Masheikh wataka ndoa zifanywe nyepesi

Masheikh nchini wametoa tathmini yao juu ya taasisi kongwe ya ndoa, wengi wakisema inapitia wakati mgumu kwa sababu vijana wengi wameikacha na badala yake wanaishi na kuzaliana kiholela.
Kutokana na hali hiyo, Masheikh wameshauri hatua za haraka zichukuliwe ikiwemo jamii kurahisisha ufungishaji ndoa, uanzishwaji wa darsa za ndoa misikitini na Masheikh kuzungumzia suala hilo mara kwa mara kwenye hotuba zao.
Mmoja wa Masheikh hao, Abdurrahman Mhina maarufu kama ‘Baba Kiruwasha,’ amesema changamoto zinazoonekana sasa zinasababishwa na kutoipa umuhimu taasisi ya ndoa kwa sababu ya kutokuwa na elimu ya jambo hilo.
Baba Kiruwasha alisema, kabla ya kuingia katika ndoa vijana wanapaswa kufahamu faida, taratibu na maadili ya ndoa kupitia Masheikh wenye weledi huo.
Aliongeza kuwa kutokana na kukosa elimu ya ndoa, watu wameshindwa kuishi na wake zao na kupelekea talaka kutolewa kiholela, licha ya ndoa kufungwa kwa mbwembwe zote.
“Leo tunashuhudia talaka nyingi zinatolewa kwa sababu ya watu kutojua umuhimu wa ndoa na namna ya kuishi katika ndoa. Watu wanachukuana tu kwa utashi wao na ndio maana utasikia juzi tu mtu fulani amefunga ndoa lakini leo ameachika. Kwa nini? Kwa sababu mtu huyu aliingia katika ndoa bila ya matayarisho,” alisema.
Aliongeza kusema, Masheikh wanatakiwa kulipa kipaumbele suala la ndoa na kulizungumza kila leo katika mimbari zao kama wanavyofanya katika suala la utoaji wa sadaka.
“Ninachokiona ni kwamba, itafika wakati suala la kuoa litaonekana halina faida kabisa maana hivi sasa elimu haitolewi ya kutosha, na hivyo watu hawajui kwa nini wanaingia kwenye ndoa na wafanye nini katika ndoa,” alisema Sheikh huyo.
Baba Kiruwasha alisema: “Kwa sababu watu hawajui faida za ndoa, wamejikuta wakiishia kuoa kwa utashi wao bila kuzingatia sifa ambazo zimetangazwa katika vitabu. … itafuteni elimu popote pale ilipo ili mpate nusura. Na wazazi nao walee watoto wao katika maadili yanayompendeza Mwenyezi Mungu.”

Sheikh Muhammad Issa

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Sunna Tanzania (BASUTA), Sheikh Muhammad Issa alisema maendeleo ya sasa ya kidunia yameathiri sana taasisi ya ndoa.
Alisema, vijana wengi wana mitazamo ya kimagharibi na wanaishi maisha ya kuiga watu wa mataifa mengine, hali inayowapelekea kudhani kuwa ndoa haina faida yoyote.
Sheikh Muhammad alisema, kwa mujibu wa mitazamo ya kimagharibi mtu kuishi bila mume au mke ndio kawaida na ndio usasa.
Alisema fikra hizo zimeshamiri mno duniani na kuenea hadi hapa nchini. “Bahati mbaya mambo haya yameenea hadi hapa nchini. Sasa vijana wanaiga watu maarufu ambao wamewafanya kiigizo chao,” alisema kwa huzuni Sheikh Muhammad.
Tatizo jingine alilolitaja Sheikh Muhammad ni kutokuwekwa mkazo wa mafundisho ya dini katika ndoa, ikiwemo mafundisho ya kuifanya kuwa jambo jepesi hasa katika suala la mahari.
Alisema wazazi wanapofanya mahari kuwa kubwa, wanawaogopesha vijana wanaotaka kuoa.
Sheikh Muhammad alisema, kujenga familia bila kufuata misingi ya ndoa kunapelekea ongezeko la watoto wa mitaani waliokosa malezi mazuri na hivyo kupelekea baadhi yao kuangukia kwenye uhalifu.
Sheikh Muhammad pia alisema katika dunia ya sasa, zinaa imepewa fursa kubwa sana ukilinganisha na zamani. “Zamani kuzini lilikuwa ni jambo la kioja, lakini siku hizi hali ni tofauti. Wenyewe wanasema, kama ninapata mayai kuna umuhimu gani wa kufuga kuku? Ndio maana tunashuhudia hali hii sasa,” alisema Sheikh Muhammad.

Sheikh Barahiyan

Naye Sheikh Salim Barahiyan akiongelea suala hilo alisema, hivi sasa jamii ya Kiislamu inakabiliwa na tatizo kubwa. “Hatuwalei vijana wetu katika misingi ya dini hadi wamefikia hatua wanafanya mambo kwa utashi wao. Haya tunayoyaona leo nina wasiwasi yanaweza kuendelea kama hayatafanyiwa kazi,” alisema.
Sheikh Barahiyan alisema, wao wenyewe katika taasisi ya Ansaar Muslim Youth Centre (AMYC), waliliona hilo na hivyo wakaamua kuwafundisha vijana mambo muhimu kama hayo.

“Hivi ninavyokwambia juzi tu tumetoka kufungisha ndoa vijana wetu …. Ninachotaka kuwaambia, watu watafute elimu hiyo, wazazi pia wasibweteke, wawashughulishe watoto wao kuitafuta elimu ya namna hii ili tufuate maagizo ya Allah,” aliongeza kusema Sheikh Barahiyan.

0 Comments