Nasaha Kwa Vinyozi

Kazi ya unyozi ni kazi ambayo asli yake ni halali, lakini ni kazi ambayo imeingizwa uharamu mwingi sana na waifanyao kazi hiyo. Aidha kwa kuiga wasio Waislamu katika utekelezaji wa kazi hiyo, au kwa ujinga na kukosekana ufuatwaji wa mafunzo sahihi ya kishariy’ah katika kuitekeleza kazi hiyo.


Aghlabu mtu anapokwenda kwa vinyozi wengi hukutana na mambo yafuatayo ya haramu:

1.      Kunyolewa watu nywele kwa mitindo mbalimbali ya kuiga makafiri na watu wasio na maadili, unyoaji ambao unapingana na shariy’ah na mafunzo aliyofundisha mbora wa viumbe, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

2.      Unyoaji wa ndevu.

3.      Unyoaji wa nyusi.

4.      Vikao vya usengenyaji na umbea. Kuweka miziki na televisheni.

5.      Aghlabu vinyozi wengi hukosa Swalaah au kwa uchache kukosa Swalaah kwa wakati.

6.      Mengine katika hizo kazi za unyoaji hupelekea vinyozi wengi kufanya matendo kinyume na urijali.

7.      Kubandikwa mapicha mbalimbali ndani ya saluni zao.

8.      Baadhi ya vinyozi kuweka wanawake wa kuwaosha wanaume nywele zao na hata wengine kuchuliwa (massage) na wanawake.

9.      Baadhi ya saluni vinyozi huwanyoa nywele wanawake.

10.  Baadhi ya watu wanaojinasibisha na uongozi wa dini wanachangia sana kudumisha mitihani hiyo kwa kuwakumbatia vinyozi wafanyao maasi na hata kuwashirikisha kwenye uongozi wa mambo ya dini

 

11. ​Mwisho tutahitimisha kwa maelekezo ya namna inavyopaswa kuwa saluni ya Muislamu anayechunga mipaka ya shariy’ah na kumcha Allaah.

 

Kinyozi wa Kiislamu anapaswa ajiepushe na yote hayo yaliyoelezwa katika vipengele hapo juu ili kuilinda Dini yake na heshima yake na vilevile kazi yake iwe ni halali na iwe yenye kipato cha halali na vilevile iwe ni kazi yenye kumridhisha Allaah (‘Azza wa Jalla).

Inasikitisha sana kupita kiasi, kuona vinyozi wengi wa Kiislamu hawana tofauti yoyote na vinyozi makafiri kwa namna wanavyofanya kazi zao na hata mionekano ya sehemu zao za kazi.

Unapokwenda au kupita maeneo ya kazi ya vinyozi wengi wa Kiislamu, huwezi kuona tofauti yoyote ile na maeneo ya kazi ya makafiri. Kuanzia unyoaji, utendaji mzima wa kazi hiyo, usengenyaji, umbea, upotezaji wakati, mapicha ya wasanii na waigizaji wa kikafiri, na mfumo mzima wa mazingira yaliyomo humo ndani.

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema katika Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

“Anayejifananisha na watu, basi ni miongoni mwao.” [Hadiyth hii iliyokusanywa na Abuu Daawuwd japo ina kauli tofauti, lakini ni Hadiyth Hasan kwa mujibu wa Imaam Ibn Hajr na vilevile Shaykh Al-Albaaniy, na ni Jayyid kwa mujibu wa Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah]

Maana ya “anayejifananisha na watu, basi atakuwa ni miongoni mwao” ni kuwa, atakuwa miongoni mwao kwa madhambi. Atashirikiana na hao anaojifananisha nao kwa madhambi.

Shaykh Al-Islaam ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) anasema:

“Hii Hadiyth inaonesha kwa dhahiri kuwa ni haramu kuwaiga watu (makafiri) na japokuwa udhahiri wake unaonesha kuwa anayewaiga, basi naye ni kafiri kama ambavyo Aayah inavyodhihirisha hilo:

“…Na yeyote atakayewafanya marafiki wao wandani; basi hakika yeye ni miongoni mwao...” [Al-Maaidah: 51]

[Mwisho wa kumnukuu Shaykh Al-Islaam katika kitabu chake Iqtidhwaau Swiraatw Al-Mustaqiym, uk, 83]

Aayah hiyo kwa ukamilifu inaeleza hivi:

“Enyi mlioamini! Msifanye Mayahudi na Manaswara marafiki wandani na ushirikiano. Wao kwa wao ni marafiki wandani. Na yeyote atakayewafanya marafiki wao wandani; basi hakika yeye ni miongoni mwao. Hakika Allaah Haongoi watu madhalimu.” [Al-Maaidah: 51]

Kadhaalika, makafiri hawatoridhika nawe hata uwaige utakavyowaiga. Anasema Allaah Aliyetukuka: 

"Na hawatoridhika nawe Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila zao. Sema: “Hakika mwongozo wa Allaah ndio mwongozo (pekee).” Na ukifuata hawaa zao baada ya yale ambayo yaliyokujia katika elimu, basi hutopata kutoka kwa Allaah mlinzi yeyote wala mwenye kunusuru." [Al-Baqarah: 120]

Inaendelea… Mambo ya Haramu yanayofanyika katika kazi ya Unyozi:

0 Comments