Kisa Cha Mtoto Aliyekuwa Akiswali Jamaa'ah Msikitini

BismiLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa ba’ad:

Kisa hichi cha kweli ni kuhusu mtoto mdogo aliyekuwa katika darasa la pili (tunampa jina la ‘Abdullaah) ambaye mama yake alifanya jitihada kubwa kumlea malezi ya dini ainukie katika Ridhaa ya Allaah (Subhaanah wa Ta'aala). Alimfundisha umuhimu wa Swalah tano na khaswa umuhimu wa kuswali Swalah ya Alfajiri msikitini. Mtoto alikuwa na juhudi ya kwenda msikitini ingawa baba yake hakuwa akifanya hivyo, bali alikuwa akilala wakati mtoto huyo akienda kuswali Swalah ya Jamaa msikitini.

Siku moja wakati yuko darasani, mwalimu aliamua kutoa adhabu ya kuwachapa wanafunzi wote darasani kwa sababu fulani. Akaanza kuwachapa wanafunzi mmoja mmoja hadi alipomfikia ‘Abdullaah. Mwalimu akamuambia ‘Abdullaah afungue mikono yake ili amchape kwa rula (mstari wa mita).

 

Mjadala ulikuwa kama ifuatavyo:

 

 

Mwalimu:                      Fungua mikono yako nikuchape.

‘Abdullaah:                    Hapana! Huwezi kunipiga mimi.

Mwalimu:                      (Akaanza kuhamaki) Fungua mikono yako ewe ‘Abdullaah nikuchape!

‘Abdullaah:                     Nakuambia huwezi kunipiga mimi!

Mwalimu:                       Akapandisha sauti kwa ukali: Husikii nakuambia fungua mikono yako nikuchape?

‘Abdullaah:                    WaLlaahi huwezi kunichapa mimi! Wallahi huwezi kunichapa mimi!

Mwalimu:                      (Akipigwa mshangao mkubwa) Unasema nini ewe ‘Abdullaah? Nitakuchapa mimi popote kama hutaki kufungua mikono yako!

‘Abdullaah:                      Nimekuambia mwalimu kuwa huwezi kunichapa mimi, hebu jaribu kunichapa kama unataka.

 Mwalimu:                      (Hali hii ikamfanya mwalimu apigwe na bumbuwazi asiweze kumchapa na badala yake kutaka kujua kwanza sababu ya kusema hivyo) Kwa nini unasema hivyo ewe ‘Abdullaah?

 

‘Abdullaah:                     Je, kwani hukusikia Hadithi ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyosema kuwa ((Yeyote atakayeswali Swalah ya Alfajiri atabakia katika himaya ya Allah?)) Na mimi nimeswali Swalah ya Jamaa'h Alfajiri msikitini, kwa hiyo niko katika himaya (kuhifadhiwa) ya Allaah. Na vile vile sikufanya kosa lolote la wewe kuniadhibu.

 

Mwalimu akasimama akiwa ameshangazwa na maneno ya ‘Abdullaah na huku akaingiwa na unyenyekevu kwa Allaah (Subhaanah wa Ta'aala). Akatoka na kwenda kumuelezea mkuu wa shule ili aitwe baba yake ‘Abdullaah ili apewe hongera kwa kumpa mwanawe malezi mema ya kumzoesha kwenda kuswali Swalah za Jamaa msikitini.

 

Lakini masikitiko ni kwamba alipokuja baba yake ‘Abdullaah ilikuwa ni mshangao kwa kila mmoja. Kwani walitambua kuwa baba huyo hakuwa ni mtu wa kujali malezi ya mtoto wake, wala hawakumuona kuwa ana alama ya uchaji Allaah usoni mwake. Kila mmoja akamuuliza : "Wewe kweli ni baba yake ‘Abdullaah?" Akajibu: "Ndiyo".

 

Wakamuuliza ‘Abdullaah: "Huyu kweli ni baba yako ewe ‘Abdullaah?" Akajibu: 'Ndio lakini yeye haji kuswali Swalah za Jamaa na mimi msikitini".

 

Mwalimu wake ‘Abdullaah akamuelezea yaliyotokea darasani baina yake na ‘Abdullaah. Baba yake ‘Abdullaah akaguswa sana na kisa cha mwanawe, na ikawa ni sababu ya yeye kurudi kwa Allaah (Subhaanah wa Ta'aala) na tokea siku hiyo akawa ni mwenye kuswali Swalah zote za Jamaa msikitini.

 

Subhaanah Allah! Tazama jinsi gani Swalah inaweza kutuathiri sisi na kutufundisha kuwa tusimkhofu mtu yeyote ila tumkhofu Allaah (Subhaanah wa Ta'aala). Hakika Swalah ni chanzo cha nguvu kwa Muumini, ni mwangaza unaomuongoza mtu katika njia iliyonyooka..  

 

Enyi ndugu Waislamu, msisahau kwamba maneno ya mwisho ya Mtume wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya kuaga dunia hii, yalikuwa ni nasaha kwetu tusiache Swalah kwani ni mawasiliano na Mola wetu Mtukufu. Swalah inayo majibu ya Du'aa zetu, mwanga katika nyuso zetu, ni hifadhi yetu kutokana na machafu na maovu, ni kisaidizi chetu katika migogoro na ni mwanga katika makaburi yetu.

Watu wengi wamo katika khofu na wasiwasi, wanakosa raha kwani hawana utulivu wa nyoyo. Na ukiwazingatia watu kama hawa utaona kwamba ni wale wanaoacha Swalah na kushughulika na dunia zaidi. Vipi mtu hataki kumuabudu Mola wake Ambaye Ndiye Anayemjaalia kuwa na umri na afya ya kuweza kuishi? Bila ya kumuomba Mola wake Azidi kumpa umri na afya atawezaje mtu kuendeleza maisha yake?

 

Utaona mtu anaweka kengele ya saa  Alfajiri kwa ajili ya kuwahi kazini, na sio kwa ajili ya Swalah, hivyo ameona kuwa kazi kwake ni bora kuliko kumuabudu Mola wake Ambaye Akitaka Anaweza Amfanyishe asiweze hata kwenda huko kazini kwa kumpa ugonjwa au maafa au mauti. Basi umefikiria  hilo ewe Muislamu usiyeswali?   

 

Tukumbuke kuwa jambo la kwanza tutakaloulizwa siku ya Qiyaamah ni Swalah zetu. Ikiwa tumezitimiza zinavyopasa basi mambo mengine yatakuwa salama Insha Allaah.  Kwa hiyo na tujitahidi kuzitimiza Swalah zetu na kuwakumbusha na kuwahimiza watoto wetu, ndugu zetu, jamaa zetu wote katika familia, na ndugu zetu Waislamu umuhimu wa Swalah.

 

Wa BiLlaahi Tawfiyq.

0 Comments