Wakati Mgumu Katika Historia Ya Kiislamu (Jinsi Ya Kuisoma Historia)

Imefasiriwa Na Muhammad Faraj


Namna Ya Kuisoma Historia
Tunapoisoma historia ya kiislamu, lazima tuisome kama vile tunavyosoma vitabu vya hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kwa sababu tunaposoma hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) huwa tunatafuta ukweli iwapo hadithi hizo ni sahihi au si sahihi.

Na hatuwezi kutambua ikiwa hadithi ni sahihi au si sahihi bila ya kuwajuwa wapokezi wa hadithi hiyo (narrators) pamoja na matni (maneno) yake, na hii ni kwa sababu katika elimu ya hadithi maulamaa wamechukuwa juhudi kubwa ya kuchunguza habari za wapokezi wake na wakaweza kuwajuwa yupi muongo na yupi mkweli miongoni mwao, yupi mwenye kusahau na yupi anayependa kuongeza maneno yake (kutia chumvi), kisha wakazichunguza hadithi na kuzidurusu na hatimaye wakaweza kupambanua baina ya hadithi sahihi na dhaifu pamoja na zile za uongo zilizopachikwa tu. Na kwa ajili hiyo wakaweza kuzisafisha hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa kuzibainisha zile za uongo zilizochomekwa na zile zilizo dhaifu.

Lakini tunaposoma vitabu vya historia (Taariykh), si rahisi mtu kuweza kutambua yote hayo, na hii ni kwa sababu utakuta ndani yake maelezo mengi yaliyoandikwa bila kutajwa majina ya wapokezi (narrators), tofauti na ilivyo katika vitabu vya elimu ya hadithi. Na mara nyingi maelezo hayo yanaambatanishwa na majina ya wapokezi yasiyokuwemo na yasiyojulikana katika vitabu vya elimu ya wapokezi wa hadithi. Kwa ajili hiyo si rahisi kujuwa iwapo wapokezi hao walikuwepo kweli, na kama walikuwepo kweli si rahisi pia kujuwa juu ya mwenendo wao kama walikuwa wakweli waaminifu au waongo wenye kupenda kuandika kila wanachosikia nk. Na kwa ajili hiyo ni vigumu sana mtu kuweza kutoa uamuzi juu ya maelezo hayo iwapo ya kweli au ya uongo.

Kwa hivyo katika kuisoma historia mambo ni magumu zaidi kuliko ilivyo katika kusoma vitabu vya elimu ya hadithi, lakini hii isitufanye kuyarahisisha mambo, bali ni wajibu wetu kuutafuta ukweli na kujuwa wapi tuitafute historia yetu.
Mtu anaweza kusema;
“Ikiwa tutavichambua vitabu vya historia na kuzitoa hadithi zisizo sahihi, basi maelezo mengi juu ya historia yetu yatapotea na kubaki machache tu”.

Lakini sisi tunamjibu kwa kumwambia kuwa; la, hayatopotea maelezo mengi, kwani yapo mengi katika maelezo ya historia yaliyoandikwa kwa isnadi zake, na hayo yamo katika vitabu vya historia mfano wa kitabu cha Atw-Twabariy na pia yamo ndani ya vitabu vya hadithi kama vile  Al-Bukhaariy na Musnad ya Imam Ahmad na Sunan At-Tirmidhiy au vitabu vilivyoandikwa na Ibni Abi Shaybah au katika vitabu vya tafsiri vinavyoandikwa ndani yake isnadi za kila riwaya kama vile tafsiri ya Ibni Jariyr na tafsiri ya Ibni Kathiyr na mara nyingine katika vitabu vinavyoandikwa juu ya matukio maalum kama vile vita vilivyotokea baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) n.k.

Na kama utashindwa kuupata ukweli, basi uamuzi utabaki pale  pale kuwa imani yetu ni kuwa haitupasi kuwatuhumu Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) kwani Allaah Subhanahu wa Taala amewasifia na kuwatakasa. Kwa ajili hiyo tukikutana na maelezo yoyote yale yanayowatuhumu Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) kwanza kabisa tunatizama isnadi ya wapokezi wa maelezo hayo (narrators), na kama isnadi ni sahihi, basi kabla ya kuwatuhumu tutizame kwanza tafsiri ya riwaya hizo na zinaleta maana gani? Ama ikiwa isnadi yake ni dhaifu, basi AlhamduliAllaah, na kama riwaya hiyo haina isnadi yoyote, basi tunarudi katika asili yetu nayo ni imani yetu kuwa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) ni watu waadilifu kama tutakavyoona kila tukiendelea mbele namna gani Allaah amewatakasa watu hawa.
Kwa hivyo tunapoisoma historia hatuna budi kuisoma kwa kuichambua vizuri kama tunavyofanya wakati tunaposoma vitabu vya elimu ya hadithi na hasa katika historia ya Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Tusome Vitabu Vilivyoandikwa Na Nani?
Wengi siku hizi wanapendelea kusoma vitabu vya historia  vilivyotungwa katika zama hizi zetu, vitabu ambavyo waandishi wake wanajishughulisha na upambaji wa maelezo au kusimulia habari zinazopotosha ukweli au yote mawili mfano wa vitabu vya ‘Abbaas Al Aqaad aliyeandika juu ya Ustadi ‘Abqariyaat’, au vitabu vilivyoandikwa na Khaalid Muhammad Khaalid ‘Khulafaa rasuul’ na ‘Rijaal haula rasuul’ au vya Taaha Husein ‘Mawqifat al Jamal’ au vya Georgie Zeidan ‘Taariykh tamadunil Islam’ au vingine vya mfano huo. Watungaji hawa wanapoandika juu ya historia hujishughulisha na uandishi na upambaji wa visa vilivyomo ndani yake bila kujali kama visa hivyo ni sahih au si sahihi, muhimu kwao ni kukuandikia kisa kizuri kinachovutia.
Kwa hivyo suali linarudi pale pale. ‘Nisome vitabu vilivyoandikwa na mwandishi gani?’

Ikiwa unao uwezo wa kuwachambua wapokezi (narrators) na na kuwajuwa wakweli na waongo miongoni mwao, basi soma kitabu cha Imam Atw-Twabariy, kwani yeye ni bingwa miongoni mwa waandishi wa Taariykh (historia), ama ikiwa huna uwezo wa kuwachambua wapokezi, basi soma kitabu cha Al Bidaya wal Nihaya kilichoandikwa na Ibni Kathir au kitabu cha Taariykh al Islam kilichoandikwa na Imam Al Dhahabi au kitabu kilichoandikwa na Abu Bakr bin al Arabi kiitwacho ‘Al Awasim minal Qawasim’, na hiki ni miongoni mwa vitabu vizuri sana vilivyoandika juu ya wakati huu mgumu.


