Undani kuhusu virusi vya korona na athari zake

Bila shaka sote tumepata kusikia kuhusu mlipuko wa maradhi ya mafua huko nchini china yaliyosababishwa na virusi aina ya korona. Virusi vya korona ni moja kati ya familia ya virusi vinavyosababisha maradhi tofauti ya mfumo wa upumuaji hususan mafua na kikohozi.
Kama tulivyobainisha, virusi hawa wapo wa aina nyingi. Baadhi husababisha athari mbaya, na wengine athari ndogo tu.
Katika mlipuko wa sasa virusi vya korona aina ya COVID-19 vimegundulika kuwa chanzo cha mlipuko huu unaowaathiri sio binadamu pekee bali pia wanyama na ndege mbalimbali. Virusi hivi huweza kusababisha dalili tofauti kutegemeana na aina ya mnyama au ndege aliyeambukizwa.

Historia ya milipuko ya korona

Hii si mara ya kwanza kwa virusi vya korona kusababisha mlipuko wa maradhi ya mafua makali yasiyosikia dawa. Mlipuko wa kwanza ulitokea nchini China mwaka 2003 na kusababisha vifo 774. Mwaka 2012, mlipuko mwengine ulitokea katika nchi za Mashariki ya Kati na kusababisha zaidi ya vifo 400. Mlipuko mwengine ulifuatia mwaka 2015 na kusababisha vifo 36 na mwengine mwaka 2018 na kusababisha vifo 41.

Takwimu za sasa

Ni wazi kuwa mlipuko wa sasa wa korona ni mbaya zaidi kuliko milipuko yote iliyowahi kutokea huko nyuma ukiijumlisha pamoja. Mpaka sasa, zaidi ya visa elfu 77 vimethibitishwa na tayari wagonjwa 2,400 wamefariki dunia nchini China pekee. Mbali na kuathiri nchi ya Si China pekee iliyoathirika, bali visa vya ugonjwa huu na vifo vimeripotiwa pia katika mataifa mengine.

Kusambaa kwake

Inakadiriwa kuwa virusi hivi vilianza kusambaa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Baada ya binadamu wa mwanzo kuambukiz
wa, mlipuko ukatokea kwa sababu virusi hivi vinasambaa kirahisi kwa njia ya ya hewa na kuathori mfumo wa upumuaji.
Baada ya mtu kuvuta hewa yenye virusi hivi, huweza kukaa baina ya siku moja na wiki mbili kabla dalili kujitokeza zinazoashiria kuambukizwa na virusi vya korona.

Dalili zake

Kama tulivyosema, virusi hawa huathiri zaidi mfumo wa upumuaji hivyo hata dalili zake zinahusisha mfumo wa upumuaji. Miongoni mwa dalili zake ni pamoja na kikohozi, homa kali, kifua kubana pamoja na kukosa hewa. Pia virusi hawa huweza kusababisha homa ya mapafu (pneumonia) na kuharibu viungo vyengine vya mwili na mwisho kusababisha kifo.

Nini kifanyike ili kupunguza usambazaji

Ingawa mpaka sasa wanasayansi na wataalamu wa afya hawajafanikiwa kugundua chanjo cha ugonjwa huu, baadhi ya mambo yanaweza kufanyika ili kupunguza kuenea kwa virusi hawa.
Hatua ambazo zimeshachukuliwa ni pamoja na kuzuia muingiliano wa watu katika maeneo yenye mlipuko pamoja na kuwatibu wagonjwa katika hospitali maalum ambazo hazina muingiliano na wagonjwa wa maradhi mengine.

Tahadhari

Ni wazi kuwa mlipuko wa korona ni dharura ya kidunia. Hivyo basi, kila mmoja, kwa nafasi yake, anapaswa kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi haya. Tahadhari hizi ni pamoja na kuepuka kutembelea maeneo ambayo yanasadikiwa kuwa na visa vya ugonjwa huu na pia kuripoti mara moja kuhusiana na dalili za mafua ambayo hayaeleweki katika vyombo husika.

0 Comments