Kubadilishwa rasmi matumizi ya jumba la makumbusho la Hagia Sophia na kuwa msikiti

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametoa amri ya kubadilisha matumizi ya jumba la makumbusho la Hagia Sophia na kulifanya msikiti.

Uamuzi huo wa Rais wa Uturuki umekabiliwa na upinzani mkubwa wa Umoja wa Ulaya na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na baadhi ya nchi duniani zikiwemo Ugiriki, Marekani na Ufaransa. Licha ya upinzani huo, Rais Erdoğan wa Uturuki anasema kubadilishwa matumizi ya jumba la makumbusho la Hagia Sophia na kuwa msikiti ni suala la ndani ya nchi na kusisitiza kuwa: Uingiliaji wa kigeni katika kadhia hiyo haukubaliki.

Awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki alikuwa amesema kuwa: "Tunaikumbusha tena Uturuki iheshimu majukumu yake ya kimataifa na isitangulize mbele maslahi ya ndani na ya kitaifa kuliko kulinda majengo muhimu kama Hagia Sophia ambayo ni turathi ya kimataifa ya wanadamu."
Katika mazingira kama haya inatupasa kujiuliza kwamba, ni kwa nini UNESCO na nchi za Magharibi kama Ugiriki ambayo ndiyo nchi pekee katika Umoja wa Ulaya ambayo mji wake mkuu hauna hata msikiti mmoja, zinapinga uamuzi wa Rais wa Uturuki na wakati huo huo zimenyamazia kimya bomoabomoa ya misikiti katika mji wa Athens? Ni wazi kuwa maadamu serikali ya Uturuki inaendelea kutekeleza siasa za kimagharibi, harakati zote za Ankara za kutaka kuwa na siasa huru na za kutokuwa tegemezi kwa Magharibi zitakuwa na gharama na madhara kwa Uturuki. Vilevile inatupasa kudokeza hapa kwamba, upinzani huo wa nchi za Magharibi na jumuiya za kimataifa unaweza kuisababishaia matatizo makubwa serikali ya Uturuki katika siku za usoni. 

Pamoja na hayo upinzani wa Ugiriki dhidi ya uamuzi wa Uturuki wa kubadili matumizi ya jumba ya makumbusho la Hagia Sophia kuwa msikiti ni mwendelezo wa hitilafu nyingi zinazotawala uhusiano wa pande hizo mbili. Hata hivyo dunia inapasa kuelewa kuwa uamuzi huo wa Recep Tayyip Erdoğan unaoana na matakwa ya idadi kubwa ya raia Waislamu wa Uturuki. Kwa maneno mengine ni kuwa, Erdoğan amepasisha uamuzi na matakwa ya wananchi ya kubadilishwa matumizi ya jumba la makumbusho la Hagia Sophia kuwa msikiti.

Hata hivyo baadhi ya wanasiasa na wataalamu wa kambi ya upinzani nchini Uturuki wanasema uamuzi huo unairudisha nyuma nchi hiyo na kwamba ni sawa na kufuta historia ya miaka 1000 ya Uturuki.

Kuhusiana na suala hilo mwandishi habari na mtaalamu maarufu wa masuala ya vyombo vya habari wa Ankara, Yıldıray Oğur aliandika makala mwezi uliopita akisema: "Maudhui ya kubadilishwa matumizi ya jumba makumbusho la Hagia Sophia kuwa msikiti ilitumiwa kwa mara ya kwanza kwa malengo ya kisiasa katika muongo wa 1965. Tunaweza kusema kuwa, suala la Waislamu kutumia jumba hilo kwa ajili ya ibada ya Swala lina historia ya miaka 55."

Tukiachilia mbali madai hayo ya mpinzani wa serikali ya Ankara ambayo yumkini yakawa yanaakisi mitazamo ya nchi za kigeni, inatupasa kusema kuwa, katika zama za utawala wa Roma ya Mashariki, Hagia Sophia ilikua kanisa. Eneo hilo lilibadilishwa na kuwa msikiti baada ya watawala wa kituruki wa Ottoman Empire kuudhibiti mji wa Istanbul, na baada ya kuundwa Jamhuri ya Uturuki na kushika madaraka Mustafa Kemal Atatürk, Hagia Sophia ilibadilishwa na kuwa jumba la makumbusho, na ilibakia hivyo hivyo hadi hii leo.

Kwa ujumla inatupasa kusema kuwa, hatua ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ya kubadili matumizi ya jumba la makumbusho la Hagia Sophia kuwa msikiti yumkini likapelekea kupatikana mshikamano wa kitaifa, lakini suala hilo hilo litatumiwa na Wamagharibi kama fimbo ya mashinikizo zaidi dhidi ya nchi hiyo yenye ushawishi katika eneo la magharibi mwa Asia.  

0 Comments