Jinsi Ya Kuipata Taqwaa Katika Ramadhwaan

Maana ya Taqwaa daima huambatana na ibaadah katika Qur-aan, 'Ibaadah maana yake ni kufanya yale Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyotuamrisha na kuepukana na yale Aliyotukataza. 'Ibaadah pia inamaanisha vitendo vyote ambavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anapenda na kukubali kama ni matendo ya moyo, ulimi, au maungo. Kwa hiyo Taqwaa inaambatana na kufanya yaliyokuwa sawa na yasiyokuwa sawa. Taqwaa ni tunda la kufanya vitendo vya 'Ibaadah. Kwa maneno mengine, ikiwa mmoja atafanya Allaah aloamrisha, na kukaa mbali na aliyoyakataza, itakuwa kapata Taqwaa. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kataja katika kitabu Chake:
{{Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Swawm, kama walivyoandikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah}} Al-Baqarah 2:183

Katika Aayah hii na nyingi nyengine, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuonyesha kuwa Taqwaa ni matokeo au matunda ya kufanya vitendo vyema vya 'Ibaadah.

Maana ya Taqwaa
Baada ya kuwa tushafafanua jinsi gani ya kupata Taqwaa, tutaainisha nini maana ya mada ya Taqwaa. Taqwaa maana yake: ni kusafisha moyo au nafsi. Jambo hili limethibitika katika baadhi ya Aayah katika Surat Ash-Shams ambapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kasema:
{{Naapa kwa jua na mwangaza wake. Na kwa mwezi unapolifuatia. Na kwa mchana unapolidhihirisha. Na kwa usiku unapolifunika. Na kwa mbingu na kwa aliyeijenga. Na kwa ardhi na kwa aliyeitandaza. Na kwa nafsi na kwa aliyeitengeneza. Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake, Hakika amefanikiwa aliyeitakasa,Na hakika amekhasiri aliyeiviza.}} Ash-Shams 91:1-10
Allaah (Subhanahu wa Ta'ala) Kaanza katika Surah hii kwa kuapa viapo saba. Popote Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anapoanza Surah kwa kuapa, Yeye (Subhaanahu wa Ta'ala) Hufanya hivyo kwa kutuonyesha chochote kitachofuatia baada ya hapo ni muhimu sana kwetu kukifahamu na kukifuata. Kwa hivyo, tuwe makini sana kwa kinachosemwa, na tuwaze maana yake. Kusafisha mmoja moyo wake na kusafisha nafsi, mmoja lazima atekeleze vitendo vyema ambavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anapenda sisi tufanye, na angamizo huwepo katika kufanya vitendo ambavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katukataza. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni Muongozi na Mlindaji wa Nafsi, tunahitajika kufanya kila kitendo chema kwa kutegemea rehma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kuogopa adhabu Zake, kuwa na imani dhabiti na kumuamini.
 
Usafishaji wa Nafsi

Miongoni mwa ujumbe wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kamtuma na amri ya kuzisafisha nafsi za Waislamu hususan, na binaadam wote kwa ujumla. Allaah (Subhanahu wa Ta'ala) Kasema:
{{Yeye Ndiye Aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, awasomee Aya Zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, japokuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri.}} Al-Jumu'ah 62:2

Katika Aayah hii tunapata mambo matatu muhimu,
1. Kufundisha Qur-aan,
2. Kufundisha Sunnah,
3. Kuonyesha njia ya kujisafisha nafsi.

Usafi huu unapatikana kwa kufanya matendo ya 'Ibaadah na kujiepusha na madhambi na maasi.

Kanuni za kupata Taqwaa
Jinsi gani mtu anaweza kujua kuwa vitendo vyake vya 'Ibaadah vitamsaidia kupata Taqwaa? Kukuza Taqwaa, mtu lazima atimize kanuni zifuatazo:

1) Ikhlaas, niyyah ya dhati kuwa vitendo vinavyofanywa ni kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Pekee, kwa mapenzi naye, ambapo wakati huo huo unategemea malipo na rehma Zake, pamoja na kuogopa ghadhabu na adhabu Zake.
2) Kufanya vitendo kwa kadiri ya Sunnah sahihi inavyosema. Kuwa na elimu ya lazima ya 'Ibaadah inayotekelezwa. Kujua jinsi gani Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kafanya vitendo hivyo na wakati muwafaqa wa kufanywa vitendo hivyo.
Ikhlaas, ni lazima iwepo wakati ule wa kabla kitendo kinapofanywa na baada ya kufanya kitendo hicho, bila ya riyaa au sum'ah (kufanya mambo kwa kujionyesha au kutaka kujulikana na watu). Kwa mfano, baada ya kufanya kitendo chema, mmoja asiseme kwa wengine, "Angalia mema yote ninayofanya", au "Mimi hasa ni mtu bora kwa sababu nafanya hichi na kile."

Ukiufuata mfumo huu wa kisayansi wa kuipata Taqwaa, na kuhakikisha unatekeleza masharti yake na haki zake, basi bila shka yoyote utaipata hiyo Taqwaa in shaa Allaah.

0 Comments