Kuna hekima kubwa nyuma ya ukewenza

Mwenyezi Mungu Aliyetukuka hawawekei Allah sheria ngumu kuitekeleza au itakayowaletea madhara katika maisha yao. hivyo, hata sharia ya ukewenza iliyokuja ndani ya Qur’an na Sunna haina kasoro au madhara.

Awali ya yote, ijulikane kuhalalishwa kwa ukewenza ni uamuzi ya Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu na Hekima, Muumba wa binadamu, anayeyajua mahitaji yao hata kabla ya kuwaumba. Kwa sababu hiyo, sharia ya ukeweza katika Uislamu ni makini na haimdhulumu yoyote washirika wa ndoa za aina hiyo. Ukiona dhuluma na unyanyasaji, elewa kuwa hayo ni matokeo ya ukiukwaji wa vipengele vya sharia hiyo.

Ni kweli kuwa, kimaumbile wanawake wengi hawapendi ndoa za ukewenza. Hata hivyo, aghalabu, wengi wao wakishaolewa kwenye ndoa hizo hugundua faida zake. Hivyo, napenda niwarai wanawake kuwa wasimpe pole mwenzao ambaye mume wake kaoa mke mwengine bali wamtie moyo kwani amri hii ya Mwenyezi Mungu ina hekima kubwa.

Ni ukweli usiofichika kwamba ukeweza una hekima kubwa na faida nyingi na ilikuwa yatosha kwetu kuamini ukewenza ni jambo jema kwa sababu Bwana Muumba, Mjuzi wa kila kitu na Mwenye Hekima ameruhusu jambo hilo na hivyo lina faida. Pamoja na hayo, katika makala haya tutataja baadhi ya hekima za ukewenza kama zilivyotajwa na wanazuoni wengi.

Baada ya kufunga ndoa inaweza kuthibibitika kitaalamu kwamba mke hana kizazi. Katika hali hiyo, badala ya kumuacha mkewe anayempenda, mume anaweza tu kuongeza mke mwingine (au wengine) ambapo kupitia wake hao huenda wataruzukiwa watoto.

Hekima ya pili ni pale mke anapokuwa na maradhi makubwa na ya muda mrefu kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yake kinyumba. Mume ataongeza mke mwingine ambaye atamkidhia haja zake za kimaumbile kwa njia sahihi, halali na salama, wakati huo huo akiendelea kubaki na kuhangaika kumtibu.

Hekima ya tatu ya mume kuongeza mke ni kutosheleza matashi ya kimwili. Kama tunavyojua, kutosheleza matashi ya kimwili ni moja ya malengo makuu ya ndoa. Nguvu hizi kwa wanaume wengi ziko juu siku zote usiku na mchana. Hata wanaume wenyewe wanatafautiana kwa hili, wengine wana nguvu zaidi. Kwa upande wa pili, matamanio ya mwanamke, aghlabu hayawezi hayafikii ya mwanamme.

Katika hali hiyo, kwa mwanamme kuongeza mke ni njia ya kutosheleza matashi haya kwa njia ya salama na kuzimua nguvu kali za kimaumbile. Je lipi bora? Umbane mwanamme asioe halafu matokeo amuasi Mola wake kwa kutafuta wanawake wa pembeni wa kuzini nao? Au bora aoe atimize matashi yake katika njia ya halali na salama? Bila shaka kuongeza mke ndiyo suluhu.

Kuirejesha ndoa ni hekima nyingine ya ukewenza. Sharia ya ukewenza hutoa fursa ya kuirejesha ndoa baada ya talaka. Chukulia mume amemuacha mkewe kisha akaoa mwingine. Iwapo maelewano yakipatikana baina ya mume na yule mke wa kwanza, hapo huwa rahisi kwa mume kumuoa tena mke wa kwanza na hivyo kuendelea na maisha yao.

