Kesi Masheikh wa Uamsho Kiza Kinene

Kesi Masheikh wa Uamsho:

‘Kiza cha haki’ chazidi kutanda

Na Bakari Mwakangwale

WAISLAMU wamepigwa na butwaa kufuatia maamuzi ya Mahakama Kuu Jijini Dar es Salaam, kutengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, iliyoruhusu watu na vyombo vya habari kusikiliza na kuripoti kesi hiyo.

Hali hiyo imefuatia taarifa kuwa Mahakama hiyo, iliyo sikiliza shauri hilo imetoa amri hiyo kwamba imetengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, iliyofuta uamuzi wake wa mwazo katika maeneo hayo.

Akiongea na Mwandishi wa Habari hizi, Wakili wa upande wa utetezi, Wakili Juma Nassoro, alisema Serikali, iliomba Mahakama Kuu kutengua amri ya Mahakama ya Kisutu, iliyoruhusu Wanahabari na wananchi kuhudhuria Mahakamani, sasa Mahakama imekubali ombi la upande wa mashtaka kwa kuzuia yote hayo.

“Maamuzi ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Leyla, ilipo sikiliza hilo shauri ndio imetoa hiyo amri kwamba imetengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, iliyofuta uamuzi wake wa mwazo wa kuruhusu watu kuingia Mahakamani na vyombo vya habari kuripoti mwenendo wa kesi hiyo, kwa hoja kwamba Mahakama ya Kisutu haikuwa na mamlaka hayo.” Amesema Wakili Nassoro.

Akifafanua kadhia hiyo kwa ujumla Wakili Nassoro, alisema mwaka 2015, Mahakama ya Kisutu ilitoa zuio kwamba watu wasiingie Mahakamani kusikiliza kesi hiyo  na wala vyombo vya habari visiripoti mwenendo wa kesi hiyo.

Hata hivyo Wakili Nassoro, alisema baada ya muda mwingi kupita upande wa utetezi waliiomba Mahakama ya Kisutu, pamoja na kufuta amri ya kuzuia watu na wanahabari lakini pia waliomba upelelezi kuharakishwa.

“Tuliiomba Mahakama itoe amri kwa upande wa Serikali, ikamilishe upelelezi kwa mujibu wa sheria ili kesi ya msingi ianze kusikilizwa na pia ifute ile amri yake ya zuio la Wanahabari kuripoti mwenendo wa kesi hiyo na Wananchi kuhudhuria kusikiliza kesi hiyo kwa sababu hiyo amri inatumika vibaya.” Amesema Wakili Nassoro.

Wakili Nassoro, alisema Mahakama ya Kisutu, ilikubali ombi lao, ikasema inatengua amri yake ya mwaka 2015, ya kuzuia watu kuingia kusikiliza kesi hiyo na Vyombo vya habari viripoti mwenendo wa kesi hiyo na kuitaka Serikali kukamilisha upelelezi wake haraka.

Alisema, hatua ya kukubaliwa kwa ombi la upande wa utetezi, wao upande wa Mashtaka (Serikali) haukuridhika na hivyo kuamua kukata rufaa Mahakama Kuu kuipinga Mahakama ya Kisutu.

“Sasa tumepokea maamuzi ya Mahakama Kuu, baada ya kusikiliza shauri hilo imetengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, iliyofuta uamuzi wake wa awali hivyo hali imerudi palepale amri ya Juni 18, 2015, imerudishwa na amri ya Septemba 5, 2019, imefutwa.” Amesema Wakili Nassoro.

Mwaka 2015, Masheikh Farid Had na Mselem Ally na wenzao walifikishwa Mahakama ya Kisutu na kufunguliwa mashtaka ya kujihusisha ya kuhifadhi magaidi.

Tokea mwaka huo mpaka sasa, kesi yao imeendelea kutajwa tu kwa madai kuwa upelelezi haujakamilika huku zuio la wanahabari na wananchi kufika Mahakamani likiwa limerudishwa.


chanzo : Annur newspaper

0 Comments