Mahakama Misri yathibitisha hukumu ya kifungo cha maisha jela alichohukumiwa kiongozi wa Ikhwanul Muslimin

Mahakama Kuu ya Misri imethibitisha hukumu ya kifungo cha maisha jela aliyopewa kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin Muhammad Badie pamoja na wenzake watano.

Vyombo vya habari vimeripoti kutoka Cairo kuwa, Mahakama Kuu ya Misri imetupilia mbali rufani aliyokata kiongozi huyo mkuu wa Ikhwanul Muslimin pamoja na wanachama wengine kadhaa waandamizi wa harakati hiyo na kuidhinisha hukumu ya awali ya kifungo cha maisha jela iliyokuwa imetolewa dhidi yao katika kesi ya "Ofisi ya Mwongozo". 


Kabla ya hukumu hiyo iliyothibitishwa jana Alkhamisi, Muhammad Badie alikuwa tayari ameshahukumiwa mara kadhaa kifungo cha maisha jela katika kesi nyingine zilizokuwa zikimkabili. Tarehe 5 Desemba 2018, mahakama ya Misri ilimhukumu kifungo cha maisha jela kiongozi huyo wa Ikhwanul Muslimin katika kesi hiyo iliyohusiana na matukio yaliyojiri katika "Ofisi ya mwongozo". Mwaka 2017 pia mahakama ya rufani ya Misri ilithibitisha hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya Muhammad Badie katika kesi za matukio ya Ismailiya na mauaji ya raia watatu.


Kiongozi huyo wa Ikhwanul Muslimin amehukumiwa pia adhabu za kutumikia vifungo jela, nyingi zao zikiwa za vifungo vya maisha katika kesi nyingine kadhaa zikiwemo za matukio ya Suez, al-Istiqama, Qalyub, uvamizi wa jela na kuvunjia heshima vyombo vya mahakama.

Wakati huo: Rais Muhammad Morsi (kulia) na Waziri wa Ulinzi Jenerali Abdel Fattah el Sisi
Baada ya jeshi la Misri likiongozwa na Waziri wa Ulinzi Jenerali Abdel Fattah el Sisi kufanya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Mohammad Morsi mnamo tarehe 3 Julai 2013 na kuondolewa madarakani rais huyo wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo, viongozi wote waandamizi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin akiwemo Morsi mwenyewe walikamatwa na kutiwa gerezani. Tangu wakati huo hadi sasa, mahakama za Misri chini ya utawala wa el Sisi zimeshatoa hukumu za vifo, vifungo vya maisha jela na vya miaka kadhaa kwa viongozi na wanachama wengi waandamizi wa Ikhwanul Muslimin. 

Morsi mwenyewe, aliaga dunia tarehe 17 Juni 2019 baada ya kuanguka mahakamani alifikishwa kujibu moja ya kesi zilizokuwa zikimkabili.../

0 Comments