Chukua tahadhari! corona bado ipo na inaua

Karibu tena katika muendelezo wa makala kuhusu ugonjwa hatari wa corona. Pengine wengi wetu hatukuufahamu ugonjwa huu kabla ya mlipuko wa sasa, lakini ni ugonjwa uliogunduliwa miaka mingi na kusababisha milipuko midogo kuanzia mwaka 2003, 2012, 2015 na 2018.
Katika mlipuko wa sasa ambao umeanza takriban miezi minne iliyopita, mataifa yote ya dunia yameathirika na ugonjwa huu.

Takwimu na nchi zilizoathirika zaidi

Wakati nikiandika makala hii Jumanne ya April 7 wiki hii, kulikuwa na zaidi ya wagonjwa Milioni 1.4 na vifo elfu 75 ulimwenguni kote kutokana na ugonjwa huu ambao ulianzia China na kisha kuenea nchi nyengine hususan Bara Ulaya na taifa la Marekani.
Mpaka sasa, orodha ya nchi zenye vifo vingi inaongozwa na Italia, kisha Hispania, halafu zinafuatia Marekani, Ufaransa, Iran, Uingereza, Iran na China. Nchi hizo zimerikodi asilimia 80 ya vifo vyote.
Inadhaniwa kuwa, sababu ya nchi hizo kuathirika zaidi ni pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wazee na wavuta sigara. Inadhaniwa pia kuwa virusi vya corona hushamiri zaidi katika nchi zenye baridi. Corona huenenezwa zaidi na vijana (kutokana na miingiliano mikubwa na watu) ila huwa hatari zaidi kwa wazee na watu wenye magonjwa mengine ya muda mrefu kama vile ukimwi na saratani.
Hata hivyo, takwimu za kuenea ugonjwa huu na vifo zinabadilika haraka mno kiasi kwamba si ajabu nchi zinazoonekana kuwa na maambukizo kidogo hivi sasa huenda zikaongoza kesho! Wakati wa kilele cha maambukizi China, nchi zinazoongoza sasa zilikuwa na wagonjwa wanaohesabika kwa vidole!
Kwa Tanzania, taarifa rasmi za mpaka Jumanne April 7 zinaonesha kuwa, kulikuwa na maambukizi 24 na kifo kimoja, huku watu wawili wakitajwa kupona kabisa.

Hali huenda ikawa mbaya zaidi…

Hata hivyo, wataalamu wa maradhi ya kuambukiza wametabiri madhara makubwa, kama hatua hazitachukuliwa, huku Afrika ikiwa hatarini zaidi kwa sababu ya uduni wa mifumo ya afya na changamoto za maisha zinazofanya mkakati wa kukaa ndani kuwa mgumu kwa watu wengi.
Hii maana yake ni kuwa, tunahitaji kuchukua tahadhari zaidi kuzuia hatari na kumuomba Mwenyezi Mungu atulinde waja wake.

Usidharau, chukua hatua

Ni wazi kuwa wengi wetu hatujaupa uzito wa kutosha ugonjwa huu. Ndugu msomaji, ugonjwa huu bado upo na unasambaa kwa kasi hivyo mimi au wewe tunaweza kuwa wahanga wa ugonjwa huu muda wowote ikiwa hatutochukua hatua.
Njia rahisi ya kujikinga na ugonjwa huu ni kukaa nyumbani; na kutoka kwa sababu maalumu au dharura. Ni vizuri kila mmoja wetu kujitenga mbali na maeneo yenye mikusanyiko hata ya watu watano. Pia ukiona dalili za ugonjwa huu, wahi mapema kutoa taarifa na jitenge na watu ili usiwaambukize wengine. Mengine kuhusu vipimo na namna ya kushughulikia wagonjwa tuwaachie wataalamu na serikali, ambao wamejiandaa vilivyo kukabiliana na janga hilo, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.

credit : islamicftz

0 Comments