Janga la corona lilivyopunguza maasi

Licha ya madhara makubwa yaliyosababishwa na kuenea kwa maradhi ya corona yanayosambazwa na kirusi cha Covid – 19, ikiwemo vifo karibu elfu 18, imegundulika kuwa maradhi haya kwa kiasi kikubwa yamechangia kupunguza maasi duniani na kujenga utangamano wa kifamilia.

Maasi yaliyopungua ni pamoja na kamari, maarufu kama ‘betting’ ambayo inaendana na kutabiri matokeo ya michezo mbalimbali, hususan ile ya ligi kuu za mpira wa miguu duniani katika nchi za Uingereza, Hispania, Italia na Ujerumani.
Kupungua kwa kamari ya utabiri wa mechi kunatokana na kusimamishwa kwa michezo hiyo duniani kote kwa hofu ya watu kuambukizana corona katika mikusanyiko ya watu. Pia katika nchi nyingi, maeneo ya kubashiri matokeo ‘betting‘ pia yamefungwa.

Kampuni za michezo hiyo ya kamari iliyoharamishwa katika Qur’an [5:90] na kuitwa kuwa ni uchafu katika kazi za shetani; tayari yameanza kutangaza mapato waliyopoteza au hasara waliyoingia.
Kwa mujibu wa tovuti ya shirika la habari la CNBC la Marekani, sekta ya kamari ya michezo imepoteza takriban dola za Kimarekani milioni 140 mwisho wa wiki iliyopita kutokana na kukosekana kwa maingizo yanayotokana na mashindano ya mpira wa kikapu ya NCAA.
Hali ni hiyo hiyo katika nchi karibu zote duniani, ikiwemo Uganda ambako gazeti la The Monitor la nchini humo linaripoti kuwa, zaidi ya asilimia 70 ya wacheza kamari ni wale wa kutabiri matokeo katika mechi za
mpira wa miguu za ligi kuu za Ulaya.

Kuhusu kamari, Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi mlioamini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa.” [Qur’ an, 5:90].

Madanguro na ulevi

Maasi mengine yaliyopungua ni zinaa ambapo katika nchi mbalimbali, klabu za usiku, baa na madanguro, matamasha makubwa ya muziki, yamefungwa kwa muda kwa hofu ya maradhi ya corona.
Huko Bangladesh, serikali imefunga madanguro makubwa zaidi duniani yaliyopo katika nchi hiyo mpaka mwezi ujao. Pia, Nevada nchini Marekani, jimbo pekee ambalo ukahaba umeruhusiwa kisheria, madanguro na klabu za usiku zimefungwa na hivyo zinaa kupungua.
Inatajwa kuwa hata makahaba wanaofanya kazi zao nyumbani wamejikuta wakikosa wateja baada ya watu wao kufuta miadi yao, kwa mujibu wa gazeti la Huffington Post.
Nako nchini Kenya, katika jimbo lenye Waislamu wengi la Mombasa, Gavana Hassan Joho mapema katikati ya mwezi huu alitangaza kufunga klabu za usiku kwa siku 30, huku nchi kadhaa za Kiarabu, ikiwemo Falme za Kiarabu, Tunisia, zikipiga marufuku ulevi wa tumbaku kupitia mfumo ‘shisha.’
Katika mfumo huo wa shisha, kunakuwa na chungu kinachochoma kilevi, aidha tumbaku au bangi, na kisha moshi kutolewa kupitia mirija ambayo watu hupokezana, jambo ambalo linahatarisha afya za wavutaji kama baadhi yao wana corona. Kukatazwa kwa shisha kuna maana kuwa ulevi ambao umekatazwa katika Qur’an nao unapungua.
Sio zinaa tu iliyopungua kutokana na kufungwa baa na klabu za usiku bali pia unywaji pombe, ambao pia umekatazwa katika Uislamu. Ulevi ni katika maasi yaliyotajwa kuwa ni ‘uchafu katika kazi za shetani’ katika aya ya Qur’an tuliyotangulia kuitaja [5:90].
Zinaa ni katika maasi makubwa katika Uislamu ambapo Mwenyezi Mungu ameonya wanadamu wasiikaribie, achilia mbali kuifanya. Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an:

“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya.” [Qur’ an, 17:32].
Kutokana na ubaya wa zinaa, Mwenyezi Mungu ameweka adhabu kali kwa wazinifu:
<

“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini.” [Qur’an, 24:2].
Jambo la kufurahisha ni kuwa, marufuku za maasi mbalimbali – klabu za usiku, madanguro, kasino, shisha, baa, maeneo ya kuchezea kamari, matamasha ya muziki – zimewekwa kila nchi duniani, za Kiislamu na hata zisizo za Kiislamu, jambo linaloonesha ufalme wa Mwenyezi Mungu.
Akielezea hali hii, Mwenyekiti wa Kamati ya Fat-wa wa Umoja wa Wanazuoni wa Afrika, Dkt. Mohamed Loh amesema ugonjwa wa Corona umethibitisha kwamba nchi zina uwezo wa kuzuia aina zote za uovu; kufunga baa, vilabu vya usiku na madanguro na pia nchi zina uwezo wa kutekeleza sheria za Kiislamu.

Dkt. Loh alisema: “Utangamano wa familia umezidi kuimarika, jambo linaloonaesha gonjwa hili limefichua kuwa kumbe inawezekana kuishi bila kuwa na kumbi za starehe, baa, matamasha, na kampuni za Kamari. Hoja kwamba watu hawako tayari kukubali sharia ni hoja isiyo sahihi.”
Dkt. Loh alisema imebainika kwamba, yote hayo yanawezekana ikiwa suala linahusu maslahi ya maisha ya duniani!
Kwa upande wake, Sheikh Izudin Alwy Ahmed ameitaka jamii kuacha kuogopa maradhi ya corona bali wachukue tahadhari, akisisitiza kuwa anayepaswa kuogopwa ni Allah pekee.

“Kwanini leo hii tunakuwa na hofu na maradhi badala ya kumuogopa aliyeleta maradhi hayo, usiogope maradhi muogope aliyesababisha hayo maradhi, na hutakuwa na hofu siku ya mwisho,” alisema Sheikh huyo.
Alisema Mwenyezi Mungu amechukua ahadi ya kutopambanisha hofu mbili, kwamba mtu akawa na hofu ya Mwenyezi Mungu duniani, hatokuwa na hofu Akhera.

“Angalia mambo mangapi ambayo tulikuwa tumekatazwa kwa ajili ya Allah lakini tumekuwa tukiyafanya. Leo hii tunakatazwa kwa ajili ya corona tunakubali kuyaepuka. Kweli sisi tunastahiki kuitwa ni watu tunayemuogopa Mungu, tunastahiki kuitwa ni watu ambao tunamuogopa Allah Jalla Jalaaluhu?” alisema Sheikh Izudin Alwy.

“Waislamu wengi sasa wamekuwa wakitii maelekezo kwa sababu ya corona. Mtii Mola wako kwa ajili anastahiki kutiiwa, muogope Mola wako kwa sababu anastahiki kuogopwa. Usiogope maradhi ila tahadhari na maradhi,” alisema.

0 Comments