Kisa Cha Nabii Ibraahiym عليه السلام - Sehemu Ya 2


www.muislamublog.com

DA'WAH KWA BABA YAKE


Ibraahiym عليه السلام alikuwa akiumia kupita kiasi kumuona baba yake (Au ‘ammi yake aliyemlea kama walivyonukuu baadhi ya Mufassiriyn) kuwa anaabudu masanamu. Bali akiumia zaidi kwani yeye huyo baba yake ndiye aliyekuwa akichonga hayo masanamu. Hii ni tabia ya mwenye kufanya da'wah anapoona jamaa zake wenyewe wako katika upotofu na khaswa inapokuwa jamaa aliye karibu zaidi kama baba, mama, ndugu, watoto na kadhalika. Kwa hiyo, lilikuwa tamanio lake kubwa kumtoa baba yake kutoka katika upotofu na kumuingiza katika Tawhiyd. Akamuita kwa maneno ya upole kabisa na kumpa kila hoja ili atambue upotofu huo:  
  ((إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا))
  ((يَا أَبَتِ إِنِّي قَدْ جَاءنِي مِنَ الْعِلْمِ مَا لَمْ يَأْتِكَ فَاتَّبِعْنِي أَهْدِكَ صِرَاطًا سَوِيًّا))
  ((يَا أَبَتِ لَا تَعْبُدِ الشَّيْطَانَ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلرَّحْمَنِ عَصِيًّا))
  ((يَا أَبَتِ إِنِّي أَخَافُ أَن يَمَسَّكَ عَذَابٌ مِّنَ الرَّحْمَن فَتَكُونَ لِلشَّيْطَانِ وَلِيًّا))
 ((Alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyosikia, na visivyoona, na visivyokufaa chochote?)) 
((Ewe baba yangu! Kwa yakini imenifikia ilimu isiyokufikia wewe. Basi nifuate mimi, nami nitakuongoza Njia Iliyo Sawa)) 
((Ewe baba yangu! Usimuabudu Shaytwaan. Hakika Shaytwaan ni mwenye kumuasi Mwingi wa Rahamah))  
 ((Ewe baba yangu! Hakika mimi naogopa isikupate adhabu inayo toka kwa Mwingi wa Rahmah ukaja kuwa mwenziwe Shaytwaan))  [Maryam: 41-45]
Lakini baba yake  Ibraahiym عليه السلام  hakutaka kuacha ibada yake na hakupendezewa na wito wa mwanawe, na ingawa Ibraahiym عليه السلام alimuita kila mara kwa upole na adabu kabisa kama aya hizo za juu "Ewe baba yangu", baba yake hakumjibu kwa upole wala hakuonyesha adabu baina ya baba na mtoto, bali alimtisha kuwa akiendelea kumwita katika ibada yake atamfukuza na kumpiga mawe,  
 ((قَالَ أَرَاغِبٌ أَنتَ عَنْ آلِهَتِي يَا إِبْراهِيمُ لَئِن لَّمْ تَنتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا))
 (((Baba) akasema: Unaichukia miungu yangu, ewe Ibraahiym Kama huachi, basi lazima nitakupiga mawe. Na niondokelee mbali kwa muda!)) [Maryam:46]
Hata hivyo Ibraahiym عليه السلام  anatupa mafunzo makubwa hapa kuwa juu ya kwamba alimuita baba yake kwa upole na adabu kisha baba yake akamjibu kwa kumkemea, majibu ya Ibraahiym   عليه السلام yalikuwa ni ya uzuri zaidi kwa kumtakia amani iwe juu yake na kumuombea kwa Allaah سبحانه وتعالى Amghufurie. 
 ((قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا))
 ((وَأَعْتَزِلُكُمْ وَمَا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّهِ وَأَدْعُو رَبِّي عَسَى أَلَّا أَكُونَ بِدُعَاء رَبِّي شَقِيًّا))   
(((Ibraahiym) akasema: Salamun ‘alayka! Amani iwe juu yako! Mimi nitakuombea msamaha kwa Mola wangu. Hakika Yeye Ananihurumia sana))
((Nami najitenga nanyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Allaah. Na ninamwomba Mola wangu ; asaa nisiwe mwenye kukosa bahati kwa kumwomba Mola wangu ))   [Maryam:47-48]

