000-Majina Ya Allaah Na Sifa Zake: Utangulizi

Majina Ya Allaah Na Sifa Zake

 

000-Utangulizi

 

بِسْمِ الله الرَّحْمنِ الرَّحِيم

الْحمْدُ لِلَّه وَالصَّلاةُ وَالسِّلامُ عَلى خَاتم الأنْبِيَاء وَالْمُرْسَلِين، الْمَبْعُوثُ رَحْمَةً لِلْعَالَمِين، مُحَمَّد وَعَلى آلِه وَأصْحابِه أجْمَعِين وَمَنْ تَبِعَهُمْ بِإِحْسَانٍ إِلَى يَوْمِ الدِّينِ.

 

Himdi zote Anastahiki Allaah, Swalaah na Salaam ziwe juu ya Nabiy na Rasuli wa mwisho, aliyetumwa awe rahmah kwa walimwengu, Muhammad, pamoja na ahli zake na Maswahaba zake wote, na wanaowafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Malipo.

 

Al-Asmaaul-Husnaa imetajwa mara nne katika Qur-aan katika kauli zifuatazo za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

قُلِ ادْعُوا اللَّـهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَـٰنَ ۖ أَيًّا مَّا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ

Sema; “Muiteni Allaah au muiteni Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah). Vyovyote mtakavyomwita basi Yeye Ana Majina Mazuri kabisa. [Al-Israa 17: 110]

 

Na pia:

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ﴿٨﴾

Allaah, hapana ilaaha (muabudiwa wa haki) ila Yeye. Anayo Majina Mazuri kabisa.[Twaahaa 20: 7-8]

Na:

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٨٠﴾

Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanaopotoa katika Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-A’raaf 7: 180]

 

Na pia:

هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ ۖ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ يُسَبِّحُ لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٢٤﴾

Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji, Mwanzishi viumbe bila kasoro, Muundaji sura na umbile, Ana Majina Mazuri kabisa, kinamsabbih Pekee viliyoko katika mbingu na ardhi, Naye Ndiye Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.  [Al-Hashr (59:22-24)]

 

Kumpwekesha Allaah Katika Majina Yake Na Kuthibitisha Sifa Za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

‘Aqiydah ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah kuhusiana na Majina Mazuri kabisa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Sifa Zake ni tawqifiyyah; yanathibitishwa Aliyoyathibitisha Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika Qur-aan na Sunnah  bila ya  ta'twiyl (kuzipinga, kukanusha uwezekano), wala  tamthiyl (kumithilisha; kulinganisha) wala takyiyf (kuainisha maana na kuziulizia namna yake au kuuliza ni vipi Sifa hiyo ipo, kuchunguza ni kwa “namna gani” zimefungamana au kuambatana na Allaah) wala tahriyf (kubadilisha maana, kupotosha Sifa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kutoa maana isiyo sahihi). Allaah Anaposema kuwa Ana Qudra (uwezo), na sisi tunaamini kuwa Anao Uwezo. Anaposema Yeye ni Qawiyy (Mwenye nguvu), na sisi tunaamini kuwa Ana nguvu. Anaposema kuwa Anaona, na sisi tunaamini kuwa Anaona. Anaposema kuwa Anasikia, na sisi tunaamini kuwa Anasikia. Lakini kuona Kwake au kusikia Kwake si kama kuona au kusikia kwa kiumbe chochote kile! Na Anaposema kuwa Anayo Macho, na sisi tunaamini kuwa Anayo Macho. Na Anaposema kuwa Anayo Mikono na sisi tunaamini kuwa Anayo Mikono, na Anaposema kuwa Anao Wajihi, na sisi tunaamini kuwa Anao Wajihi. Lakini Uwezo Wake, au Nguvu Zake, au Macho Yake au Masikio Yake au Wajihi Wake, hakuna mfano wowote na kitu chochote wala kiumbe chochote kile kama Anavyosema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١١﴾

Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa 42: 11]

 

Kwa hiyo Anapotujulisha kuwa Yeye ni Al-‘Aliym (Mjuzi wa yote daima), hatuwezi kusema hivyo kwa bin Aadam. Na kadhalika hatuwezi pia kufananisha Sifa Zake nyinginezo kwa kiumbe chochote kile. Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٧٤﴾

Basi msimpigie mifano Allaah! Hakika Allaah Anajua nanyi hamjui. [An-Nahl 16: 74]

 

Kutokuzithibitisha sifa ambazo Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amejipa ni kuzigeuza na kuzipotoa; Anaonya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa): 

