiwemo sheria itakayowaongoza kufikia utu wao hapa duniani na maisha bora huko Akhera. Kwa jambo hili la kuchafua sifa ya vazi la hijabu, Waislamu tunamshtakia Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye ajuae atawafanya nini watu wa namna hiyo.
Lakini kuna watu wengine wanavaa lakini wa mekosa kujua mantiki na hekima nzima ya amri hii. Huvaa hijabu kisha wakajisahau kutengeneza tabia zinazoendana na hijabu.
Ikiwa mwanamke atavaa hijabu iliyotimiza masharti yake yote (mpaka niqab), lakini akawa mropokaji na kunyanyua sauti mbele ya wanaume, anaongea popote pamoja na mipasuko ya vicheko, tunasema, dada yetu hajaipa hijabu haki yake na wala haimfikishi kwenye makusudio ya sheria yaani uchamungu.
Kwa mujibu wa nususi za Qur’an na Sunna, wanaume hawavutiwi na mwili na sura tu za wanawake. Sauti zao nyororo pia ni kivutio. Qur’an inasema: “ …ikiwa mwataka kuwa wachamungu,msilegeze sauti mnapoongea asijekuwa na tamaa (ya kufanya uchafu) ambaye ndani ya moyo wake kuna maradhi na mseme kauli njema” [Qur’an, 33:32].
Iwapo mwanamke anavaa hijabu vizuri lakini anasifikana kwa vitimbi anavyomfanyia mumewe, mke mwenzake ama watoto wake wa kambo kwa sababu za wivu mwingi, huyu ameshindwa kujua maana haswa ya kujisitiri. Hijabu ilitakiwa iathiri na tabia zake nazo kama ilivyoupamba mwili wake.
Makala yetu haina maana ya kukemea wivu, la-hasha. Tunaelewa kwamba wivu ukiwa katika mipaka yake kisheria ni sehemu ya maumbile na haukwepeki, si tu kwa watu bali hata kwa wanyama.
Tunachozungumzia hapa ni uadui unaofanywa na baadhi ya wanaotazamwa na jamii kwa jicho la matumaini kwa kuwa wamepambwa na hijabu wanazotoka nazo majumbani mwao; lakini kinyume na matarajio, jamii ikashuhudia vituko vya ajabu na vya hatari kutoka kwao ikiwemo dhidi ya waume zao, wake wenza, wakwe zao au watoto wa kambo. Inasemwa, mwanamke ni wivu, hata wake wa Mitume walikuwa nao! Hapana, wake wa Mitume walikuwa na wivu siyo uadui dhidi ya nafsi zao na za wenzao.
Ni kweli kwamba, wake wa Mitume (rehema za Allah na amani zimshukie), walikuwa na wivu mwingi na wakiudhihirisha haswa, lakini walipojisikia kuruka mipaka walikuwa tayari kuombana radhi yakaisha. Je, hivi leo kuna yoyote aliyeshikwa na shetani (wivu), akaharibu mambo, kisha akakiri makosa na kumuomba radhi mumewe au dada yake (mke mwenziwe)? Kama wapo ni wachache!
Wivu sahihi ni ule unaomfanya mume au mke kuwa mwema zaidi kwa mwenzake na kuwa mbunifu wa mbinu salama za vivutio vya kuupumbaza moyo wake ampende zaidi, lakini pamoja na kuchunga haki za wengine.
Mwanamke anayevaa hijabu na akawa anapenda kutoka, tena bila yasababu za msingi na kuhangaika majiani bila ridhaa na idhini ya mumewe, huwa ameshindwa kujua kwamba, hijabu ya kwanza ni nyumba yake na inamtosha midamu hapajakuwa na haja ya kutoka.
Kadhalika, kwa vile manukato pia ni moja ya vivutio, mwanamke kuvaa hijabu akatoka huku akinukia; hijabu hiyo haimsaidii kitu. Hivyo hivyo, kuonekana anavaa hijabu muda wote, Masha- Allah lakini katika minasaba, mathalan, ya sherehe za harusi huvua hijabu yake na kuonesha mapambo au sehemu zisizofaa kuonekana na wanaume, tunasema kwamba huyo ameikosea hijabu na kuidhulumu haki yake. Kama ameivaa kwa lengo la kutekeleza Uislamu alipaswa katika maeneo hayo ajisitiri zaidi.
Kwa kumalizia, mwanamke anayetaka kupata radhi za Allah Ta’ala, anapaswa kuzivika hijabu tabia na mwenendo wake wa kila siku kama anavyouvika mwili wake vazi hilo tukufu. Tunamuomba Allah atuongoze na awaongozee mama, dada, mabinti zetu pamoja na wanawake wote. Amin.

0 Comments