BABA YAKE IBRAAHIYM عليه السلام ATAGEUZWA KUWA FISI
SIKU YA QIYAAMAH NA KUTUPWA MOTONI

Ibraahiym عليه السلام alijiombea Du'aa mwenyewe na kumuombea baba yake:  
 
 رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿83﴾ وَاجْعَل لِّي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الْآخِرِينَ ﴿84﴾ وَاجْعَلْنِي مِن وَرَثَةِ جَنَّةِ النَّعِيمِ ﴿85﴾ وَاغْفِرْ لِأَبِي إِنَّهُ كَانَ مِنَ الضَّالِّينَ ﴿86﴾ وَلَا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ ﴿87﴾ يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿88﴾ إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿89
((Mola wangu ! Nitunukie hukumu na Uniunganishe na watendao mema))
((Na Unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakaokuja baadaye)) 
((Na Unijaalie katika warithi wa Bustani za neema))
((Na Umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu)) 
((Wala Usinihizi Siku watakapofufuliwa))
((Siku ambayo kwamba mali hayatofaa kitu wala wana))  
((Isipokuwa mwenye kumjia Allaah na moyo safi))
[Ash-Shu'araa: 83-89]
Tunaona kwamba katika Du'aa hizo Ibraahiym عليه السلام amemuombea baba yake maghfira kwa Allaah سبحانه وتعالى  Na Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

((وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلاَّ عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِلّهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لأوَّاهٌ حَلِيمٌ))
((Wala haikuwa Ibraahiym kumtakia msamaha baba yake ila kwa sababu wa ahadi aliyofanya naye. Lakini ilipo mbainikia kwamba yeye ni adui ya Allaah, alijiepusha naye. Hakika Ibraahiym alikuwa mwingi wa kuomba, mnyenyekevu, mvumilivu)) [At-Tawbah:114]
Ibn 'Abbaas رضي الله عنه  amesema: "Ibraahiym عليه السلام aliendelea kumuomba Allaah سبحانه وتعالى  Amsamehe baba yake mpaka alipokufa. Baada ya hapo alipotambua kwamba baba yake amekufa akiwa ni adui ya Allaah, akajitenga naye".   [At-Twabariy 14.519]
Katika kauli ya
((وَلاَ تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ))
((Wala Usinihizi Siku watakapofufuliwa)) [Ash-Shu'araa 87]
Imaam Al-Bukhaariy amesimulia Hadiyth ifuatayo:
عن أبي هريرة، رضي الله عنه، عن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((إن إبراهيم رأى أباه يوم القيامة عليه الغَبَرَةُ والقَتَرَةُ))  البخاري 4768
Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه  kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:  (Ibraahiym atamuona baba yake siku ya Qiyaamah akiwa amefunikwa na vumbi na kiza)) [Al-Bukhaariy 4768]
Usimulizi mwingine kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema:
))يلقى إبراهيم أباه، فيقول: يا رب، إنك وعدتني أنك لا تخزيني يوم يبعثون. فيقول الله: إني حرمت الجنة على الكافرين))
((Ibraahiym atakutana na baba yake na atasema: "Ee Mola, Umeniahidi kwamba Hutonihizi siku watakaofufuliwa viumbe vyote". Allaah Atasema: "Nimeiharamisha Pepo kwa makafiri")) [Fat-h Al-Baariy 8:357]
Usimulizi mwingine vile vile:
((يلقى إبراهيم أباه آزر يوم القيامة، وعلى وجه آزر قَتَرَةٌ وغَبَرة، فيقول له إبراهيم: ألم أقل لك: لا تعصني فيقول أبوه: فاليوم لا أعصيك. فيقول إبراهيم: يا رب، إنك وعدتني ألا تخزيني يوم يبعثون، فأي خزي أخزى من أبي الأبعد؟ فيقول الله تعالى: إني حرمت الجنة على الكافرين. ثم يُقال: يا إبراهيم، ما تحت رجليك؟ فينظر فإذا هو بذبح متلطخ، فيؤخذ بقوائمه فيلقى في النار)) البخاري 3350.
((Ibraahiym atakutana na baba yake Aazar siku ya Qiyaamah na kutakuweko na vumbi na kiza usoni mwa Aazar. Ibraahiym atamuambia: "Sikukuambia kwamba usiniasi?". Baba yake atasema: "Leo sikuasi". Ibraahiym atasema: "Ewe Mola, Umeniahidi kwamba hutonihizi siku watakaofufuliwa, lakini hizaa gani itakuwa kubwa zaidi ya kumuona baba yangu katika hali hii?". Allaah Atamuambia: "Nimeharamisha Pepo kwa makafiri". Kisha itasemwa: "Ewe Ibraahiym! Tazama chini ya miguu yako". Atatazama na ataona (kwamba baba yake amebadilishwa kuwa) fisi amefunikwa katika samadi/kinyesi, atachukuliwa kwa miguu yake na kutupwa motoni)) [Al-Bukhaariy 3350 katika kunukuliwa na Fat-h Al-Baariy 6:445]
Kugeuzwa baba yake Ibraahiym kuwa fisi ni Rahma kutoka kwa Allaah ili Ibraahiym عليه السلام asimuone baba yake katika sura yake akiwa anatupwa motoni. 