 

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٨٠﴾

Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanaopotoa katika Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-A’raaf 7: 180]

 

Hiyo ndiyo ‘Aqiydah sahihi kabisa waliyoitakidi Salaf wa ummah na ndivyo ipasavyo kuzikubali Sifa zote za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) bila ya kukisia kwa akili zetu namna yake au mfano wake, wala kuogopa kuzithibitisha zilivyo kwa kukhofia kufananisha na viumbe. Kuzithibitisha vile vile zilivyokuja kutoka katika Kitabu Chake kama Alivyoziita Mwenyewe (‘Azza wa Jalla) na Alivyotaka Yeye, hiyo ndio salama kwetu. Tujisalimishe na Alivyojithibitishia Mwenyewe na alivyothibitisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwani akili zetu haziwezi kufikia upeo wa utambuzi na ujuzi wa Sifa Zake (‘Azza wa Jalla).

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾

Na wala usiyafuate (kusema au kushuhudia) yale usiyokuwa nayo elimu. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitakuwa vya kuulizwa (Siku ya Qiyaamah). [Al-Israa 17:36]

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا ﴿١١٠﴾

Anajua yale yaliyoko mbele yao, na yale yaliyoko nyuma yao, na wala hawawezi kuzunguka elimu Yake. [Twaahaa 20: 110]

 

Umuhimu wa kuyajua na kujifunza Majina Mazuri kabisa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Sifa Zake:

 

1-’Ilmu kuhusu Majina ya Allaah na Sifa Zake ni kumtambua Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kutambua Utukufu Wake.

 

Unapotaka kutaamali na mtu, hakuna shaka kuwa utataka kujua jina lake, kun-yah yake na kuulizia khabari zake upate ufahamu bayana kumhusu yeye hata uridhike unapotaamali naye. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametuumba na Ndiye Anayeturuzuku kila kitu na tunakhofia ghadhabu Zake na tunataraji rahmah Zake Atughufurie madhambi yetu Asituadhibu. Kwa hiyo, hakuna budi kutambua yanayomridhia ili Naye Aridhike na sisi, na pia kutambua yanayomghadhibisha ili tujiepushe nayo. Kama vile ambavyo huwezi kumpenda usiyemjua, hali kadhaalika huwezi kumkhofu na kumpenda Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa haki apasayo kukhofiwa na kupendwa isipokuwa kwa kumtambua Utukufu Wake, na njia mojawapo ni kutambua Majina Yake Mazuri kabisa na Sifa Zake. Usipomtambua ukampenda, Naye Hatokutambua wala kukujali.

Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ نَسُوا اللَّـهَ فَأَنسَاهُمْ أَنفُسَهُمْ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ﴿١٩﴾

Na wala msiwe kama wale waliomsahau Allaah, Naye (Allaah) Akawasahaulisha nafsi zao, hao ndio mafasiki. [Al-Hashr 59: 19]

 

Hivyo, kumtambua Allaah kunapelekea katika kumpenda, na kumkhofu, na kutawakali Kwake, na kumsafishia niyyah (ikhlaasw) katika matendo na kutaraji rahmah Yake.

 

2-’Ilmu Ya Majina ya Allaah na Sifa Zake ni ’Ilmu ya asasi.

 

’Ilmu kuhusu Majina ya Allaah na Sifa Zake ni’ilmu ya asasi, kwani ni aina ya tatu ya Tawhiyd. Na tawhiyd ndio jambo kuu walilokuja nalo Rusuli wote katika ulinganiaji wao. Na ni ’ilmu bora na tukufu kabisa kuitambua. Na ndio lengo kuu na kuumbwa kwa kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika ’ibaadah. 

 

3-’Ilmu ya Majina ya Allaah na Sifa Zake Inazidisha Iymaan.

 

 ’Ilmu kuhusu Majina ya Allaah na Sifa Zake ni sababu ya kuzidisha iymaan kama alivyosema Imaam As-Sa’dy (Rahimahu Allaah): “Hakika kuamini Asmaa Allaah Al-Husnaa na utambuzi wake, inajumuisha aina tatu za tawhiyd; Tawhiyd Ar-Rubuwbiyyah, Tawhiyd Al-’Uluwhiyyah (’Ibaadah) na Tawhiyd Asmaa wasw-Swifaat. Na aina hizi ndio roho ya iymaan na ndio furaha halisi na kitulizo cha dhiki za moyo, na ndio asili yake na lengo lake. Basi kila mja anapozidi kutambua maarifa ya Asmaa Allaah na Sifa Zake ndipo inapozidi iymaan yake na kuthibitika yakini yake. [At-Tawdhiwyh Wal-Bayaan Lishajaratil-Iymaan Lis-Sa’dy, uk. 41]