Tujitahadharishe Na Nini?
Tunaposoma vitabu vya historia lazima tujitahadharishe tusije tukachukuliwa na rai ya mtungaji, kwani inatupasa tuwe waadilifu huku tukisoma, na hatuna budi kuziangalia riwaya zenyewe na si kuangalia rai ya muandishi, na hatuna budi pia kuwa na mambo mawii akili mwetu huku tukisoma vitabu vinavozungumza juu ya historia ya Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam);
La kwanza; ni kuwa na itikadi kuwa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni viumbe bora kupita wote baada ya Mitume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na hii ni kwa sababu Allaah Subhanahu wa Taala amewasifia na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pia amewasifia na akatuabainishia katika hadithi nyingi kuwa kuwa umma ule ulikuwa ni umma bora kupita zote baada ya Mitume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Jambo la pili; inatupasa tuelewe kuwa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hawakukingwa na kufanya makosa (si Maasumin), ndiyo sisi tunaitakidi kuwa hawawezi kufanya makosa katika jambo lolote walokubaliana nalo wote kwa pamoja (Ijamai), na hii ni kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikwishatuambia kuwa umma huu hauwezi kukubaliana wote kwa pamoja katika jambo la upotofu (upotevu), lakini unapowachukulia kama watu binafsi, wao hawakukingwa na kufanya makosa, kwani walokingwa ni Mitume wa Allaah peke yao, ama wengine wasiokuwa wao sisi hatuamini kuwa yupo yeyote aliyekingwa na kufanya makosa (asiyefanya makosa).

Kwa hivyo hatuna budi kuamini kuwa Maswahaba ni umma bora kupita umma zote na hatuna budi kuamini kuwa wao wanaweza kufanya makosa.

Kwa hivyo itakapokujia riwaya (maelezo) ambayo ndani yake mna lawama juu ya Sahaba basi usikimbilie kuikataa na pia usiikubali moja kwa moja mpaka kwanza uitizame vizuri. Utakapoona kuwa isnadi ya riwaya hiyo ni sahihi basi ujuwe kuwa hii ni katika yale mambo ambayo hawakukingwa nayo, ama ikiwa isnadi ya riwaya hiyo ni dhaifu, basi unarudi katika itikadi yetu ya asili nayo ni kuwa Maswahaba ni watu wema.

Ama sifa ambazo Allaah Amewasifia Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) ni katika aya ifuatayo;
“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na walio pamoja naye ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama kwa kurukuu na kusujudu (pamoja), wakitafuta fadhila za  Allaah na radhi (Yake). Alama zao zi katika nyuso zao kwa taathira (athari) ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati. Na mfano wao katika Injili (umetajwa hivi). Kuwa (wao) ni kama mmea uliotoa matawi yake; kisha (matawi hayo) yakautia nguvu, ukawa mnene ukasimama sawasawa juu ya kigogo chake, ukawafurahisha walioupanda ili awakasirishe makafiri kwa ajili yao. Allaah amewaahidi walioamini na kutenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa.”
Al Fat-h- 29
Katika aya hii Allaah Amewasifia Maswahaba wa Mtume wote kwa pamoja. Kwa hivyo asili ya itikadi yetu ni kuwasifia, na imepokelewa hadithi sahihi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) isemayo;
“Msiwatukane Maswahaba wangu, lau kama mmoja wenu atatoa dhahabu ukubwa wake mfano wa jabali la Uhud, basi haitofikia gao lao wala hata nusu yake”
 Al-Bukhaariy na Muslim

Hizi pia ni sifa ambazo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amewasifia Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhum), na tutaelezea kwa ufafanuzi zaidi tutakapoufikia mlango nilioutenga katika kitabu hiki niloupa jina la ‘Uadilifu wa Maswahaba’.
Kitabu muhimu kupita vyota katika elimu ya tarekh ni kile kilichoandikwa na Imam Atw-Twabariy na wengi wananukuu kutoka katika kitabu hicho. Ahlu Sunnah wananukuu kutoka katika kitabu cha ‘Taariykh Atw-Twabariy’, na Ahlul Bida’a (wanofuata madhehebu a ki Shia) pia wananukuu kutoka katika kitabu cha Taariykh Atw-Twabariy.
Ahlu Sunnah wanatoa hoja zao katika kitabu cha Taariykh Atw-Twabariy na Ahlul Bida’a wanatoa hoja zao kutoka katika kitabu cha Taariykh Atw-Twabariy.


Kwa Nini Kitabu Cha Taariykh Atw-Twabariy Kinapendekezwa Kuliko Vingine?
Kwa sababu nyingi zikiwemo zifuatazo;
1.     Kitabu cha Atw-Twabariy kimeandikwa wakati ulio karibu zaidi na matukio yenyewe.

2.     Imam Atw-Twabariy anahadithia pamoja na isnadi (majina ya wapokezi wa hadithi hizo).

3.     Utukufu wa Imam Atw-Twabariy pamoja na haiba na heshima yake kutokana na daraja yake ya elimu.

4.     Vitabu vingi vya historia vinanukuu kutoka kwake.

Kwa ajili hiyo na sisi tunapotaka kuisoma historia inatubidi tukiendee kitabu hicho cha Atw-Twabariy moja kwa moja. Lakini kama nilivyosema ni kuwa Ahlus Sunnah wananukuu kutoka kitabu hicho kiitwacho ‘Taariykh Atw-Twabariy’, na Ahlul Bida-a nao pia wananukuu kutoka katika kitabu hicho cha Taariykh Atw-Twabariy. Sasa vipi tutaweza kusawazisha baina ya hii na ile?
Tulikwishaelezea hapo mwanzo kuwa uzuri wa kitabu hiki cha Taariykh Atw-Twabariy ni kwamba hakiandiki juu ya hadithi isipokuwa lazima kitataja majina ya wapokezi wa hadithi hiyo (isnadi). Ahlus Sunnah wao wanachukuwa hadithi zilizo na isnadi sahihi katika kitabu hicho lakini Ahlul Bida-a wao wanachukuwa zilizo sahihi na zisizo sahihi, muhimu zikubalieni na matamanio ya nafsi zao.

