Kufanyika swala ya kwanza ya Ijumaa katika msikiti wa Hagia Sophia

Sala ya kwanza ya Ijumaa ilisaliwa Ijumaa katika msitiki wa Hagia Sophia nchini Uturuki tarehe 24 mwezi huu wa Saba baada ya miaka 86 kwa kuhudhuriwa na rais, viongozi wa serikali na pia wananchi wa nchi hiyo.

Baadhi ya televisheni za Uturuki zilionyesha mubashara sala hiyo ya kwanza ya Ijumaa kuswaliwa katika msikiti wa Hagia Sophia baada ya kubadilishwa matumizi ya eneo hilo takatifu. Idadi kubwa ya wananchi wa Uturuki walitii sheria za kutokaribiana watu ndani ya msikiti huo na katika maeneo ya wazi kando yake.

Kufanyika Sala ya kwanza ya Ijumaa katika msikiti wa Hagia Sophia kuna umuhimu mkubwa kwa serikali na wananchi wa Uturuki na pia kwa Ulimwengu wa Kiislamu. Ukweli ni kuwa hatua hiyo ya serikali ya Uturuki inaweza kutajwa kuwa ni ushindi mbele ya sehemu muhimu ya Ulimwengu wa Magharibi. Hasa ikizingatiwa kuwa, Marekani, aghalabu ya serikali za Magharibi na hata taasisi za kimataifa zilionyesha radiamali hasi kufuatia hatua ya Rais wa Uturuki ya kutangaza mwezi Mei mwaka huu suala la kubadili matumizi ya jumba hilo la makumbusho na kuwa msikiti wa Hagia Sophia.Kuhusiana na suala hilo, hata baadhi ya serikali za Magharibi kama Ugiriki na Ufaransa pia zilitoa vitisho kwa hatua hiyo ya serikali ya Ankara. Kwa mfano, serikali ya Ugiriki ambayo ina historia ya uhusiano uliojaa mivutano na mizozo kati yake na Uturuki, tarehe 29 mwezi Mei mwaka huu ililisema kuwa kusomwa aya za Qur'ani ndani ya Hagia Sophia haikubaliki na kwamba hatua hiyo inajeruhi hisia za kidini za Wakristo duniani. Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki pia alisema: "Tunaikumbusha Uturuki iheshimu majukumu yake ya kimataifa; na isifadhilishe maslahi yake ya ndani na ya kitaifa juu ya kulinda majengo muhimu kama Hagia Sophia ambayo ni turathi za kimataifa za mwanadamu.  

Viongozi wa serikali ya Ugiriki wametoa matamshi kama haya katika hali ambayo Athens ni mji mkuu pekee wa Ulaya usiokuwa  na msikiti. Wakati huo huo, viongozi wa Athens wamebomoa aghalabu ya maeneo matakatifu ya Kiislamu khususan misikitiki nchini humo ikiwa ni katika kuendelea  hitilafu kati ya Ugiriki na Uturuki. Waziri wa Utamaduni wa Ugiriki pia ameitaja hukumu ya Mahakama ya Uturuki ya kuibadili  Hagia Sophia na kuwa msikiti kuwa ya kichochezi.  

Katibu Mku uwa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) amesema amesikitishwa na uamuzi wa serikali ya Uturiki wa kubadili matumizi ya Hagia Sophia kuwa msikiti na kusisitiza kuwa: ''Unesco inapasa kupewa taarifa kuhusu kubadilishwa kivyovyote kwa Hagia Sophia; na mabadiliko hayo kuchunguzwa katika kamati ya turathi za kimataifa za shirika hilo.   

Joseph Borrell Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya pia ametoa taarifa na kueleza kusikitishwa na uamuzi huo.  

Naye Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amesema: Amevunjwa moyo na uamuzi huo wa Uturuki. Hagia Sophia kilikuwa kituo cha kanisa la Orthodox la Ugiriki kwa zaidi ya miaka 900; na eneo hilo lilibadilishwa kwa ajili ya matumizi ya msikiti baada ya kukombolewa Istanbul na utawala wa Othmania mwaka 1453. Kiujuma tunapasa kusema kuwa kufanyika Swala ya kwanza ya Ijumaa katika msikiti wa Hagia Sophia kumeandaa uwanja wa kushikamana zaidi wananchi na serikali ya Uturuki licha ya serikali mbalimbali za Magharibi kubainisha wasiwasi wazo kufuatia hatua hiyo. 

0 Comments