KUVUNJA MASANAMU  
Allaah سبحانه وتعالى Anatuambia kuhusu Khaliyl Wake Ibraahiymعليه السلام na vipi Alivyomjaalia uongofu tokea zamani yaani tokea udogoni mwake. Alimpa moyo kwa kumuonyesha haki na dalili dhidi ya watu wake kwa yale waliokuwa wakiabudu kama Anavyosema:
((وَتِلْكَ حُجَّتُنَا آتَيْنَاهَا إِبْرَاهِيمَ عَلَى قَوْمِهِ))
 ((Na hizo ndizo hoja Zetu Tulizompa Ibraahiym kuhojiana na watu wake)) [Al-An'aam:83]
Na kumpa uongofu tokea alipokuwa mdogo Anasema Allaah سبحانه وتعالى  
((وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِن قَبْلُ وَكُنَّا بِه عَالِمِينَ))
((Na hakika Tulikwishampa Ibraahiym uwongofu wake zamani, na Tulikuwa tunamjua)) [A-Anbiyaa:51]
Na ndio maana alipokuwa mdogo alikuwa anashangazwa na ibada yao ya masanamu, akiyaendea masanamu hayo kuyatazama na kuona jinsi walivyokuwa wapumbavu watu wake kuabudu mawe yaliyochongwa ambayo akiona kuwa hayawezi kuwafaa kitu wala kuwadhuru kitu.
Akaapa Ibraahiym عليه السلام kuwa atayavunja haya masanamu, na alipoapa kiapo hicho mmoja wa watu wake alimsikia. Walikuwa wana sikukuu ambayo walikuwa wakienda wote kusherehekea. Yeye akabakia, na walipomuuliza sababu ya kutokwenda aliwajibu kuwa anaumwa. 
((فَنَظَرَ نَظْرَةً فِي النُّجُومِ)) 
 
 ((فَقَالَ إِنِّي سَقِيمٌ)) 
((Kisha akapiga jicho kutazama nyota)) 
 ((Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa!)) [As-Swaaffaat: 88-89]
Ilikuwa siku moja baada ya kuapa kuwa atayavunja masanamu.  Watu wake wakatoka kwenda kwenye sherehe zao, huku nyuma Ibraahiym عليه السلام akayavunja masanamu yote isipokuwa sanamu kubwa kabisa, akachukua shoka alilotumia kuwavunjia na kuliweka katika mikono ya hilo sanamu kubwa ili watu wafikiri kuwa hilo sanamu ndilo lililovunja masanamu mingine. 
 ((وَتَاللَّهِ لَأَكِيدَنَّ أَصْنَامَكُم بَعْدَ أَن تُوَلُّوا مُدْبِرِينَ))  
 
((فَجَعَلَهُمْ جُذَاذًا إِلَّا كَبِيرًا لَّهُمْ لَعَلَّهُمْ إِلَيْهِ يَرْجِعُون))
((Na Wallahi! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya baada ya mkishageuka kwenda zenu))
((Basi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili wao walirudie)) [Al-Anbiyaa: 57-58]
Walikuwa wanawaekea chakula masanamu yao na alipokwenda kuyavunja masanamu Ibraahiym عليه السلام aliyasemesha na kuyauliza masanamu kwa kejeli,
((فَتَوَلَّوْا عَنْهُ مُدْبِرِينَ))
 
