Muongozo wa Uislamu katika kutembeleana

Mara nyingi inaelezwa kwamba Uislamu ni dini ya maumbile na ni mfumo mzima wa maisha ya wanadamu hapa ulimwenguni. Hivyo basi, hakuna nukta yoyote ya maisha ila Uislamu umeielekeza kwa ufasaha kabisa.

Moja ya mambo ya kimaumbile na ni kawaida sana kutokea katika maisha ya watu ni kualikana na kutembeleana. Ziara rasmi zilizotanguliwa na wito ama mualiko na zisizo rasmi (za bahati-bahati) ni kawaida sana kutokea.

Ndugu, jamaa na marafiki, hupenda kualikana mmoja mmoja majumbani au wengi pamoja kwenye chakula cha karamu. Ni kosa kudhani kwamba, Uislamu umeacha suala kubwa kama hili watu walifanye kwa namna waonavyo, bila kuliwekea kanuni.

Umuhimu wa kutembeleana

Tunajifujifunza kitu kutokana na tukio la Mtume Ibrahim (amani ya Allah imshukie) kufikiwa na Malaika nyumbani kwake ambao hata hivyo hakuwajua mara moja kwa vile walikuja kwa sura za binadamu. Nabii Ibrahim aliwachangamkia na kuwaandalia chakula kama inavyoelezwa katika Qur’an. Hili ni moja ya dalili zinazotilia mkazo suala la kutembeleana na kuwakirimu wageni. [Qur’an, 11 :69-71].

Katika kutaja faida za kutembeleana, Mtume ([rehema za Allah na amani zimshukie] amesema:

“Atakayemkagua mgonjwa au akamtembelea nduguye katika imani, huambiwa na Malaika, ‘Umefanya vyema, na umebarikiwa katika ziara yako, na umeandaliwa makazi peponi.’” [Tirmidhi].

Makala yetu wiki hii inalenga kukuelewesha mpendwa msomaji mafunzo ya Uislamu juu ya suala la kualikana na kutembeleana, kwa mujibu wa Qur’an na Sunna, tukiamini kwamba utafaidika vya kutosha inshaAllah.

Muislamu anapotaka kualika ama kuwatembelea wengine anatakiwa achunge nidhamu kadhaa.

ADABU (NIDHAMU) ZA KUALIKA

Awaalike wacha Mungu Ikitokezea Muislamu anaalika wageni nyumbani kwake, apendelee zaidi kualika watu wema, wacha Mungu na wenye tabia njema. Katika hili Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] anasema:

“Usifanye urafiki na mtu ila Muumini, na wala asile chakula chako ila mchamungu.” [Ahmad, Abuu Daud].

Moja ya hekima ya jambo hilo ni ili wamuombee dua. Lakini pia, mgeni hutarajiwa kuacha athari kwa familia aliyoitembelea.

Haitarajiwi waalikwa waovu – kama vile walevi, wazinzi, wenye lugha chafu na wengine kama hao – kumuombea dua mwenyeji baada ya kuwakirimu au kuibakishia familia yake athari njema.

Angalizo

Si vibaya kumualika mtu mwenye maasi au tabia mbaya iwapo mwenyeji ana lengo la kumrekebisha, lakini ili afikie lengo lake, inashauriwa asimrekebishe kwa wito wa mara ya kwanza.

Bali yafaa amuite mara nyengine, na labda hata mara ya nyingine, ndio amlinganie. Pia, yatakiwa asimlanganie mgeni ila baada ya kumkirimu. Pia, asifanye hivyo mbele za watu bali wakiwa wawili peke yao.

Mualiko usiwe kwa matajiri tu

Lengo la kuwaalika wageni ni kutekeleza agizo la sharia, na kupata radhi za Allah kwa kitendo cha kuingiza furaha ndani ya nyoyo za Waumini kwa kule kuwakirimu. Kwa hiyo, haitakiwi kuwahusisha matajiri tu au watu maarufu na kuwaacha mafakiri, bali awaalike wote.