Taratibu Alizotumia Imam Atw-Twabariy Katika Kuandika Kitabu Chake Cha Taariykh
Imam Atw-Twabariy Allaah amrehemu ametupumzisha sana katika jambo hili kutokana na utangulizi wa kitabu chake hicho, yareti wale wanaokisoma kitabu hiki cha Taariykh wangesoma utangulizi huo.
Anasema Imam Atw-Twabariy katika utangulizi wake;
“Ajue msomaji wa kitabu chetu hiki kuwa yote niliyoyaelezea humu yanatokana na maelezo niliyoyapokea kutoka kwa wasimulizi wa habari na nimejiwekea masharti ya kuandika isnadi (mlolongo wa majina ya wapokezi) ya yote yale walionihadithia.
Iwapo ndani ya kitabu changu hiki zimo habari zozote nilizozisimulia juu ya waliotangulia zisizompendeza msomaji au zitakazomuudhi msikilizaji, na habari hizo zikawa siyo sahihi, basi atambuwe msomaji au msikilizaji huyo kuwa habari hizo hazikutokana na sisi, isipokuwa sisi tumezifikisha vile vile kama tulivyofikishiwa”.
Nadhani Imam Atw-Twabariy kwa utangulizi wake huu amekutupia mzigo wewe msomaji, kama kwamba anakwambia;
“Ukikuta ndani ya kitabu changu hiki habari zisizokufurahisha au zisizokubalika, basi tizama kutoka kwa nani tumezipokea habari hizo. Na kama nilivyoahidi kuwa nitaandika majina ya wale walionipa habari hizo, kwa hivyo ukiona kuwa wale niliopokea kutoka kwao habari hizo ni watu wa kuaminika, basi zikubali, la kama si wa kuaminika basi usizikubali”.
Utaratibu huu ndio uliofuatwa na wengi kati ya waandishi wa vitabu vya elimu ya hadithi. Iwapo mtu atarudia na kusoma vitabu vya hadithi, ukivitowa vitabu vya  Al-Bukhaariy na Muslim, kwa sababu waandishi wa vitabu hivyo viwili wameahidi kuandika hadithi zilizo sahihi tu ndani yake. Lakini vitabu vingine kama vile Attirmidhy au Abu Daud au Addaraqutniy au Addarimiy au Musnad ya Imam Ahmad au kitabu chochote kingine katika vitabu vya elimu ya hadithi, utaona kuwa waandishi wake wanakutajia mlolongo wa majina ya wapokezi wa hadithi hizo (isnadi) kwa sababu wao hawakutoa ahadi ya kuandika hadithi zilizo sahihi peke yake, na kwa ajili hiyo wakawa wanakuandikia isnadi na unachotakiwa wewe ni kuziangalia isnadi hizo. Ikiwa wapokezi ni watu wanoaminika utazikubali, ama ikiwa si watu wa kuaminika, basi usizikubali.
Kutokana na utangulizi wake, Atw-Twabariy hakutoa ahadi ya kuandika yale yaliyo sahihi peke yake, isipokuwa ametoa ahadi ya kuandika majina ya wale ambao kutoka kwao amepokea maelezo hayo.
Ikiwa mambo yenyewe ni kama hivyo, basi Imam Atw-Twabariy hakutoa ahadi (ya kuandika hadithi zile sahihi tu). Na katika kitabu chake, Attabari amenukuu habari nyingi kutoka kwa mtu mmoja aitwae Luut bin Yahya, maarufu kwa jina la ‘Abu Makhnaf’.
Imam Atw-Twabariy amenukuu kutoka kwa Luut bin Yahya huyu, riwaya mia tano na themanini na saba. Na riwaya hizi zinaelezea kuanzia wakati alipofariki Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kumalizikia wakati wa ukhalifa wa Yazid bin Muawiya, na huu ndio wakati nitakaozungumza juu yake katika kitabu chetu hiki, zikiwemo habari za Saqiyfat Bani Saaidah, kisha cha Shuura, sababu zilizowafanya Khawarij wachukuwe msimamo dhidi ya ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) na hatimae kuuliwa kwake, ukhalifa wa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), vita vya ‘Al Jamal’, vita vya ‘Siffin’, kuhukumu, (Tahkiym), vita vya Naharawan, ukhalifa wa Mu’aawiyay (Radhiya Allaahu ‘anhu), kuuliwa kwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhum). Katika yote haya utazikuta riwaya zilizosimuliwa na Abi Makhnaf, riwaya ambazo Ahlul Bida-a ndiyo wanaozitegemea sana na kuzishikilia.
Na si Abu Makhnaf peke yake mwenye riwaya za uongo, isipokuwa tu, Abu Makhnaf ni mashuhuri kupita wenzake, lakini wapo wengine waongo kama yeye kama vile Al Waaqidiy ambaye katika elimu ya hadithi anajulikana kuwa ni muongo ambaye hadithi zake hazikubaliwi, juu ya kuwa yeye ni mjuzi wa riwaya nyingi na mtaalamu wa historia, isipokuwa si mtu mwaminifu wa kufikisha habari.
Wa tatu ni Seif bin ‘Umar At Tamimi ambaye pia ni mtaalamu wa historia maarufu, isipokuwa naye pia si muaminifu wa kufikisha habari na anajulikana kuwa ni mtu muongo na hadithi zake hazikubaliwi.
Yupo mwingine pia aitwae Al Kiliy ambaye ni muongo mashuhuri, na kwa ajili hiyo mtu inampasa achunge asije akazikubali riwaya zilizosimuliwa na watu wa aina hii.
Turudi kwa Abu Makhnaf na tutazame maulamaa wamesea nini juu yake.
Ibni Maiyn ambaye ni mwanachuoni maarufu wa elimu ya wapokezi wa hadithi amesema;
“Abu Makhnaf si mwenye kuaminika”.
Na Abu Hatim amesema;
“Abu Makhnaf hazikubaliwi riwaya zake”.
Na Imam Ad Daraqutny amesema;
“Abu Makhnaf ni dhaifu”.
Imam Adhahabi amesema;
“Mwingi wa habari na mtungaji wa maneno asiyeaminika”.
Na wewe unapokifungua kitabu cha Taariykh ya Atw-Twabariy na ukakumbana na riwaya inayowalaumu Maswahaba wa Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kisha ukaona kuwa Atw-Twabariy amezinukuu habari hizi kutoka kwa Abu Makhnaf, basi ni juu yako kuziweka upande habari hizo. Kwa nini? Kwa sababu ni riwaya iliyosimuliwa na Abi Makhnaf.
Na Abu Makhnaf huyu amekusanya riwaya nyingi zenye mambo ya Bida-a ndani yake na za uongo.


Njia Zinazotumiwa Na Waletao Habari Katika Kuipaka Matope Historia
1- Uzushi na maneno ya uongo.
Wanatunga kisa fulani, mfano wa kisa walichokitunga juu ya Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba eti alisujudu kwa ajili ya kumshukuru Allaah aliposikia habari za kifo cha ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu). Bila shaka hiki ni kisa cha uongo.

 2- Kuongeza maneno au kupunguza kwa nia ya kuleta sura mbaya.
 Huenda kisa cheyewe kikawa ni sahihi, kwa mfano kisa cha tukio la Saqiyfat bani Sa’ad. Kisa hiki kilitokea kweli mara baada ya kufariki kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) walipokutana Abu Bakr na ‘Umar na Abu ‘Ubaydah upande mmoja, na upande wa pili alikuwa Al Khabab bin Mundhir na Sa’ad bin ‘Ubaadah na wengineo katika watu wa Madiynah (Radhiya Allaahu ‘anhum). Waandishi hao wakaongeza maneno yao kama nitakayokuja kuelezea kila tukiendelea mbele. Wameongeza kwa nia ya kuharibu sifa za Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

3- Kufasiri visivyo sahihi hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Nako ni kuyafasiri maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kama wanavyotaka wao ili yakubaliane na matamanio yao na itikadi zao.

4 -Kudhihirisha lugha mbaya au makosa.
Kisa kinakuwa cha kweli, lakini wao wanakielezea huku wakitilia mkazo pale
Sahaba (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipofanya makosa kwa nia ya kuyabainisha makosa hayo huku wakiyaficha mema yao bila kuyabainisha.