((فَرَاغَ إِلَى آلِهَتِهِمْ فَقَالَ أَلَا تَأْكُلُونَ))
 
((مَا لَكُمْ لَا تَنطِقُونَ))
 
((فَرَاغَ عَلَيْهِمْ ضَرْبًا بِالْيَمِينِ))
((Nao wakamwacha, wakampa kisogo))
((Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli?)) 
((Mna nini hata hamsemi?)) 
((Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia)) [As-Swaaffaat: 90-93]
Waliporudi wakapatwa na mshangao mkubwa kuona miungu yao imevunjwa! 

(( قَالُوا مَن فَعَلَ هَذَا بِآلِهَتِنَا إِنَّهُ لَمِنَ الظَّالِمِينَ))
 
(( قَالُوا سَمِعْنَا فَتًى يَذْكُرُهُمْ يُقَالُ لَهُ إِبْرَاهِيمُ))
 
((قَالُوا فَأْتُوا بِهِ عَلَى أَعْيُنِ النَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَشْهَدُونَ))    
 
 ((قَالُوا أَأَنتَ فَعَلْتَ هَذَا بِآلِهَتِنَا يَا إِبْرَاهِيمُ))
 
  ((قَالَ بَلْ فَعَلَهُ كَبِيرُهُمْ هَذَا فَاسْأَلُوهُمْ إِن كَانُوا يَنطِقُونَ))  

((Wakasema: Nani aliyeifanyia haya miungu yetu? Hakika huyu ni katika waliodhulumu))
((Wakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibraahiym))
((Wakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia!)) 
((Wakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe Ibraahiym?)) 
((Akasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni ikiwa wanaweza kutamka)) [Al-Anbiyaa:59-63]
Wakajirudi kidogo kuwaza kwamba kweli walikuwa wanaabudu miungu isioweza hata kujikinga na madhara, lakini kuwaza kwao kulikuwa kwa muda mdogo, kisha wakarudi katika upotofu ule ule,

((فَرَجَعُوا إِلَى أَنفُسِهِمْ فَقَالُوا إِنَّكُمْ أَنتُمُ الظَّالِمُونَ))
 
 ))ثُمَّ نُكِسُوا عَلَى رُؤُوسِهِمْ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا هَؤُلَاء يَنطِقُونَ))
 
((قَالَ أَفَتَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّهِ مَا لَا يَنفَعُكُمْ شَيْئًا وَلَا يَضُرُّكُمْ))  
 
(( أُفٍّ لَّكُمْ وَلِمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّهِ أَفَلَا تَعْقِلُونَ))   
((Basi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa madhaalimu!)) 
((Kisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema: Wewe unajua kwamba hawa hawesemi)) 
((Akasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiyekuwa Allaah wasiokufaeni kitu wala kukudhuruni?)) 
((Aibu yenu nyinyi na hivyo mnavyoviabudu badala ya Allaah! Basi nyinyi hamtii akilini))  [Al-Anbiyaa: 64-67]
Hii ndio ilikuwa sababu khaswa ya Ibraahiym عليه السلام ya kuyavunja hayo masanamu ili wajiulize na watambue ujinga wao wa kuabudu vitu visivyosema na wala visivyoweza kujihifadhi na madhara.   