 

4-’Ilmu kuhusu Majina ya Allaah na Sifa Zake ni sababu ya kupata Jannah:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِنَّ لِلَّهِ تِسْعَةً وَتِسْعِينَ اسْمًا مِائَةً إِلا وَاحِدًا مَنْ أَحْصَاهَا دَخَلَ الْجَنَّةَ))

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ’anhu) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Ana Majina tisini na tisa, atakayejifunza moyoni ataingia Jannah.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

Ahswaahaa imekusudiwa: Kuyafahamu maana Zake, kuyahifadhi, kufanyia kazi, kuomba du’aa kuyatumia kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ

Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. [Al-A’raaf 7: 180]

 

Imaam Ibn ’Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema: Ahswaahaa haimaanishi kuwa ni kuyaandika Majina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwenye karatasi na kuyakariri mpaka mtu aweze kuyahifadhi bali inamaanisha:

  • Kujifunza kuyatamka.
  • Kufahamu maana Zake.
  • Kumwabudu Allaah kwayo, kwa njia mbili:

Kwanza:  Kumuomba du’aa kwayo kwa sababu Allaah Anasema:

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ

Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. [Al-A’raaf 7: 180]

Kwa hivyo, uyafanye kuwa ni wasiylah (kurubisho) ya du’aa yako, hivyo utachagua Jina linalowafikiana na haja yako. Unapotaka  kuomba maghfirah useme: ”Yaa Ghafuwru nighufurie.” Na si kusema: ”Yaa Shadiyd Al-’Iqaab Ighfir-liy (Ee Mkali wa kuakibu nighufurie!)” kwani hii inakuwa kama ni istihzaa. Linalopasa (ikiwa utamwita Allaah hivyo) useme ”Ee Mkali wa kuakibu, Niepushe na ikabu Yako.”

 

Pili:  Katika ’ibaadah zako, vitendo viashirie  Majina Yake. Kama Ar-Rahiym (Mwenye kurehemu) kusudio lake ni rahmah, basi fanya vitendo vyema vitakavyosababisha kupata rahmah ya Allaah. 

 

Hiyo ndio maana ya ahswaahaa. Basi itakapotekelezwa hayo ndipo itakapostahiki kuingizwa Jannah.” [Majmuw’ Fataawa wa Rasaail Ibn ’Uthaymiyn (1/74)]

’Ulamaa wamekubaliana kwamba Majina ya Allaah si tisini na tisa pekee bali yako zaidi ya hayo kwa dalili ya Hadiyth:

 

عن عَبْدِ اللَّهِ بن مسعود قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَا أَصَابَ أَحَدًا قَطُّ هَمٌّ وَلا حَزَنٌ فَقَالَ: اللَّهُمَّ إِنِّي عَبْدُكَ، وَابْنُ عَبْدِكَ، وَابْنُ أَمَتِكَ، نَاصِيَتِي بِيَدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤُكَ، أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ سَمَّيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحَدًا مِنْ خَلْقِكَ، أَوْ أَنْزَلْتَهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ اسْتَأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الْغَيْبِ عِنْدَكَ، أَنْ تَجْعَلَ الْقُرْآنَ رَبِيعَ قَلْبِي، وَنُورَ صَدْرِي، وَجَلَاءَ حُزْنِي، وَذَهَابَ هَمِّي، إِلا أَذْهَبَ اللَّهُ هَمَّهُ وَحُزْنَهُ وَأَبْدَلَهُ مَكَانَهُ فَرَجًا)) فَقِيلَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَلا نَتَعَلَّمُهَا؟ فَقَالَ: ((بَلَى يَنْبَغِي لِمَنْ سَمِعَهَا أَنْ يَتَعَلَّمَهَا)) صححه الألباني في السلسلة الصحيحة (199)

Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote atakayefikiwa na dhiki na huzuni kisha akasema:

 

Allaahumma inniy ‘abduka, ibnu-‘abdika, ibnu-amatika, naaswiyatiy Biyadika, maadhwin fiyya hukmuka, ‘adlun fiyya qadhwaauka, as-aluka bikullismin huwa Laka, sammayta bihi Nafsaka aw Anzaltahu fiy Kitaabika, aw ‘Allamtahu ahadan min Khalqika, awis-staa-tharta bihi fiy ‘ilmil-ghaybi  ‘In-daka, an Taj-’alal-Qur-aana rabiy’a qalbiy, wanuwra swadriy, wajalaa-a huzniy, wa dhahaaba hammiy.

