Mambo yanayoharibu amali

YANAYOHARIBU AMALI NJEMA ZA MJA

Mja anapojitahidi kufanya ibada za wajibu na sunna, anapata ujira adhimu mbele ya Allah kutokana na amali zake hizo. Hata hivyo, yapo mambo ambayo Muumini anapaswa kujichunga nayo ili asiharibu matendo yake mema. Juu ya hilo, Allah Mtukufu anasema:

“Enyi Mlioamini! Mtiini Allah na mtiini Mtume, wala msiviharibu vitendo vyenu.” [Qur’an, 47:33]. Akasema tena Mwenyezi Mungu: “Na anayemuasi Allah na Mtume wake, na kuiruka mipaka yake, (Allah) atamwingiza motoni, humo atakaa milele na atapata adhabu ifedheheshayo.” [Qur’an, 4:14]. Kwa kuzingatia hayo, makala hii itakufafanulia mambo matano ya msingi ambayo Waislamu wanapaswa kujiepusha nayo ili waweze kulinda na kuhifadhi amali njema walizofanya. Na sasa tutataja mambo hayo yaliyotajwa kuwa yanaharibu amali njema za mja

Mosi, kumshirikisha Allah

Neno shirk, maana yake ni kumwekea Allah mshirika katika Uungu wake au ibada yake au sifa zake. Na shirk ndiyo dhambi kubwa kuliko madhambi yote na ni dhuluma kubwa isiyo na msamaha mbele ya Allah.

Allah anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika huyo amezua dhambi kubwa.” [Qur’an, 4:48].

Na imepokewa kutoka kwa Abdullah bin Mas‘oud (Allaa amridhie) amehadithia kwamba, iIlipoteremshwa aya hii:

“Wale walioamini na hawakuchanganya imani zao na dhuluma.” [Qur’an, 6:82], watu walitatizika, wakasema: “Nani katika sisi hajadhulumu nafsi yake?” Mtume akawaambia: “Si kama vile mnavyomaanisha! Hamsikii pale mja mwema aliposema, ‘Ewe mwanangu! Usimshirikishe Allah, hakika shirk ni dhuluma kubwa mno!” [Ahmad].

Kwa kutambua uzito wa dhambi hii (shirk), Allah Aliyetukuka alimwambia Mtume wake:

“Na kwa yakini, yamefunuliwa kwako na kwa waliokuwa kabla yako: Bila ya shaka ukimshirikisha Mwenyezi Mungu, amali zako zitaanguka, na lazima utakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara.” [Qur’an, 39:65]. Hivyo, ni wajibu kwa waja kumpwekesha Allah pasina kumshirikisha na chochote.

Pili, kuichukia haki

Kuichukia haki ni sababu ya kuporomoka na kuharibika kwa matendo ya mja kama anavyobainisha Mwenyezi Mungu:

“Hayo ni kwa sababu wao walifuata yaliyomchukiza Mwenyezi Mungu na wakachukia yanayomridhisha, basi akaviangusha vitendo vyao.” [Qur’an, 47:28].

Uislamu, ambao ni mfumo kamili wa maisha ya mwanadamu umetufundisha mambo mengi. Miongoni mwa mambo hayo ni suala la kumuabudu Allah na kuamiliana na watu kwa wema na huruma. Bahati mbaya sana, watu wengi wamepuuza mambo ya wajibu na wengine wamefikia hatua ya kuyachukia na kuyabeza.

Tatu, kumtangulia Allah na Mtume wake

Miongoni mwa adabu njema anazopaswa kuwa nazo kila Muislamu ni kulazimiana na mafundisho ya Allah na Mtume wake (rehema za Allah na amani zimshukie). Hata hivyo, tumekuwa tukishuhudia mara kwa mara baadhi ya watu wakimvunjia heshima Allah na Mtume wake. Huu ni utovu wa nidhamu, na ni ukosefu wa adabu kwa Allah Aliyetukuka na Mtume wake.

Juu ya hilo, Allah Mtukufu anaonya: “Enyi mlioamini! Msitangulie mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua. Enyi mlioamini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa kelele kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi, visije vitendo vyenu vikaharibika, na hali hamtambui.” [Qur’an, 49:1–2].

Nne, unafiki

Unafiki ni miongoni mwa mambo yanayoharibu imani ya Muislamu na kuporomosha amali njema alizofanya. Katika kuwazungumzia wanafiki, Allah Mtukufu anasema:

“Utawaona wale wenye maradhi nyoyoni mwao wanakimbilia kwao wakisema, ’Tunahofu yasitusibu mabadiliko.’ Huenda Mwenyezi Mungu akaleta ushindi au jambo jingine litokalo kwake wakawa wenye kujuta kwa waliyoyaficha katika nafsi zao. Na walioamini watasema, ‘Hivyo hawa ndiyo wale walioapa ukomo wa viapo vyao kuwa wao wako pamoja nanyi? Vitendo vyao vitapotea bure, na wataamkia kuwa wenye hasara.’” [Qur’an, 5:52–53].

Tano, ria (kujionesha)

Duniani, watu hufanya mambo mbalimbali ya kheri kwa malengo tofauti. Miongoni mwao, wapo waja wema ambao hufanya mambo ya kheri kwa utakasifu wa nia na kutaraji malipo kutoka kwa Allah.

Lakini, kwa upande mwingine, wapo wafanyao mema kwa malengo ya kupata maslahi ya kidunia. Hili ni mojawapo ya mambo aliyoyakemea Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Mtume ametuambia:

“Tahadharini na shirk iliyojificha. Mtu anasimama kusali, anaipamba na kuiremba sala yake kwa kujua kuwa kuna watu wanamtazama.” [Ibn Khuzaymah].

0 Comments