IBRAAHIYM  عليه السلامANAINGIZWA KATIKA MOTO

Hapo tena ndipo walipotaka kumchoma moto,
((قَالُوا حَرِّقُوهُ وَانصُرُوا آلِهَتَكُمْ إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ))
((Wakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo!)) [Al-Anbiyaa:68]
Wakakusanya kuni nyingi kabisa za kuandaa moto mkubwa.  Wakachimba shimo na ukawashwa moto uliowaka kwa cheche kubwa, moto ambao haujapata kuwashwa moto kama huo kabla wakamtia Ibraahiym عليه السلام
Yafuatayao ni maelezo mbali mbali kuhusu tukio hilo:
-Bwana mmoja Mkurdi  aliyekuwa ni mhamajihamaji, ambaye ametokea  Persia, alitoa rai kuwa Ibraahiym عليه السلام atiwe katika manati kubwa (chombo cha kurushia mawe)   [Al-Qurtubiy 11:303] 
-Shu'ayb Al-Jabaa'i kasema:  (Bwana huyo) "Jina lake alikuwa ni Hayzan na kwa sababu ya rai yake hiyo aliyotoa, Allaah سبحانه وتعالى  Kamjaalia kumezwa na ardhi na ataendelea kudidimia hadi siku ya Qiyaamah.
Alipotumbukizwa Ibraahiym عليه السلام katika moto alisema:
حَسْبُنا اللَّه وَ نِعْم الْوَكِيل
"Ananitosheleza Allaah na Yeye Ndiye Mbora wa kupanga mambo yangu" [At-Twabariy 18:465]
-Inavyosemekana kuwa zilikusanywa kuni kwa muda wa mwezi na alipotupwa kwenye moto huo alikuja Jibriyl عليه السلام akasema: Ewe Ibraahiym, una haja yoyote? Akajibu: Ama kwako la!
حَسْبِيَ اللَّه وَنِعْمَ الْوَكِيِل
Hasbiya-Llahu Wa Ni'mal-Wakiyl [Aysarut-tafaasiyr – Abu-Bakkar Al-Jazaairiy 3:426]
Kutokana na wingi wa kuni zilizokusanywa ilifika hadi watu kuweka nadhiri, ya kupeleka kuni. 
-As-Sudi kasema:"Mwanamke alipokuwa akiumwa akiweka nadhiri kuwa akipona ataleta kuni za kumuunguza Ibraahiym عليه السلام.[Al-Qurtubiy 11:303]
-Kutokana na Hadiyth ifuatayo Sahiyh, baadhi ya Mufassiriyn wamesema kwamba fadhila hii ya kuwa Ibraahiym عليه السلام atakuwa ni mtu wa kwanza kuvishwa nguo, ni kwa sababu yakutiwa motoni bila ya sababu yoyote ya haki bali kwa kushikilia tawhiyd na kukanusha shirk:   
عن ‏ ‏ابن عباس ‏ ‏رضي الله عنهما ‏ عن النبي ‏ ‏صلى   الله عليه وسلم ‏ ‏قال:((إنكم محشورون  حفاة عراة غرلا ثم قرأ ((كما بدأنا أول خلق نعيده)) وأول من يكسى يوم القيامة  إبراهيم)) البخاري ومسلم

Imetoka kwa Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :
amesema: ((Mtafufuliwa bila ya viatu, uchi nabila ya kutahiriwa (khitaan) kisha akasoma: ((Kama Tulivyoanza umbo la awali tutalirudisha tena)) na wa kwanza kuvalishwa nguo siku ya Qiyaamah ni Ibrayhim)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
-Sa'iyd bin Jubayr karipoti kwamba Ibn 'Abbaas kasema:  "Ibraahiym عليه السلام alipotupwa katika moto, Malaika wa mvua alisema: Lini nitaruhusiwa kuteremsha mvua?  Lakini Allaah سبحانه وتعالى  Alijibu haraka kama aya inavyosema:
 ((قُلْنَا يَا نَارُ كُونِي بَرْدًا وَسَلَامًا عَلَى إِبْرَاهِيم))
((Sisi tukasema: Ewe Moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibraahiym!)) [Al-Anbiyaa: 69]
-Na kwa maneno hayo ya Allaah سبحانه وتعالى hakuna moto uliokuwa ukiwaka duniani wakati huo ila ulizimwa [At-Twabariy 18:466]
-Ibn 'Abbaas na Abu Al-Aliyah kasema: "Ingelikuwa Allaahسبحانه وتعالى Hakusema (Hakuuambia moto) : 
((وَسَلَامًا))
((Na salama))
Ibraahiym عليه السلام angelidhurika kwa ubaridi wake    [At-Twabariy 18:466, 465]
-Qataadah amesema: "Siku hiyo hakikuweko kiumbe kisichojaribu kuuzima moto wa Ibraahiym عليه السلام ila mjusi" [At-Twabariy 18:467].
-Az-Zuhriy kasema: "Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliamrisha kuwa (mjusi) auliwe na akaitwa 'mnyama mharibifu' [At-Twabariy 18:467 na pia imesimuliwa katika Muslim Namba 2238]
Mbinu zao za kutaka kumuunguza Ibraahiym عليه السلام katika moto hazikufaulu kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى
((وَأَرَادُوا بِهِ كَيْدًا فَجَعَلْنَاهُمُ الْأَخْسَرِينَ)) 
((Wao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio
 waliokhasirika)) [Al-Anbiyaa:70]
Moto ukamalizika kuwaka, watu wakiwa wanasubiri kwa hamu kubwa waone majivu tu, lakini dhana yao iliwashtua, na walitahayarika walipomuona Ibraahiym عليه السلام anatoka salama mbele ya macho yao akitembea mzima bila ya kudhurika popote.  Ni muujiza mkubwa hakika!
Lakini kama kawaida ya hali ya watu wa zamani walivyokuwa na ukaidi wao hawakumuamini Ibraahiym عليه السلام na wito wake wa ibada ya Tawhiyd kwamba kuna Mungu Apasaye kuabudiwa Pekee, Mungu Aliyefanya maajabu haya ya Moto  kutokumuunguza Ibraahiym  عليه السلام.