 

Ee Allaah hakika mimi ni mtumwa Wako, mtoto wa mtumwa Wako, mtoto wa kijakazi Chako, utosi wangu uko Mikononi Mwako, yaliyopita kwangu yako katika hukumu Yako, ni usawa kwangu kunihukumu Kwako, nakuomba kwa kila Jina ambalo ni Lako Ulilojiita  Mwenyewe au Uliloliteremsha katika Kitabu Chako, au Ulilomfundisha yeyote yule kati ya viumbe Vyako, au Ulilolihifadhi Wewe mwenyewe (na kujihusisha kulijua) katika ’ilmu ya ghayb Kwako, nakuomba Ujaalie Qur-aan kuwa ni rabiy' (uhuisho, raha, furaha na ustawisho) wa moyo wangu na nuru ya kifua changu, na ufumbuzi wa  huzuni yangu, na sababu ya kuondoka wahka wangu. - Akisema hivyo hakuna isipokuwa Allaah Atamuondoshea dhiki na huzuni na Atambadilisha badala yake faraja.” Ikasemwa: Ee Rasuli wa Allaah! Je tujifunze? Akasema: ”Ndio, inampasa kwa mwenye kuisikia kujifunza.” [Ameipokea Ahmad (1/391) [452], Al-Haakim (1/509) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (199) na Al-Kalimi Atw-Twayyib (124)]

 

Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

 

“Hii (du’aa katika Hadiyth hiyo) ni dalili kwamba Allaah Ana Majina zaidi ya tisini na tisa.” [Majmu’w Al-Fataawa (6/374)]

 

Na Imaam Ibn ’Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema alipoulizwa kuhusu idadi ya Majina ya Allaah:

“Majina ya Allaah hayana idadi maalumu. Na dalili ni kauli ya (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

((Ee Allaah hakika mimi ni mtumwa Wako, mtoto wa mtumwa Wako, mtoto wa kijakazi Chako, utosi wangu uko Mikononi Mwako, yaliyopita kwangu yako katika hukumu Yako, ni usawa kwangu kunihukumu Kwako, nakuomba kwa kila Jina ambalo ni Lako Ulilojiita Kwako Mwenyewe au Uliloliteremsha katika Kitabu Chako, au Ulilomfundisha yeyote yule kati ya viumbe Vyako, au Ulilolihifadhi Wewe mwenyewe (na kujihusisha kulijua) katika ’ilmu ya ghayb Kwako)).

 

Basi ambayo Aliyoyahifadhi Allaah katika ’ilmu ya ghayb hayawezi kujulikana, na ambayo hayajulikani hayawezi kuhesabika. Ama kauli ya (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

”Hakika Allaah Ana Majina tisini na tisa, atakayejifunza moyoni ataingia Jannah.”

 

Haimaanishi kuwa Hana isipokuwa Majina haya tu. Lakini inayokusudiwa ni kwamba atakayehifadhi Majina haya tisini na tisa basi ataingia Jannah. Kauli yake: Man Ahswaahaa (atakayejifunza kwa moyo) ni kamilisho la sentensi ya mwanzo na si kiendelezo kilichojitenga, ni kama vile Waarabu wanaposema: “Nina farasi mia ambao nimewaandaa kwa jihaad kwa ajili ya Allaah”; Hii haimaanishi kwamba msemaji ana farasi mia tu bali hawa mia ndio aliowaandaa kwa ajili ya jambo hili.” [Majmuw’ Fataawa Ibn ‘Uthaymiyn (1/122)]

 

Kazi hii ya ku-tarjam na kuelezea Majina ya Allaah na Sifa Zake tuliyoyakusanya humu hakika ni mukhtasari tu kwa sababu ’ilmu yake ni pana mno haiwezekani kuijumuisha kwa makala fupi kama hizi. Lakini tunatumai kuwa mukhtasari huu utatoa maarifa ya kumtoshelezea kiasi msomaji kutambua maana za msingi za Majina ya Allaah na Sifa Zake.

 

Haya ndio Ambayo Allaah Ametuwezesha kwa tawfiyq Yake, huku tukimuomba Ajaalie kazi hii iwe yenye ikhlaasw Kwake na ilete manufaa kwa jamii na Atutakabalie. Aamiyn.

 

0 Comments