5- Kutunga mashairi kwa ajili ya kuyapa nguvu matukio ya kihistoria.
Wanatunga mashairi kisha wanayanasibisha na ‘Aamiri wa Waislamu ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) au wanayanasibisha na Mama wa Waislamu Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), au wanayanasibisha na Az-Zubayr bin Awaam au Talha (RAnhuma) kwa ajili ya kumtuhumu mmojawapo katika ya Maswahaba, kama walivyotunga shairi la kumkashifu Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kisha wakalinasibisha na Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu).

4- Kutunga barua za uongo
Kama tutakavyoona InshaaAllaah katika kisa cha kuuliwa kwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu), jinsi barua za uongo zilivyoandikwa, kisha akasingiziwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa yeye ndiye aliyeziandika, na namna gani zilivyoandikwa barua za uongo na kunasibishwa na Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) na nyingine zikaandikwa na kusingiziwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa ndiye aliyeziandika na Talha na Az-Zubayr (Radhiya Allaahu ‘anhu), haya ukiacha kuhesabu barua na vitabu kama kitabu kiitwacho Nahjul Balagha kilichoandikwa na kunasibishwa na ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) pamoja na kitabu kiitwacho Al Imamah walichokinasibisha na Imam Ibni Qutaybah.


Juhudi Za Mashia Katika Kuingiza Uongo Na Kuipa Sura Mbaya Historia Ya Kiislamu
Walio mashuhuri kupita wote katika historia kwa uzushi na kwa uongo ni Mashia, na hii ndiyo maana maulamaa wanawapigia mifano kwa kusema;
“Muongo kuliko Rafidhiy (Shia)”, na hii inatokana na wingi wa kusema uongo kwao”.
Anasema Al A-amash;
“Niliwahi kuishi na watu waliokuwa wakijulikana kwa jina la ‘waongo’.
Anasema Shurayh Al-Qaadhiy;
“Naipokea elimu kutoka kwa yeyote nitakayeonana naye isipokuwa Mashia, kwa sababu wao wanatunga hadithi za uongo kisha wanaigeuza hadithi hiyo kuwa dini yao”.
Anasema Imam Shafi;
“Sijapata kuona wenye kusema uongo kuliko Mashia”.
Kusudi langu ni kuwa ingawaje makundi mengine pia yanasema uongo lakini hawa ni mashuhuri sana kuliko wengine katika kueneza habari zisizo za kweli na kutunga hadithi za uongo.


Taratibu Za Kuhakikisha Ukweli Wa Hadithi Kwa Ahlus Sunnah – Wakati Gani Zilianza?
Zilianza baada ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe (fitan).
Muhammad bin Siriyn (Rahimahu Allaah) ambaye ni miongoni mwa maulamaa wakubwa wa Taabi iyn amesema;
“Watu hawakuwa wakiuliza juu ya isnadi za hadithi walizokuwa wakizisikia, mpaka pale ilipotokea ‘fitna’ (vita vya wenyewe kwa wenyewe), wakaanza kusema; ‘Tutajieni majina ya wale mlopokea hadithi hizi kutoka kwao’, Ikawa watu wanaangalia majina ya wapokezi wa hadithi zinazosimuliwa na watu wa Ahlus Sunnah na kuzikubali riwaya zao, na wanapoangalia majina ya wapokezi wa Ahul Bida-a, wanazikataa riwaya zao”.
(Haya yamo katika utangulizi wa kitabu cha Sahih Muslim).
Na hii ni kwa sababu watu wanapokea riwaya kutoka kwa wanoaminika, na Ibni Siyrin ni mmojawapo wa wakubwa wa maulamaa wa At-Tabiiyn aliyewahi kuishi na baadhi ya Maswahaba na akaishi pamoja na maulamaa wakubwa wa Taabiiyn na wadogo wao, na kwa sababu fitna zilizotokea ndiyo maana kukatokea makundi ya Shia na Khawarij na Qadiriyah.


Kuja Kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)

Siku ya Jumatatu tarehe 12 mwezi wa Rabiul awwal (ipo khitilafu juu ya siku aliyozaliwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)), Allaah aliwatunukia walimwengu wote zawadi kubwa sana kwa kuzaliwa kwa bwana wa viumbe vyote na kiongozi wao Muhammad bin ‘Abdullaah bin ‘Abdul Muttwalib Al-Haashimy kutoka katika kabila la ki Quraysh.
Alizaliwa akiwa yatima hana baba na alipotimia miaka sita mama yake akafariki na akachukuliwa na babu yake ‘Abdul Muttwalib, na miaka miwili baadaye babu yake akafariki na akachukuliwa na ammi yake Abu Twaalib.
Alipotimia miaka arubaini Allaah alimpa utume ili awe mwenye kuleta bishara njema na mwenye kuonya, akausimamia ujumbe wake kama unavyostahiki kusimamiwa na akafikishi yale Allaah alomuamrisha ayafikishe kwa ajili ya kuwatowa watu katika giza na kuwaingiza katika nuru. Wakubwa wa kabila lake wakamfanyia uadui na wakawatendea wafuasi wake kila aina ya udhia, wakamfuata makundi ya watu walioiuza dunia yao kwa ajili ya akhera, wakapigana jihadi katika njia ya Allaah kwa mali zao na kwa nafsi zao, wakainusuru (dini ya) Allaah na Mtume wake.
Allaah Anasema;
“(Basi) wapewe (mali hayo) mafakiri wa Kimuhajiri ambao walifukuzwa katika nyumba zao na mali zao; (wakakhiari kuwacha hayo) kwa jili ya (kutafuta) fadhila za Allaah na radhi (yake) na kuinusuru (dini ya) Allaah na Mtume wake. Basi hao ndio Waislamu wa kweli”.
Al Hashr - 8

Akaendelea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwalingania watu muda wa miaka kumi na tatu mpaka Allaah alipomuamrisha kuhamia Madiynah, mji ambao Allaah ameutia nuru kwa kumjaalia Mtume wake kuhamia huko. Wakahamia huko pia Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na kuacha mali zao na watoto wao nyuma yao, yote hayo kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah.

Alipowasili Madiynah akapokewa vizuri na watu wa mji huo, waliomnusuru na kumsaidia. Wakawasaidia wale waliohama pamoja naye, wakagawana nao mali zao na nyumba zao na hata wake zao, kwani watu wa Madiynah wenye wake wawili au zaidi walikuwa wakiwaambia watu wa Makkah;
“Chagua mmoja kati ya wake zangu yule unayemtaka ili nimtaliki kisha nikuozeshe wewe”.
Allaah Anasema;
“Na wale waliofanya maskani yao hapa (yaani Madiynah) na wakautakasa Uislamu (wao barabara) kabla ya kuja hao (Muhajir huko Madiynah) na wakawapenda hao waliohamia kwao, wala hawapati (hawaoni) dhiki nyoyoni mwao kwa hayo waliyopewa (hao Muhajiri), na wanawapendelea kuliko nafsi zao ingawa wenyewe wana hali ndogo. Na waepushwao na ubakhili wa nafsi zao hao ndio wenye kufaulu kweli kweli”.
Al Hashr –9

