Waislamu tuwe wavumilivu yanapotokea majanga

Katika maisha ya binadamu yeyote kuna nyakati kuu mbili, za raha na shida. Kila mwanadamu atambue kuwa atakabiliwa na moja kati ya hali hizo mbili.
Wapo wanaokata tamaa wakati wa huzuni na kufanya mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine yanawafanya wawe na huzuni; na pia kuna wanaotumia vibaya nyakati za furaha na hatimaye kuingia kwenye huzuni isiyokoma.
Vijana wengi huchanganywa na nyakati hizi (wakati wa shida na raha) na kushindwa kuamua kama wanataka wasonge mbele, warudi nyuma au wawe watumwa wa watu au vitu fulani. Yapo mambo mengi ambayo yanapaswa kufanywa ili kukabiliana na kipindi cha huzuni.
Miongoni mwa mambo hayo ni kuamini kuwa hakuna magumu yanayomfika mtu bila sababu maalumu. Allah Mtukufu anasema: “Na misiba inayokupateni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu. Naye (Mwenyezi Mungu) anasamehe mengi.” [Qur’an, 42:30]. Cha kujifunza baada ya majanga kupita ni kutosahau nyakati za huzuni kwa sababu zitajirudia wakati wowote.

Hofu ni mtihani

Kuibuka kwa virusi vya corona (Covid – 19) ni miongoni mwa mitihani mizito ambayo Allah ameikadiria kuwafikia waja ili wapate kumkumbuka kama anavyosema: “Na bila shaka tutawaonjesha adhabu ndogo kabla ya adhabu kubwa. Huenda wakarejea kwa kutubia.” [Qur’an, 32:21].
Virusi vya corona vimeendelea kusababisha hofu na mashaka kote ulimwenguni kutokana na kuenea kwake kwa haraka katika kipindi cha muda mfupi. Hii ni kwa sababu, hofu ni suala linalofungamana na hekima ya kuumbwa kwa mwanadamu na kuwepo kwake katika maisha haya ya duniani.
Allah anatuambia: “Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya hofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanaosubiri. Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye tutarejea. Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola Wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka.” [Qur’an, 2: 155–157].
Muislamu anaposhindwa kuvaa nguo ya ushujaa na kukabiliana na vikwazo na majaribu hatoweza kupambana na mitihani ya ulimwengu.

Hofu iliyopitiliza ni alama ya unafiki

Hofu ni hali ya kisaikolojia na kitabia iliyopo ndani ya nafsi ya mwanadamu. Licha ya kuwepo ikhtilafu baina ya wataalamu wa elimu ya saikolojia wa sasa na wa zamani juu ya maana halisi ya hofu, wataalamu wa kale wa elimu ya saikolojia wanaona kwamba hofu ni matamanio na matakwa binafsi ya mtu.
Hata hivyo, wataalamu wa sasa wanalipinga hilo wakisema kwamba hofu ni muelekeo wa kitabia au haja ya kiasili inayokubali mabadiliko. Wanasema pia kuwa, hakuna matakwa na matamanio ya hofu, bali kuna hali ya wasiwasi na hofu katika maisha ya mwanadamu ambayo ni kinga ya nafsi dhidi ya hatari za walimwengu.

Tofauti iliyopo

Baadhi ya watu hudhani kuwa tofauti kubwa iliyopo baina ya Muumini na asiyekuwa Muumini ipo katika itikadi na mambo ya kiibada. Waumini wana itikadi yao maalumu juu ya ulimwengu na wanajilazimisha kufanya mambo mbalimbali ya kiibada wakati wale wasioamini Mungu hawashikamani na misingi yoyote ya dini wala hukumu zake.
Tofauti hizi ni za kweli na sahihi lakini kuna tofauti nyingine inayojitokeza kati ya watu hao wawili. Qur’an Tukufu na Hadithi za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) vimeliweka kundi la Waumini upande mmoja na kuliweka kundi la makafiri pamoja na wanafiki upande mwingine.
Hii ni sawa na kusema, itikadi na ibada vyote vinalenga kuzibainisha tofauti zilizopo kati ya makundi hayo mawili. Alama hizo kubwa (aqida na ibada) ambazo zinafungamana na imani ndio kioo cha imani katika nafsi ya mwanadamu. Muumini anakuwa na nafsi iliyokamilika na asiyekuwa Muumini nafsi yake hukumbwa na hofu.
Hofu ni tatizo ambalo hutofautiana kati ya nafsi ya Muumini na nafsi ya asiyekuwa Muumini. Muumini wa kweli na aliyekamilika huepukana na tatizo la hofu na kasoro yoyote haingii katika nafsi yake kwa sababu kumuogopa asiyekuwa Allah ni jambo linalopingana na imani yake. Kwa sababu hii, Mwenyezi Mungu anatuonya kwa kutuambia:
“Hakika huyo ni Shetani anawatia hofu marafiki zake, basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi (Mola wenu) ikiwa nyinyi ni Waumini.” [Qur’an, 3: 175].

0 Comments