Adhabu Ya Kaburi

Imekusanywa Kutoka Katika Duruws Za Imaam Muhammad Bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)

 

 

Anasema Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu):

 

‘Zipo dalili nyingi sahihi zinazoelezea juu ya Adhabu ya kaburini. Allaah Anasema:

“Adhabu ya Motoni wanadhihirishiwa (makaburini mwao) asubuhi na jioni. Na siku ile kitakapotokea Qiyaamah (kutasemwa) “Waingizeni watu wa Fir’awn katka adhabu kali zaidi.”Al-Muumin (Ghaafir - 46)

 

Hii ni dalili katika Qur-aan kuwa Fir’awn na watu wake wanadhihirishiwa adhabu asubuhi na jioni kabla ya Siku ya Qiyaamah. Kwa sababu Aayah inaendelea kusema : ‘Na siku ile kitakapotokea Qiyaamah ‘na maana yake ni kuwa hiyo adhabu iliyotajwa ya kudhihirishiwa Moto asubuhi na jioni ilikuwepo kabla ya Siku ya Qiyaamah.’

 

[Soma pia : Utapokea Kitabu Chako Kwa Mkono Gani?]


Na katika Hadiyth nyingi sahihi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

‘Muombeni Allaah akukingeni na adhabu ya Moto.’ Wakasema: ‘Tunajikinga kwa Allaah na adhabu ya Moto.’ Akasema: ‘Muombeni Allaah Akukingeni na adhabu ya Kaburi.’ Wakasema: ‘Tunajikinga kwa Allaah kutokana na adhabu ya Kaburini.’ [Muslim]

 

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alisema juu ya Muislamu :

‘Anapanuliwa kaburini mwake kiasi cha upeo wa macho yake.’ [Al-Bukhaariy]

 

Dalili kama hizi ziko nyingi sana, na haijuzu mtu kuzikanusha kwa ajili ya matamanio ya nafsi yake.

 

Adhabu ya kaburini ni ya kiroho na si jambo linalohusu mwili, na hii ndiyo sababu ikawa imani juu yake ni katika mambo ya ghaibu. Na hali ya mambo katika maisha ya Barzakh hayawezi kukisiwa kwa hali ya maisha yetu ya hapa duniani.

 

Isitoshe, adhabu ya Kaburini na neema zake anayadiriki maiti peke yake na wanaadamu wengine hawawezi kuyaona wala kuhisi au kuyadiriki. Mfano wake ni sawa na mfano wa mtu anapoota usingizini. Anaota kuwa anakwenda anarudi, anapigwa anapiga. Anajiona yupo mahali penye nafasi kubwa na mara nyingine anajiona yupo penye nafasi ndogo iliyodhikika. Anayaona yote wakati walio karibu yake hawayaoni wala hawayahisi.’

(Mwisho wa maneno ya Imaam Ibn Uthaymiyn)

 

[Soma pia :  Jazaa Ya Waja Wema Na Neema Za Jannah ]


Kama ilivyoeleza Aayah ya adhabu wanayopata Fir’awn na watu wake hadi siku ya Qiyaamah, pia zipo aya nyingi zinazoelezea juu ya neema wanayopata Waumini na pia juu ya adhabu wanayopata makafiri wanapotolewa roho zao, na baada ya kutolewa roho zao.

 

Allaah Anasema:

‘Na laiti ungeliona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakiwapiga nyuso zao na migongo yao na kuwaambia; Ingojeni adhabu ya moto.

Hayo ni kwa sababu ya (maasi) yake yaliyofanya na mikono yenu. Na hakika Allaah si mwenye kuwadhulunu waja (Wake)’ Al-Anfaal: 50-51

 

Na Akasema juu ya Mashuhadaa:

‘Wala usiwadhani wale waliouawa katika njia ya Allaah kuwa ni wafu (maiti) bali wahai wanaruzukiwa kwa Mola wao.

Wanafurahia Aliyowapa Allaah kwa fadhila Zake na wanawashangilia wale ambao hawajajiunga nao, walio nyuma yao ya kwamba haitokuwa khofu juu yao wala hawatohuzunika.’ Aal-‘Imraan: 169-170

 

 

Aayah kama hizi za kuadhibishwa makafiri pale wanapotolewa roho zao na baada yake, pamoja na neema wanazopata Waislamu wanapotolewa roho zao na baada yake pamoja na Adhabu wanayopata Fir’awn na watu wake ni nyingi sana, jambo linalotufanya tusiweze kukanusha juu ya adhabu ya kaburini zilizotajwa wazi wazi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhio wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth zake nyingi sahihi.

0 Comments