Mtume anasema: “Chakula kibaya zaidi ni karamu, kwani hualikwa matajiri na kuachwa masikini/ mafakiri.” [Bukhari na Muslim].

Ikhlas

Maana ya Ikhlas ni kufanya kwa ajili ya Allah. Muislamu anatakiwa aitakase nia yake kwa kila jambo analolifanya, ikiwemo jambo la kuwakaribisha wageni na kuwakirimu kwani nalo hilo ni tendo la kibada. Mualikaji anatakiwa akusudie kufuata Sunna ya Mitume na sio kujifaharisha, kutaka sifa au umaarufu. Vile vile, kama tulivyogusia, awe na lengo la kuingiza furaha na mapenzi katika nyoyo za ndugu zake Waislamu.

Asimualike ambaye itamsumbua kufika

Uislamu ni dini nyepesi na haitaki wafuasi wake kupata uzito wowote. Kwa msingi huo, na kama lengo ni kumfanya mgeni kujisikia furaha akiwa kwako, si vema kumualika mtu ambaye unajua itamuwia uzito kuja kwako na kurudi atokapo kwa sababu ya umbali au shida za safirini. Kadhalika, haipendezi kumualika ambaye kutakuwa na jambo la kumuudhi, kama vile kuwakutanisha wake wenza wasioelewana, au wanaodaiana bila taarifa.

Kwa maneno mengine, kama unajua kwamba fulani na fulani hawaelewani kwa sababu moja ama nyengine, si vyema kuwaalika pamoja mahala ambapo palitarajiwa kutawaliwa na furaha na bashasha na nyuso kukunjuka. Utakuwa umewapa mtihani mzito.

Adabu za kuitika mwaliko

Muislamu anapopata wito wa ndugu yake, kama hana dharura ya nafsi yake au ya dini, anatakiwa asikatae, bali aende tena bila ya kuchelewa. Utaratibu huu, wa kutokataa mialiko, ndio alioufuata Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie] na ndio walioufuata Maswahaba na wema waliotangulia. Katika hadith amesema Mtume (rehema za Allah na amani zismhukie):

“Atakayeitwa na aende.” [Muslim].

Jambo muhimu la kuwakumbusheni hapa ni kwamba, Muislamu hatakiwi kuwa na ubaguzi katika kuitikia mualiko na kuwatembelea ndugu zake. Anapaswa kwenda kwa wenye uwezo na mafakiri pia, watu maarufu wa kawaida. Na huu pia ndio ulikuwa mwenendo wa Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie].

Kukataa mualiko eti kwa sababu mualikaji ni maskini na hivyo hana uwezo wa kukirimu, ni moja ya aina za kiburi; na kiburi ni haramu. Kukataa mwaliko pia pia ni kumvunja moyo ndugu yako na kuziathiri hisia za upendo wake kwake. Kitendo hicho pia kuleta dhana ya utabaka katika jamii iliyotakiwa ishikamane na kuwa kitu kimoja.

Akiwa amefunga

Kimsingi, mmoja wetu anapoalikwa sehemu, moja ya malengo ni kukirimiwa kwa chakula. Hivyo, mwenyeji huwa amejipanga kwa hilo kadri ya uwezo wake.

Hata hivyo, inaweza kutokea siku mgeni amefunga. Katika mazingira haya, mgeni aliyealikwa anashauriwa afungue na ale chakula hususan iwapo mwenyeji wake anapendelea hilo. Hata hivyo, usifungue swaum iwapo ni katika mwezi wa Ramadhan.

Lakini, mualikwa akiamua aendelee na swaum yake, si vibaya pia. Tunajifunza hayo katika kauli ya Mtume isemayo:

“Mmoja wenu akialikwa na aende, ikiwa amefunga na amuombee dua (ndugu yake), na kama hakufunga ale.” [Muslim].

0 Comments