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaendelea na da’awah yake nje ya mji wa Madiynah na hatimaye bara ya Arabu yote mpaka ilipofika siku ile tukufu ambayo Allaah Alimfungulia Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mji mtukufu wa Makkah (alipouteka mji wa Makkah) na watu wake wakaingia katika dini ya Kiislamu na baada ya hapo bara ya Arabu yote ikawa chini ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Baada ya kuwalingania watu pamoja na kupigana jihadi muda upatao miaka ishirini na mitatu, ikamfikia qudra ya lazima kwa kila mtu inayosadikishwa na kauli ya Allaah isemayo;
“Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume tu. Wamepita kabla yake Mitume (wengi kabisa),. Basi akifa au akiuawa ndiyo mtarudi nyuma (kwa visigino vyenu muwe makafiri kama zamani?) Na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru Allaah chochote . Na Allaah atawalipa wanaomshukuru”.
Aali ‘Imraan – 144

Dunia ilikuwa kama kwamba imeingia giza totoro kutokana na tukio hili. Na kwa nini isiwe hivyo wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema;
“Atakayekutwa kati yenu na msiba, basi akumbuke msiba wake kwangu (wa kifo changu), kwani huo ndio msiba mkubwa zaidi”.
Atw-Twabaqaat al-Kubraa na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy.
Haukupata kutokea msiba mkubwa wakati wowote ule tokea iumbwe dunia kuliko msiba wa kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Na huyu Bibi Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) binti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wakati baba yake alipokuwa akijiwa na sakrati l mauti alikuwa akisema;
“Baba yangu! ameitikia mwito wa Mola wake, baba yangu! Pepo ya Firdausi makazi yake, baba yangu! kwa Jibril tunafikisha pole yake”.
Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye alisema;
“Siku ile Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipoingia mji wa Madiynah, kila kitu kilikuwa kikitowa mwangaza, ama siku ile aliyofariki kila kitu kiliingia giza, na tulipokuwa tukipangusa mikono yetu michanga baada ya kumzika tulihisi nyoyo zetu zimenyongeka (kwa sababu wahyi umeshakatika na hautoshuka tena baada yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)”.

Ibni Majah katika ‘Kitaabul Janaaiz – mlango wa ‘Wafaatun Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Baada ya kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), Abu Bakr alimwambia ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhum);
“Twende tukamtembelee Ummu Ayman”.
Walipowasili kwake, Ummu Ayman alilia sana, wakamuuliza;
“Kwa nini unalia hivyo wakati atakayopata Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa Mola wake ni bora zaidi?”
Akajibu;
“WaAllaahi ninalia si kwa sababu sielewi kuwa yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi kwa Mtume wake, isipokuwa kinachoniliza ni kukatika kwa wahyi kutoka mbinguni”.
Maneno hayo yaliwaliza sana Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma)
Muslim

Na hivi ndivyo nafsi hii njema ilivyohamia kwa Mola wake.


Ukhalifa Wa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘Anhu)
Mara baada ya kutangazwa kufariki kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), Abu Bakr alikwenda moja kwa moja mpaka mahali alipolazwa, akaufunua uso wake na kumbusu juu ya kipaji cha uso wake baina ya macho yake, kisha akasema;
“(Nakufidia) Kwa baba yangu na mama yangu, unapendeza ukiwa hai au umekufa”.
Kisha akaufunika uso wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), akanyanyuka na kupanda juu ya membari na kusema;
“Kama yupo aliyekuwa akimuabudu Muhammad, basi Muhammad kesha kufa, ama kama mlikuwa mkimuabudu Allaah, basi Allaah yuhai na hafi. (kisha akaisoma kauli ya Allaah ifuatayo;)
“Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume tu. Wamepita kabla yake Mitume (wengi kabisa). Akifa au akiuawa ndiyo mtarudi nyuma (kwa visigino vyenu), muwe makafiri kama zamani? Na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru Allaah cho chote. Na Allaah atawalipa wanaomshukuru”.
Aali ‘Imraan – 144
Watu wakawa wanalia na wengine wakawa wanatembea mitaani huku wakiikariri aya hiyo. Anasema Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu);
“Ilikuwa kama kwamba hatujapata kuisikia aya hiyo isipokuwa wakati ule (kama kwamba tunaisikia kwa mara ya mwanzo)”.
 Al-Bukhaariy – kitabu cha Fadhila za Maswahaba.
Juu ya kuwa Qur-aan ilikwisha kamilika kabla ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kabla ya kufariki kwake, lakini aya hii ilikuwa kama ni mpya kwao, kama kwamba hawakupata kuisikia kabla ya siku hiyo kutokana na mshituko waloupata kwa kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Al-’Abbaas bin Abdul Muttalib na ‘Aliy bin Abi Twaalib na Az-Zubayr bin Al-‘Awaam (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndio waliofanya kazi ya kumuosha na kumkafini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kumshughulikia mpaka aliposaliwa, na hii ni kwa sababu Al-’Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni ‘Ami yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni mtoto wa ammi yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Az-Zubayr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni mtoto wa shangazi lake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kwa ajili hiyo wao ndio waliostahiki zaidi kujishughulisha na hayo.

