Chukua katika mali yake kiasi cha kukutosha


Kutoka kwa mama wa Waumini, Aisha (Allah amridhie) amesimulia kuwa Hindu bint Utba, mke wa Abu Sufian (Allah amridhie) aliingia nyumbani kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akasema: “Ewe Mjumbe wa Allah! Hakika Abu Sufian ni mtu bahili, hanipi matumizi (yanayonitosha) mimi pamoja na watoto wangu. Hivi nitakuwa na kosa nikichukua sehemu ya mali yake bila ya idhini yake?” Mtume akamwambia: “Chukua katika mali yake kiasi cha kukutosha wewe na watoto wako kwa uangalifu.” [Bukhari na Muslim].

Mafunzo ya tukio

Ndoa ni jambo kubwa katika maisha ya binadamu, ni jambo linaloambatana na haki na wajibu wa wanandoa (mume na mke). Ndoa iliyojengwa katika msingi wa kutambua wajibu na haki, yaani mume na mke kutekeleza majukumu yao ya ndoa kikamilifu ina nafasi kubwa ya kudumu.

Kinyume chake, ndoa ambayo haikujengwa juu ya msingi wa kutekeleza majukumu muhimu ya ndoa husheheni magomvi, mizozo, chuki, visasi na kutoaminiana.

Tukio hili linatuonesha namna udhaifu katika kutekeleza majukumu ya ndoa unavyoweza kusababisha migongano na migogoro inayoajitokeza mara kwa mara katika ndoa.

Ukweli ni kwamba, wanawake ndiyo ambao hukumbana na changamoto nyingi za kimaisha pindi waume zao wanaposhindwa kutekeleza wajibu wao na hivyo kujikuta wakitekeleza majukumu yasiyokuwa yao. Ni wajibu kwa wanaume kutambua majukumu yao na kuyasimamia ipasavyo.

Haki na wajibu wa mke kwa mumewe

Kama ilivyotangulia kuelezwa hapo awali, mke ana haki mbalimbali kisharia anazostahili kuzipata kutoka wa mumewe. Baadhi ya haki hizo zimefungamana na mali kama tutakavyoona katika maelezo ya hapo chini.

Kwanza: Mahari

Mahari ni kiwango maalumu cha mali kinachobainishwa na kutolewa na mwanamume kwa makubaliano kuwa ni sadaka ya mwanamke katika ndoa. Allah anasema:

“Na wapeni wanawake mahari zao kwa maridhawa. Lakini wakitoa chochote wenyewe katika mahari yao kwa hiyari zao, basi kuleni kwa kufurahia na kunufaika.” [Qur’an, 4:4].

Mahari siyo sharti wala nguzo katika ndoa bali ni haki ya mke ambayo mwanamume analazimika kuitoa. Haki hii inadhihirisha ukubwa na heshima ya mkataba wa ndoa na pia ni takrima kwa mwanamke kutokana na kuridhia kwake kuolewa.

Pili: Matumizi

Kama tulivyoona katika tukio hili, mke wa Abu Sufian alimuendea Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kumlalamikia kuhusu kitendo cha mumewe (Abu Sufian) cha kutoacha matumizi ya nyumbani. Changamoto iliyokuwa inamkabili mke wa Abu Sufian inawakabili wanawake wengi katika zama zetu hizi.

Ni ukweli usio na chembe ya shaka kwamba wanawake wengi siku hizi wanalazimika kufanya kazi za vibarua ili waweze kuhudumia familia zao, jukumu ambalo lilipaswa kufanywa na waume zao. Allah amewawajibisha wanaume kuhudumia familia zao kwa kusema:

“Na juu ya baba yake chakula cha akina mama, na nguo zao kwa mujibu wa ada. Wala halazimishwi mtu ila kwa kadri ya uwezo wake.” [Qur’an, 2:233].

Mume anapaswa kumpatia mkewe na watoto wake mahitaji yote ya msingi yakiwamo mavazi, chakula na malazi kadri Allah atakavyomuwezesha. Katika Hijja yake ya mwisho, Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie) aliwausia Waislamu kwa kusema:

“Enyi watu !Ni kweli mna haki juu ya wanawake na wao pia wana haki juu yenu. Kumbukeni mmewachukua kuwafanya wake zenu kwa amana ya Allah Ta’ala na mmehalalishiwa (kustarehe) nao kwa neno lake (Allah). Nakuusieni kuwatendea wema wanawake (kwa kuwalisha na kuwavisha kadiri muwezavyo) na muwahurumie kwani wao ni wake zenu na wasaidizi wenu.” [Muslim].

Tatu: Makazi

Ni wajibu mume kumpatia mkewe makazi (nyumba) mazuri yatakayomhifadhi na kutunza heshima yake. Qur’an inatuambia: “Wawekeni humo humo mnamokaa nyinyi kwa kadiri ya pato lenu wala msiwaletee madhara kwa kuwadhiki.” [Qur’an, 65:6]. Mwanamke anapaswa kupewa makazi bora yenye amani na utulivu ili aweze kushirikiana na mumewe katika kuwalea watoto katika misingi ya imani na maadili ya dini.

Haki zisizofungamana na mali

Mosi: Uadilifu

Ni wajibu wa mume mwenye mke zaidi ya mmoja kufanya uadilifu baina ya wake zake katika mambo au vitu muhimu kama vile chakula, malazi na kugawa siku za kulala baina ya wake zake.

Kutofanya uadilifu baina ya wake ni katika madhambi makubwa mbele ya Allah Aliyetukuka. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Mwenye wake wawili na akaelemea kwa mmoja wao, atakuja Siku ya Kiyama huku ubavu wake mmoja ukiwa umelemaa.” [Abu Daud na Tirmidhy].

Ama kufanya uadilifu katika dhati ya moyo hilo siyo wajibu kwa sababu hakuna anayeliweza. Na haya ndiyo makusudio ya kauli yake Allah Mtukufu isemayo:

“Na hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wake hata mkifanya bidii.” [Qur’an, 4:129].

Pili: Kuishi nao kwa wema

Utulivu, mapenzi na maelewano baina ya wanandoa (mume na mke) ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya ndoa. Allah anasema:

“…na kaeni nao (wanawake) kwa wema; na kama mkiwachukia basi (msiwaache) kwani huenda mkakichukia kitu ambacho Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake.” [Qur’an, 4:19].

0 Comments