Wengi hawajali uhalali wa bidhaa wanazotumia

Watanzania wameshauriwa kula vyakula vyenye ubora na vilivyoidhinishwa na bodi za Halal zilizopo ili kuimarisha afya zao na kujikinga na maradhi yasiyoambukiza yakiwamo ya saratani.

Ushauri huo umetolewa na Amir wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Mussa Kundecha wakati akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu.

Katika maelezo yake, Sheikh Kundecha alisema uuzaji wa bidhaa unahitajika kwa sababu ni moja ya shughuli zinazochangia kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla, lakini akaonya kuwa, si kila bidhaa inaweza kuwa bora na sahihi kwa afya za walaji.

Sheikh Kundecha alisema wengi wa wafanyabiashara wamekuwa wakipuuza sheria za uzalishaji zinazowataka wazalishe bidhaa halali na zenye viwango vya ubora vilivyoidhinishwa na mamlaka za kudhibiti ubora wa vyakula.

Kwa mujibu wa Sheikh Kundecha, upo uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya vyakula na maradhi yasiyoambukiza yakiwamo ya moyo na kiharusi.

Hata hivyo, Sheikh Kundecha alikiri kuwepo kwa tatizo la bidhaa zisizo halali na ambazo hazina ubora kutokana na mwamko mdogo wa wananchi katika kuhoji ubora wa bidhaa wanazozitumia.


“Walaji ndio wanaotakiwa kuhoji uhalali wa bidhaa wanazotumia, lakini wengi wanashindwa kuhoji uhalali wa kile wanachonunua… kama watu wanaingia tu uwanja wa fisi na kula nyama pasipo kujua kama nyama hiyo ni ya paka au ya mbwa, muuzaji hawezi kuzingatia ubora na uhalali wa nyama anayouza,” Sheikh Kundecha alibainisha.


“Qur’an inatueleza kuwa tuchinje na tule vyakula halali lakini kwa sababu mbalimbali tumekuwa tukila chakula bila kujua kimeanzia wapi na kimepita katika njia gani,” alisema.

Amir Kundecha aliongeza kuwa wateja wengi hasa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu hukimbilia bidhaa za vyakula zinazoingia sokoni kwa mara ya kwanza na hivyo kukosa nafasi ya kuchunguza kama ni halali au la. “Tumejionea kwenye mitandao ya kijamii na ninyi mmepata kusikia fununu juu ya kuwepo kwa mayai bandia,” alisema Sheikh Kundecha.

Kuhusu changamoto ya ubora wa bidhaa halali, alisema Tanzania ina viwanda vichache vya uzalishaji bidhaa za vyakula na ndio maana mwamko wa watu ni mdogo katika kufuatilia uhalali na ubora wa bidhaa
ukilinganisha na nchi nyingine kama vile Afrika ya Kusini na Zimbabwe ambazo ukaguzi wa bidhaa za viwandani ni mkubwa.


“Imeshakuwa mazoea na walaji hawajali afya zao kwa kununua vyakula visivyo halali na vyenye ubora,” alisema Sheikh Kundecha.

Kutokana na hali hiyo, Sheikh Kundecha alitoa wito kwa Masheikh, taasisi za dini na vyombo vya habari kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia bidhaa zilizowekwa nembo ya Halal.

Sheikh Kundecha alisema: “Nembo ya Halal si alama inayofichwa ili umma isiifahamu. Inatangazwa kwenye vyombo vya habari na mara kwa mara tumekuwa na semina za kuhamasisha watu kutumia bidhaa halali.”

chanzo : Imaan Newspaper

0 Comments