Maharusi wapitie mafunzo rasmi kabla ya ndoa

Moja ya jambo kubwa lililojitokeza katika habari ile ni umuhimu wa kuanzishwa kwa darasa za mafunzo maalumu ya ndoa misikitini. Maoni ya masheikh ya kutaka ziwepo darasa za ndoa yamekuja katika wakati muafaka kwani hivi sasa taasisi ya ndoa inakabiliwa na matatizo mengi.

[soma hapa pia : Masheikh Wataka Ndoa Zifanywe Nyepesi ]
Mmoja wa masheikh waliohojiwa, Abdurrahman Mhina maarufu kama ‘Baba Kiruwasha,’ alisema vijana wanaingia katika ndoa bila ya kuwa na elimu ya jambo hilo.
Baba Kiruwasha alisema, kabla ya kuingia katika ndoa vijana wanapaswa kufahamishwa mambo mengi ikiwemo maana ya ndoa, faida za ndoa, taratibu za maisha ya ndoa na maadili yake, changamoto zake na kadhalika. Elimu hii inapaswa kutolewa na masheikh wenye weledi huo.
Sheikh Kiluwasha alisema, kutokana na ukosefu wa elimu ya ndoa, vijana wameshindwa kuishi na wake zao na kupelekea talaka kutolewa kiholela, licha ya ndoa kufungwa kwa mbwembwe zote.
Sheikh Kiluwasha yupo sahihi sana kwani kila jambo lifanywalo linataka matayarisho. Matayarisho yanayotakiwa katika muktadha huu ni hii elimu ya maisha ya ndoa.

Tuirasmishe elimu ya ndoa

Si kwamba elimu ya ndoa haitolewi kabisa kwa vijana wanaooa, la hasha. Elimu hiyo inatolewa lakini sio katika namna rasmi na iliyopangiliwa vema na kwa mtaala maalumu.
Mara nyingi mafunzo yanayotolewa yanatokana na uzoefu tu wa wazee wa maisha ya ndoa au utaalamu wao wa mambo ya kimila (unyago). Ni nadra kukuta mafunzo ambayo msingi wake ni Uislamu.
Hali hiyo ni tofauti na wenzetu Wakristo ambao kabla ya kuingia katika ndoa huhudhuria mafunzo maalumu ya kuwaandaa bwana na bibi watarajiwa kwa maisha hayo mapya. Sisi hatufanyi hivyo, licha ya kuwa, yapo maarifa mengi ambayo maharusi wanastahili kupewa.
Waislamu tuna bahati sana kwani Mtume wetu Muhammad (rehema za Allah na amani zishukie) ambaye ni kiigizo chetu chema aliishi maisha ya ndoa na wakeze na yamerekodiwa ikiwa ni chanzo cha pili cha mafunzo ya dini yetu, baada ya maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyomo ndani ya Kitabu chake, Qur’an Tukufu.
Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Wabora wenu ni wale walio bora kwa familia zao; nami ni mbora wenu kwa familia yangu.” [Tirmidhy]. Katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Ibn Abbas, Mtume amesema: “Mbora wenu ni yule aliye bora kwa mkewe, na mimi ni mbora wenu kwa wake zangu.” [Sunan Ibn Majah].
Hadithi hizi zinathibitisha kuwa Mtume ni kiigizo chema; na kwamba kupitia maisha yake, Waislamu tunajifunza namna bora ya kua miliana na wenza wetu na watoto zetu na upi wajibu wa kila mmoja.

Mpango kazi wa mafunzo

Kama tunakubaliana kuwa mafunzo ni muhimu kwa wanandoa watarajiwa, kinachofuata ni taasisi zetu kubwa kama Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Sunna Tanzania (BASUTA) na Umoja wa Wanazuoni (Hayatul Ulamaa) kuliendea hili.
Katika kuliendea hilo, jambo muhimu la kwanza ni mtaala wa mafunzo hayo, kuamua kuhusu muda wa mafunzo, semina za walimu ambao watatoka katika misikiti na kisha kuyatangaza mafunzo hayo kwa umma. Kama suala hili haitashughulikiwa tutegemee ongezeko la ugomvi wa wandoa, vitendo vya kikatili, uasherati na talaka kila uchao. Talaka nazo zinazalisha shida nyingi za kimalezi ya watoto, jambo ambalo halifurahishi.

0 Comments