Jeshi la Myanmar lajitayarisha kuwashambulia Waislamu katika jimbo la Rakhine

Jeshi la Myanmar linajitayarisha kutekeleza oparesheni mpya dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine magharibi mwa nchi hiyo jambo ambalo limepelekea maelfu ya Waislamu kuanza kuhama eneo hilo.

Serikali ya Myanmar imethibitisha habari za mpango wa oparesheni hiyo katika jimbo hilo la Waislamu na kudai kuwa oparesheni hiyo ya kijeshi katika eneo la  Kyauktan jimboni Rakhine inalenga kukandamiza wanamgambo.

Waziri wa Usalama na Mipaka  katika jimbo la Rakhine Min Than amesema oparesheni hiyo itaendelea kwa muda wa wiki moja na kwamba kila atakayesalia katika eneo la oparesheni atatambuliwa kuwa mwanamgambo na kulengwa.

Kuanzia Oktoba 25 mwaka 2017, Jeshi la Myanmar likisaidiwa na Mabuddha wenye misimamo ya kufurutu ada, lilianzisha oparesheni ambayo ilipelekea zaidi ya Waislamu 6,000 kuuawa kwa umati na wengine zaidi ya milioni moja kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh.

Baada ya kupita takribani miaka mitatu tokea Jeshi la Myanmar lianzishe hujuma na mauaji dhidi ya Waislamu nchini humo katika jimbo la Rakhine, bado taasisi za kimataifa hasa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo hazijachukua hatua yoyote ya maana ya kuzuia mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Myanmar. Dunia inaendelea kunyamazia kimya jinai za Myanmar dhidi ya Waislamu. Ni wazi kuwa Waislamu wa Myanmar wasio na ulinzi wanaendelea kutendewa jinai za kivita na wanakabiliwa na mauaji ya kimbari mikononi mwa Jeshi la Myanmar na Mabuddha wenye misimamo mikali nchini humo kutokana na kimya cha jamii ya kimataifa.
Katika hatua ya hivi karibuni ya kuwakandamiza Waislamu, Jeshi la Myanmar linakusudia kutumia kisingizio cha kuwasaka wanamgambo kutekeleza mashambulizi makubwa dhidi ya Waislamu katika jimbo la Rakhine. Kufuatia kuenea ripoti za kukaribia oparesheni hiyo ya mauaji, wakaazi wa eneo hilo wameingiwa na hofu kubwa na maelfu ya Waislamu wameondoka katika makao yao na kutafuta hifadhi kwingineko ili kuokoa maisha yao wakati wa oparesheni hiyo ya kijeshi.

Pamoja na kuwa Umoja wa Mataifa umeshasema kuwa vitendo vya Jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu ni jinai za kivita lakini Baraza la Usalama la umoja huo, ambalo moja ya majukumu yake muhimu ni kulinda usalama na kudumisha amani duniani, halijachukua hatua yoyote ya kusitisha jinai za utawala wa Myanmar. 

Miezi michache iliyopita, kamati ya serikali ya Myanmar ilitangaza matokeo ya uchunguzi wake kuhusu mauaji ya Waislamu Warohingya na kusema baadhi ya wanajeshi wa Myanmar walitenda jinai lakini ripoti hiyo ilidai kuwa jeshi kwa ujumla halijatenda jinai ya kivita.

Anthony Kartaluchi, mtaalamu na mweledi wa jiopolitiki ya kisiasa anasema kuwa: Kile ambacho kinatajwa katika sheria za kimataifa kama 'mauaji ya kizazi' kinatokea katika mkoa wa Rakhine dhidi ya Waislamu Warohingya. Kundi ambalo linafanya mauaji ya kizazi dhidi ya jamii ya wachache ya Rohingya, limeweka suala la mauaji ya kizazi kama malengo yake ya awali.

Kamati huru ya Umoja wa Mataifa imefanya uchunguzu kuhusu yaliyojiri katika jimbo la Rakhine na kufikia natija kuwa, jeshi la nchi hiyo limetekeleza mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
Mbali na kuongezeka ukosefu wa usalama kwa Waislamu katika jimbo la Rakhine, waliokimbia jimbo hilo kwa kuhofia maisha yao na kufika katika mpaka wa Myanmar na Bangladesh wanakabiliwa na hali mbaya sana kwani hawana makazi, chakula, dawa wala huduma za afya.

Karibu wakimbizi milioni moja Waislamu Warohingya wanaishi katika makazi ya muda nchini Bangladesh na serikali ya nchi hiyo imesema haina uwezo wa kukidhi mahitaji yao na imeionya jamii ya kimataifa kuwa wanakabiliwa na maafa ya kibinadamu. Hata hivyo nchi za Magharibi zinazodai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu zimenyamaza kimya mbele ya mauaji ya kimbari na jinai za kivita ambazo zinatendwa dhidi ya Waislamu Warohingya nchini Myanmar.

Aidha madola ya Magharibi yamepuuza wito wa kutumwa misaada ya dharura ya kiafya na chakula kwa ajili ya wakimbizi Warohingya walioko nchini Bangladesh. Pamoja na kuwa  faili la jinai za kivita za Jeshi la Myanmar lilifikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai miezi sita iliyopita, lakini wahusika wakuu wa jinai hizo hawajakamatwa.

Matarajio ya waliowengi duniani ni kuwa taasisi za kimataifa, hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai  zitachukua hatua za kivitendo kuhusu faili la mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Myanmar na kusitisha jinai hiyo sambamba na kuwafikisha kizimbani wahusika.

0 Comments