Baba wa mtuhumiwa wa ugaidi afariki

Hajapata kuonana na mwanae tangu akamatwe
Yupo gerezani mwaka wa sita sasa

Bakari Mwakangwale

MTUHUMIWA wa kesi za ugaidi, Said Omar Said, amefiwa na baba yake mzazi akiwa gerezani huku kesi yake ikiwa bado haijaanza kusikilizwa kutokana na upelelezi kutokamilika kwa mwaka wa sita sasa.

Baba wa mtuhumiwa Said, aliyetajwa kwa majina ya Mzee Omar Said Omar, aliyemkazi wa Zanzibar, amefariki Juni 20, 2020 na kuzikwa Juni 21, 2020, katika makaburi ya Basra, Visiwani Zanzibar, baada ya kuugua shinikizo la damu kwa muda mrefu.

Marehemu Mzee Omar, hakupata kuonana na mwanae kwa miaka sita tokea akamatwe Visiwani Zanzibar na kuwekwa Gerezani Jijini Dar es Salaam, na kujumuishwa katika kundi la Masheikh Farid Had na Msellem Ally, na kupewa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kigaidi.

Akiongea kwa njia ya simu  kutoka Zanzibar mapema wiki hii, mtoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa majina ya Almasi Omari Said, amesema Mzee Omari, amefariki kwa ugonjwa wa Presha.

Bw. Almasi alisema Mzee Omari, amesumbuliwa na ugonjwa huo kwa muda mrefu na kusababisha kupooza mkono na mguu, na kipindi hiki cha mwisho ilimpelekea kushindwa hata kuongea.
“Tokea amepatwa na maradhi hayo, huu ni mwaka wa nane sasa, hata hivyo hali hiyo ilikuwa inamjia kisha anapata tiba na kupata nafuu kisha baada ya muda humrudia tena ndio ilikuwa sehemu ya maisha yake.”

“Mwanae Said Omar, tangu akamatwe sasa ni mwaka wa sita yupo gerezani na kesi yake haijaanza kusikilizwa, si baba wala mama na hata mimi hatupata kumtia machoni tokea wakati huo na hana taarifa kama baba yake amefariki. Amesema Bw. Alamasi.

Akifafanua alisema, Mzee Omari, alianza kuungua ugonjwa huo kabla mwanae hajakamatwa na alikuwa  msaada kwa Mzee wake akishirikiana na yeye mdogo wake (Bw. Alamasi), hivyo kukamatwa kwake kuliacha pengo kubwa la huduma kwa mzee wao na familia kwa ujumla.

Alisema, kaka Saidi, alikamatwa  akiwa Zanzibar, na awali alipelekwa katika gereza la Segerea Jijini Dar es Salaam, lakini baadae waliambiwa kuwa amehamishiwa katika gereza la Jijini Arusha.
Hata hivyo Bw. Almasi, alisema wao kama familia hawajawahi kwenda gerezani kumuona tokea akamatwe akiwa Jijini Dar es Salaam wala Arusha, akasema hali hiyo imesababishwa na hali ya ugonjwa wa baba yao aliyepooza na alikuwa wa kusaidiwa kila kitu na mama nae afya yake si nzuri tokea apate taarifa za kukamatwa kwa mwanae.

“Baada ya kaka kukamatwa Mama alipata mshutuko kwa muda wa wiki mbili alishindwa kula chakula zaidi ya kunywa maji na uji na kuanzia hapo afya yake na yeye mpaka sasa sio nzuri kwa maana hiyo nikawa na wagonjwa wawili. Amesema Bw. Almasi.

Aidha, Bw. Alamsi, alisema pamoja na kutokwenda kumuona wamekuwa wakipata taarifa za ndugu yao kupitia kwa familia ya Sheikh Farid Had, ambao wao huenda mara kwa mara, kuwatembelea na wakirudi lazima wafike nyumbani kwao kuwapa salam na maendeleo yake. 
Ustadhi Said Omari, alikamatwa Visiwani Zanzibar, miaka sita iliyopita na kujumuishwa na kina Sheikh Faridi Had, katika kesi ya tuhuma za Ugaidi.

 Ustadh Said alikuwa dereva wa kina Sheikh Farid, katika shughuli zao kabla ya kukamatwa kwao.


0 Comments