Saqiyfat Bani Saa’idah
Wakati Al-’Abbaas na Ali na Az-Zubayr (Radhiya Allaahu ‘anhu) walipokuwa wakijishughulisha na kumtayarisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), baadhi ya watu wa Madiynah walikutana mahali panapoitwa Saqiyfat Bani Saa’idah, na nitakielezea kisa hiki kwanza kama kilivyoelezwa katika kitabu cha Taariykh cha Imam Atw-Twabariy namna kilivyoelezwa na Abi Makhnaf ‘muongo’, kisha nitakielezea kama kilivyoelezwa na Imam  Al-Bukhaariy, kisha pima wewe mwenyewe baina ya riwaya mbili hizi ili uweze kuujuwa uongo ulio ongezwa na Abu Makhnaf.
Huenda mengi katika uongo huo uliozidishwa ukawa katika wakati wetu huu ni jambo lililokwisha kubalika miongoni mwa watu, na haya tutakuja kuyaona pale tutakapozungumza juu ya tukio la Shuura.
Anasema Imam Atw-Twabariy (Allaah Amrehemu):
Ametuhadithia Hisham bin Muhammad kutoka kwa Abi Makhnaf, (kuwa) amesema: Nimehadithiwa na ‘Abdullaahi bin ‘Abdur-Rahmaan bin Abi Amru bin Abi Amrah Al Ansari kuwa Mtume alipofariki, watu wa Madiynah walikusanyika (mahali panapoitwa) Saqiyfat bani Saa’idah wakasema;
“Baada ya Muhammad tumchaguwe Sa’ad bin Ubada awe kiongozi wetu”.
Mmoja wao akainuka na kusema;
“Kwa panga zenu waarabu wote wamekufuateni, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amefariki akiwa ameridhika nanyi na akiwa amefurahika nanyi (kwa hivyo) musiiache fursa hii wakaja kuichukuwa watu wengine”.
Wote wakajibu;
“Rai yako ni sawa”.
Mmojawao akasema;
“Wakikataa wahajiri wa KiQuraysh tutawaambia ‘Aamiri mmoja atoke kwao na ‘Aamiri mmoja atoke kwetu”.
Akasema Sa’ad bin ‘Ubaadah;
“Huu ni udhaifu wa mwanzo”.
Kisha zikamfikia habari ‘Umar bin Al-Khattwwaab kuwa baadhi ya watu wa Madiynah wamekusanyika Saqiyfat bani Saa’idah wakisema: ‘Amri mmoja kutoka kwetu na ‘Aamiri mmoja kutoka kwenu’. Alipewa habari hizo na mmojawapo katika watu wa Madiynah. Akenda moja kwa moja mpaka kwa Abu Bakr na kumueleza juu ya jambo hilo, akamwambia:
“Ndugu zetu katika watu wa Madiynah ‘Al Ansar’, wamekusanyika na wanasema hivi na vile, tuwaendee huko haraka sana”.
‘Umar na Abu Bakr walipokuwa wakiondoka wakakutana na Abu ‘‘Ubaydahh wakamwambia:
“Twende pamoja”.
Wakaondoka watatu hao na kuelekea mahali walipojikusanya watu wa Madiynah. Anasema ‘Umar;
“Nilikuwa nimekweshajitayarishia maneno ya kusema, na nilipokuwa nikijitayarisha kusema, Abu Bakr akaniashiria kuwa ninyamaze na akaanza Abu Bakr kusema;
“AlhamduliAllaah”, kisha akampwekesha Allaah, kisha akasema;
“Hakika Allaah amemleta Muhammad…..”
Kisha akaitaja khutba ndefu iliyotolewa na Abu Bakr na kwamba alisema ndani ya khutba hiyo kuwa watu wa Makkah ‘Muhajirin’ ndio wanaostahiki kuwa Makhalifa.
Akasema Al Habaab bin Mundhir;
“Enyi watu wa Madiynah! Mumiliki wenyewe amri yenu, kwani watu wako chini ya kivuli chenu na hawezi yeyote kujaribu kwenda kinyume nanyi na watu hawatofuata isipokuwa rai yenu, nyinyi ndio wenye nguvu na wenye mali na wenye idadi kubwa ya watu na wenye ulinzi, na kama wakikataa kukufuateni basi watoweni nje ya mji (wenu) huu. Waongozeni nyinyi katika mambo haya, kwani nyinyi waAllaahi ndiwo wenye haki kuliko wao, kwa sababu kwa panga zenu wameingina katika dini hii walioingia wale wasiokuwa na dini. Mimi ndiye mwenye kuistahikia zaidi na mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kulibeba jukumu hili kuliko wengine”
‘Umar na Abu ‘‘Ubaydahh wakamwambia Abu Bakr;
“Tandaza mkono wako tufungamane nawe”, walipokuwa wanataka kufungamana naye, akawatangulia Bashir bin Sa’ad (mtu wa Madiynah) na akawa yeye mtu wa mwanzo kufungamana naye, na hivi ndivyo watu walivyofungamana na Abu Bakr.
Anasema (Abu Makhnaf);
“Akainuka Usayd bin Hudhair aliyekuwa miongoni mwa viongozi wa kabila la Aus waliokuja kufungamana na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)  katika ‘Fungamanao la Aqaba la pili’ kabla ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuhamia Madiynah, akasema;
“WaAllaahi ikiwa uongozi juu yenu watauchukuwa watu wa kabila la Khazraj mara moja tu, basi haitoondoka tena fadhila yao hiyo juu yenu”.
(Abu Makhnaf anamaanisha hapa kuwa Usayd alimuonea husda Sa’ad bin ‘Ubaadah anayetokana na kabila la Khazraj kwa kuteuliwa na watu wa Madiynah kuwa kiongozi wa Waislamu”.
(Aus na Khazraj ni makabila mawili makubwa ya watu wa Madiynah)
Sa’ad akasema;
“WaAllaahi kama ningelikuwa na nguvu za kujinyanyua, basi ungelisikia kutoka kwangu mngurumo utakaokujeruhi wewe na sahibu zako, kisha waAllaahi ningelikufukuzia kwa kaumu ambayo wewe ulikuwa ukiwafuata tu na wala hawakufuati, niondoweni mahali hapa”.
Wakamnyanyua na kumuingiza nyumbani kwake, akaachwa kwa muda wa siku nyingi kisha akasema;
“Ama waAllaahi mpaka nikuvurumishieni mishale niliyoibeba ndani ya mfuko wake, na niipake rangi (damu) meno yake (mishale hiyo), kisha nikupigeni kwa upanga wangu kisha nikupigeni vita mimi na watu wa nyumba yangu pamoja na watakaonitii katika watu wa kabila langu”.
Anasema (Abu Makhnaf):
“Sa’ad akawa hasali sala yao wala hasali Ijumaa pamoja nao, anahiji lakini hafuatani nao, akaendelea katika hali hiyo mpaka alipofariki Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)”.

Hii ni riwaya kama ilivyoelezewa na Abu Makhnaf juu ya tukio la Saqiyfat Bani Saa’idah, na sasa someni riwaya iliyosimuliwa na Imam Al-Bukhaariy juu ya kisa hiki, kisha linganisheni.
Anasema Imam Al-Bukhaariy;
“Nimehadithiwa na Ismail bin ‘Abdullaah, nimehadithiwa na Suleiman bin Bilal kutoka kwa Hisham bin Uruwah amesema: Amenambia Uruwah bin Az-Zubayr kuwa ‘Aaishah mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema;
“Hakika alipofariki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) watu wa Madiynah walijumuika kwa Sa’ad bin Ubada mahali panapoitwa Saqiyfat bani Saa’idah, wakasema;
“‘Aamiri mmoja atoke kwetu na ‘Aamiri mmoja atoke kwenu”.
Abu Bakr na ‘Umar na Abu ‘‘Ubaydahh wakawaendea, na ‘Umar alipotaka kuhutubia akanyamazishwa na Abu Bakr, na ‘Umar alikuwa akisema;
“WaAllaahi kwa kufanya vile sikuwa na nia nyingine isipokuwa nilitaka kusema maneno yaliyonipendeza niliyokwishayatarisha na nikaogopa Abu Bakr asije akashindwa kuifikisha fikra hiyo, lakini Abu Bakr akaweza kuifikisha vizuri kupita mtu yeyote, na akasema katika maneno yake;
“Ma ‘Aamiri watoke kwetu na Ma Waziri watoke kwenu”.
Akasema Khubab bin Mundhir:
“WaAllaahi hatukubali. Kwetu atoke ‘Aamiri na kwenu atoke ‘Aamiri”.
Abu Bakr akasema;
“Sivyo hivyo, sisi ni Ma Amri na nyinyi ni Ma Waziri, wao (MaQuraysh) ndio waarabu wa kati kwa kati kupita wote na watukufu kupita wote, Fungamaneni na ‘Umar au Abu ‘Ubaydahh”.
‘Umar akasema;
“Bali tutafungamana na wewe, kwani wewe ndiye bwana wetu na mbora wetu na unayependwa zaidi na Mtume wa Allaah kuliko sisi. Kisha ‘Umar akauchukuwa mkono wake na akafungamana naye, na watu wote wakafungamana naye”.
Sahihul Al-Bukhaariy katika mlango wa Fadhail al Sahaba