Kwa upande mwingine, ana siku kadhaa ambazo hazimruhusu kumkamilishia furaha mumewe. Mwenyezi Mungu amejaalia kuwa hii ni ibada ya mwanamke yoyote ya kila mwezi. Si hivyo tu, mwanamke pia hubeba ujauzito na kisha kulea mtoto. Vilevile, ana kazi nyingi za nyumbani na hivyo hutokea wakati fulani kuchoka.

Katika mazingira kama haya, inafaa kumhurumia mwanamme shababu ,mwenye afya njema ambaye aghalabu hushindwa anaweza kujikuta anashindwa kumgojea mkewe mpaka awe tayari tena. Kwa maana hiyo, pasingekuwa na ruhusa ya kuongeza mke, mwanamme angeishi maisha ya huzuni na huenda hata angejikuta anaingia kwenye maasi ya kuwakodolea macho wanawake wasio halali yake njiani.

Ukewenza pia ni chachu ya mapenzi. Nafsi ina tabia ya kukichoka kitu au hukichukia, hata kama kizuri na kinapendeza kiasi gani. Kadri mwanamke atakavyompenda mumewe, lakini iwapo atakuwa anamtia maachoni kila siku, kila wakati; nafsi itamkinai.

Kwa mantiki hiyo, ukewenza ni sababu ya kumuondolea uchovu mwanamke, na pia kuzidisha mapenzi na mazoeano baina ya mume na mke. Mwanamme kugawa zamu humpa mwanamke hamu na shauku ya kutaka kumona mumewe pale anaporudi kutoka zamu kwa mke au wake wengine. Mwanamme naye huwa na shauku ya kumuona mke wake mwingine kwenye zamu.

Ukewenza pia ni chuo bora cha kuilea na kuitakasa nafsi na uchoyo, na kuipamba na subira na kujua haki za wengine. Binadamu katika maisha haya anatakiwa aishi kijamii, na hawezi kufikia hapo mpaka awe tayari kusamehe baadhi ya haki zake kwa ajili ya wengine. Hali ya mwanamke kung’ang’ania kubaki peke yake tu, hujengwa na tabia ya umimi na uchoyo. Kwa nini usikubali mwanamke mwenzako asitirike, kama ulivyositirika wewe? Kwa mwanamke kujiunga na chuo hiki (ukeweza) ni hatua muhimu ya kupata mafunzo ya kuilea nafsi.

Wanawake wa Kiislamu wanatakiwa waige wanawake wema waliotangulia wakiwemo wakeze Mtume ambao ukiacha Bi. Khadija , wote waliobaki waliishi maisha ya ukewenza. Hali ni hiyo hiyo kwa wake wa Makhalifa Waongofu na Maswahaba wengine.

Katika walosoma wakafaulu vizuri katika chuo cha ukewenza ni Bi Saudat (Allah amridhie) ambaye aliolewa na Mtume mara tu baada ya kufariki Bi. Khadija (Allah amridhie). Huyu ndiye mwenyeji aliyewakaribisha wakeze wengine Mtume katika ukeweza, baada ya kuishi naye kwa miaka mitatu akiwa mke pekee.

Kwa kumalizia makala hii, napenda kuonya kuwa iwapo jamii italipuuzia suala hili la sharia ya ukewenza tutaishia kubeba mzigo mzito na mtihani mkubwa kwa kuwa na mabinti na wajane wengi. Ikumbukwe kuwa, ni haki ya mabinti hawa ya kimsingi kukidhi matashi yao ya kimaumbile. Iwapo wakiikosa haki hii kwa njia ya halali, wataitafuta kwa lazima kupitia njia za vichochoroni za haramu za zinaa. Kwa hiyo, kimantiki, inatudhihirikia kuwa faida za ukewenza kwa wanawake ni kubwa zaidi kuliko kwa wanaume.

Wito wangu kwa Waislamu ni kuwa tuzisome sharia za Mwenyezi Mungu kwa makini na kujua hekima zake, kisha tuzinyenyekee katika utendaji wetu wa kila siku ili tupate radhi zake, vinginevyo tukisikiliza maneno ya maaduui wa Uislamu yatatudhuru na kututoa katika dini.

0 Comments