IBRAAHIYM  عليه السلام ANAHAMA IRAQ KUELEKEA SHAAM

Hakuamini mtu isipokuwa Luwtw عليه السلام ambaye alikuwa ni binamu (cousin) wake, na mke wake Saarah.   
((فَآمَنَ لَهُ لُوطٌ وَقَالَ إِنِّي مُهَاجِرٌ إِلَى رَبِّي إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ))
((Luwtw akamuamini, na akasema: Mimi nahamia kwa Mola wangu. Hakika Yeye Ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hikmah)) [Al'Ankabuut: 26]
Vile vile akasema Ibraahiym عليه السلام :
((وَقَالَ إِنِّي ذَاهِبٌ إِلَى رَبِّي سَيَهْدِينِ))
 
 ((رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ))
((Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu ; Yeye Ataniongoa))
((Ewe Mola wangu! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema))[As-Swaaffaat:99-100]
Hapo tena Allaah سبحانه وتعالى Akamhamisha na kumpeleka Shaam  nchi ambayo ndio iliyokusudiwa kuwa 'nchi Tulioibariki'.
((وَنَجَّيْنَاهُ وَلُوطًا إِلَى الْأَرْضِ الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا لِلْعَالَمِينَ))
((Na Tukamwokoa yeye na Luwtw Tukawapeleka kwenye nchi tulioibariki kwa ajili ya walimwengu wote)) [Al-Anbiyaa:71]
Na kutokana na Du'aa yake hiyo ya:
((رَبِّ هَبْ لِي مِنَ الصَّالِحِينَ))
((Ewe Mola wangu! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema))[As-Swaaffaat:100]
Allaah سبحانه وتعالى Akamjaaliya kupata watoto kama aya zifuatazo zinavyotuelezea:
((فَبَشَّرْنَاهُ بِغُلَامٍ حَلِيمٍ))
((Basi Tukambashiria mwana aliye mpole)) [As-Swaaffaat:101] 
Aya hii imekusudiwa ni Ismaa'iyl عليه السلام
Na katika Aayah nyingine Amesema Allaah سبحانه وتعالى :
((وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَقَ وَيَعْقُوبَ نَافِلَةً وَكُلًّا جَعَلْنَا صَالِحِينَ))  
((Naye Tukampa Is-haaq, na Ya'quwb kuwa ni ziada. Na wote Tukawajaalia wawe watu wema)) [Al-Anbiyaa:72]
'Atwaa' na Mujaahid wamesema:  "Naafilatan (Na ziada) ina maana kwamba zawadi" [At-Twabariy 18:471]
Ibn 'Abbaas na Qataadah wamesema: "Zawadi ya mtoto mwenye mtoto, maana kwamba Ya'aquub alikuwa mtoto wa Is-haaq kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى :
((فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَقَ وَمِن وَرَاء إِسْحَقَ يَعْقُوبَ))
((Basi Tukambashiria (kuzaliwa) Is-haaq, na baada ya Is-haaq Ya'quwb))[Huud:71]

 Kisa kinaendelea .....3

0 Comments