Hii ni riwaya ya Imam  Al-Bukhaariy, kama unavyoiona kuwa ni fupi na ndogo na huu ndio uhakika wa mambo yalivyokuwa katika Saqiyfat bani Saa’idah. Ama yale aliyozidisha Abu Makhnaf kama mlivyosikia kwamba eti Sa’ad bin ‘Ubaadah alisema;
“Nitapigana vita na nyinyi…” na kwamba eti hakuwa akihiji wala kuswali pamoja nao wala hakuwa akisali Ijumaa pamoja nao wala hakuwa akifuatana nao, na kwamba Al Khabaab bin Mundhir alimjibu Abu Bakr, pamoja na nyongeza nyingine (yoote hayo ni uongo mtupu), kwani tukio la Saqifa halikuchukuwa zaidia ya nusu saa, na tazameni namna gani walivyokifanya kisa hicho kuwa kikubwa kuliko kinavyostahiki.
Ama kuhusu Sa’ad bin ‘Ubaadah, imepokelewa hadithi katika Musnad ya Imam Ahmad kutoka kwa Humaid bin Abdur Rahman kuwa amesema;
“Alizungumza Abu Bakr na wala hajaacha sifa zozote katika zile walizoteremshiwa watu wa Madiynah ndani ya Qur-aan au zile alozitaja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) asizitaje (Amezitaja sifa zote za watu wa Madiynah). Akasema;
“Mnakumbuka kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema; “Na lau kama watu wote watafuata njia zao katika mabonde na mitaa, na watu wa Madiynah watafuata njia nyingine, basi mimi ningefuata njia watakayopita watu Madiynah”.
Kisha baada ya hayo Abu Bakr akamwambia Sa’ad bin ‘Ubaadah;
“Na wewe unakumbuka ewe Sa’ad kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) (siku moja) ulipokuwa umekaa alikwambia: “MaQuraysh ndio watakao ongoza amri hii, na watu wema wanawafuata wema wao na waovu wanawafuata waovu wao”.
Baada ya kusikia maneno hayo Sa’ad akasema;
“Umesema kweli! Sisi ni Ma Waziri na nyinyi Ma ‘Aamiri”.
Riwaya hii imesimuliwa na Ahmad katika Musnad yake kwa isnadi sahihi iliyonyanyuliwa (mursal) na Humaid bin ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhiya Allaahu ‘anhu), na ingawaje riwaya hii imenyanyuliwa, lakini ina nguvu zaidi kuliko riwaya za muongo yule – Abu Makhnaf.


Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Jina lake ni ‘Abdullaah bin ‘Uthmaan bin ‘Aamir bin Amru bin Ka’ab bin Sa’ad bin Tiym bin Murrah bin Kaab bin Luayyi bin Ghalib bin Fihr, na Fihri huyu ndiye Quraysh.
Amesema ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu);
“Allaah ameteremsha jina la Abu Bakr (la) Asw-Swiddiyq kutoka mbinguni”.
Atw-Twabaraaniy hadithi nambari 1/55 na ameitaja hadithi hii pia Al-Haafidh Ibn Hajar katika Al-Fatah 7/11.


Kusilimu Kwake
Kutoka kwa Abu Dardaa (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema;
“Nilikuwa nimekaa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akatokea Abu Bakr akiwa ameshika (na kuinyanyua) ncha ya nguo yake hata goti lake likawa linaonekana, akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam);
“Ama sahibu yenu (anaonesha) kesha kasirishwa”.
Abu Bakr akatoa salamu kisha akasema;
“Ilikuwa baina yangu na ‘Umar jambo, nilimfanyia haraka, kisha nikajuta, nikamuomba anisamehe akakataa, nikakujia wewe”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;
“Allaah akughufirie ewe Abu Bakr (akasema hivyo mara tatu)”.
Kisha ‘Umar naye akajuta, akenda mpaka nyumbani kwa Abu Bakr na kuuliza;
“Abu Bakr yupo?”
Wakasema;
“Hayupo”.
Akenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na uso wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ukawa umebadilika rangi kwa ghadhabu, mpaka Abu Bakr akamuonea huruma ‘Umar, akapiga magoti mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kusema;
“Ewe Mtume wa Allaah, waAllaahi mimi ndiye niliyemkosea (mara mbili)”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;
“Allaah alinituma kwenu (na nyote) mkanambia muongo, (isipokuwa) Abu Bakr alisema; ‘nakusadiki’, akaniliwaza kwa kwa hali na mali, sasa nyinyi mtamuacha sahibu yangu (akasema hiyvo mara mbili)”.
Tokea siku hiyo Abu Bakr hakukasirishwa tena na mtu.
 Al-Bukhaariy mlango wa Fadhila za Maswahaba
Na kutoka kwa ‘Amaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema;
“Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa hakufuatana na zaidi ya watu watano na wanawake wawili na Abu Bakr”.
Al-Bukhaariy


Kuhajiri Kwake
Kutoka kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema;
“Nilikuwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pangoni, nikanyanyua kichwa changu, nikajikuta nipo karibu na miguu ya watu (makafiri). Nikasema; “Ewe Mtume wa Allaah mmoja wao akitupa jicho lake chini atatuona”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;
“Nyamaza ewe Abu Bakr, (sisi) wawili na AAllaah wa tatu wao”.
Al-Bukhaariy kitabu cha sifa za watu wa Madiynah, mlango wa Hijra ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Sahaba zake. Hadithi nambari 3922.
Muslim kitabu cha wa sifa za Maswahaba hadithi nambari 1.


Fadhila Zake
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema;
“Nilimsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema;
Atakayetoa viwili vya aina moja katika njia ya Allaah (mfano ngamia wawili au mbuzi wawili au dirham mbili n.k.), ataitwa kwenye milango ya Peponi huku akiambiwa; “Ewe mja wa Allaah, hii ni kheri (yaani njoo uingie Peponi kupitia mlango huu). Aliyekuwa katika watu wenye kuswali (kwa wingi) ataitwa kupitia mlango wa Sala, na aliyekuwa katika watu wa Jihadi ataitwa kupitia mlango wa Jihadi, na aliyekuwa mtoaji wa Sadaka (mwingi wa kutoa Sadaka) ataitwa kupitia mlango wa Sadaka na aliyekuwa katika watu wa Swawm (mwingi wa kufunga) ataitwa kupitia mlango wa Swawm au mlango wa Ar-Rayaan”.
Abu Bakr akasema;
“(Nimefahamu kuwa) Si lazima mtu aitiwe kupitia milango yote hiyo (muhimu aingie Peponi tu).
Kisha Abu Bakr akauliza;
“Yupo atakayeitwa kupitia milango yote hiyo ewe Mtume wa Allaah?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;
“Naam – yupo na nataraji utakuwa miongoni mwao ewe Abu Bakr”.
 Al-Bukhaariy kitabu cha ‘Fadhila za Maswahaba’, hadithi nambari 3666

Kutoka kwa Anas bin Malik (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema;
“Aliupanda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Abu Bakr na ‘Uthmaan (mlima Uhud), ukatikisika mlima, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;
“Tulia (ewe) Uhud, kwa sababu juu yako yupo Mtume na Asw-Swiddiyq na mashahidi wawili (watakaokufa shahid)”.
 Al-Bukhaariy kitabu cha ‘Fadhila za Maswahaba’ hadithi nambari 3675

Kutoka kwa ‘Amru bin Al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema;
“Nilimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): mtu gani unayempenda zaidi kupita wote?”
Akanambia;
“‘Aaishah”.
Nikamuuliza tena:
“Yupi katika mwanamume (unayempenda zaidi)?”
Akanambia:
“Baba yake”.
Nikamuuliza:
“Kisha nani?”
Akanambia:
“‘Umar bin Al-Khattwwaab”.
 Al-Bukhaariy katika kitabu cha Fadhila za Maswahaba hadithi nambari 3662
Muslim mlango wa Fadhila za Maswahaba hadithi nambari 8
Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema;
"Katika watu walonisaidia sana kwa hali na mali ni Abu Bakr, ingelikuwa naweza kumchagua Khalil (rafiki), basi angekuwa Abu Bakr, lakini ni ndugu katika Uislamu na kupendana. Milango yote iliyoelekea msikitini ifungwe isipokuwa mlango wa Abu Bakr".
Al-Bukhaariy kitabu cha Fadhila za Maswahaba hadithi nambari 3654
Kuwa Kwake Pamoja Na Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Sallam)

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoulizwa juu ya jambo gani ovu kupita yote alowahi kutendewa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na washirikina, akasema;
“Nilimuona ‘Uqbah bin Abi Mu’it akimuendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wakati akiwa anasali, akamzungushia nguo yake shingoni pake na kumkaba nayo rohoni pake kwa nguvu sana, akatokea Abu Bakr na kumsukumilia mbali na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kisha akasema;
Oh! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allaah? Na kwa yakini yeye amekujieni kwa dalili waziwazi zitokazo kwa Mola wenu”
 Al-Bukhaariy kitabu cha Fadhila za Maswahaba hadithi nambari 3678


Dalili Za Kupewa Ukhalifa Kutoka Kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)
Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema;
“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa akiumwa alinambia;
“Muamrishe Abu Bakr asalishe watu”.
 Al-Bukhaariy katika kitabu cha ‘Adhani’ mlango wa ‘Ahlul ilm wal fadhal ahaqu bil Imamah’, hadithi nambari 678

Kutoka kwa Jaafar bin Mut’im amesema:
“Alikuja mwanamke mmoja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamuarisha arudi siku nyingine, akauliza:
“Nisipokukuta (nifanyeje)?” (kama kwamba anamuuliza ‘ukifa nimuendee nani?”
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
“Usiponikuta mwendee Abu Bakr”.
 Al-Bukhaariy kitabu cha Fadhila za Maswahaba hadithi nambari 3659
Muslim kitabu cha Fadhila za Maswahaba hadithi nambari 10

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema:
“Alinambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa akiumwa: “Niitie Abu Bakr na ndugu yako ili nimwandikie maneno kwani mimi naogopa asije akatamani mwenye kutamani kisha akasema: “Mimi ndiye ninayestahiki zaidi na Allaah hamkubali mwengine na Waislamu hawamkubali mwengine isipokuwa Abu Bakr”.
Muslim kitabu cha Fadhila za Maswahaba hadithi nambari 11
Al-Bukhaariy kitabu cha ‘Kuumwa’ mlango wa ‘Anachoruhusiwa mgonjwa kusema anapoumwa hadithi nambari 5666


Mambo Muhimu Yaliyotokea Wakati Wa Ukhalifa Wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

1- Jeshi La ‘Usaamah
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa keshatayarisha jeshi chini ya ongozi wa ‘Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) litakalokwenda kupigana vita nchi ya Sham, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifariki dunia kabla ya jeshi hilo kuondoka Madiynah, na jambo la mwanzo alofanya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni kulipeleka jeshi hilo la ‘Usaamah.
Na katika kulipeleka jeshi hilo la ‘Usaamah, ilikuwa pigo kubwa kwa wanafiki waliortadi waliodhania kuwa baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) Uislamu utadhoofika na kutoweka, na katika kulipeleka jeshi hilo pia kulinyanyua nguvu za irada ya Waislamu.


2- Vita Vya Walortadi
Walortadi ni wale waliotoka katika Uislamu baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na wengi wao ni wafuasi wa Musailima l Kadhab (Mtume wa uongo) na Taliha al Aswad na Sajaaj, na vilipiganwa vita vikali sana na vilivokuwa vikali zaidi ni vita vilivyojulikana kwa jina la ‘Mapambano ya bustanini’ (Maarakatul hadiqah) dhidi ya Musailimah l Kadhab katika mji wa Yamama na Waislamu wakashinda
ushindi mkubwa kabisa.


3- Vita Dhidi Ya Walokataa Kutoa Zakaah
Waliokataa kutoa Zakaah ni wale walikuwa wakidhania kuwa zile pesa za Zakaah walizokuwa wakimpa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa ni kodi na kwamba baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hapana haja tena ya kuilipa kodi hiyo.
Imetolewa na Al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:
“Alipofariki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Abu Bakr akawa khalifa walikufuru waliokufuru katika waarabu na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema (kumwambia Abu Bakr): Vipi tutapigana vita na watu wanaoitamka shahada ya laa ilaaha illa Allaah wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema: ‘Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watamke Laa ilaaha illa Allaah, na atakayeitamka itahifadhika kwangu mali yake na nafsi yake na hesabu yake iko kwa Allaah?
Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;
"WaAllaahi nitapambana na kila anayefarikisha baina ya Sala na Zakaah kwa sababu Zakaah ni katika haki ya mali. WaAllaahi kama watakataa kunipa mbuzi mdogo waliyekuwa wakimpa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ningepigana nao kwa kukataa kwao huko”.
Sahih Al-Bukhaariy kitabu cha Zakaah mlango wa ‘Kuwajibika kwa Zakaah’ hadithi nambari 1399


Kutekwa Kwa Miji Ya Uajemi (Iran)
Abu Bakr alipeleka majeshi yake katika nchi ya Uajemi (Iran) yakiongozwa na Al Muthanna bin Al Haritha, kisha akampeleka Khaalid bin Waliyd na akamfuatilia na Al Qaa qaa bin ‘Amru At-Tamimiy.


Kutekwa Kwa Miji Ya Sham
Abu Bakr alimchaguwa Khaalid bin Said bin Al-’Aasw kuwa mkuu wa majeshi yake aliyoyapeleka katika nchi ya Sham, akapambana na majeshi ya Warumi na alipotaka mSa’ada kutoka kwa Abu Bakr, akampeleka Al Waliyd bin Utbah na Ikrimah bin Abu Jahal na Amru bin Al-’Aasw na Abu ‘Ubaydah ‘Aamir bin Al-Jaraah na yeye ndiye aliyechukuwa uongozi wa majeshi baadaye.
Yakasonga mbele majeshi ya Waislamu mpaka yakaweza kuuteka mji wa Yarmuk, kisha Abu Bakr akampeleka huko Khaalid bin Waliyd na Allaah akawapa ushindi.

Itaendelea InshaAllaah

0 Comments