OIC yalitaka Baraza la Usalama lisimamishe uporaji wa ardhi za Wapalestina

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka za kusitisha utekelezaji wa mpango wa utawala haramu wa Israel wa kutwaa ardhi zaidi za Palestina huko Katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mwito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa OIC, Yusuf al-Uthaimeen katika barua yake kwa nchi wanachama wa Baraza la Usalama na na kamati ya pande nne ya kutatua mgogoro wa Asia Magharibi inayojumuisha Umoja wa Ulaya, Russia, Umoja wa Mataifa na Marekani.

Barua hiyo imelitaka Baraza la Usalama lichukue hatua za kivitendo za kuzuia utekeleza wa mpango huo wa kughusubiwa ardhi zaidi za Wapalestina.

Katibu Mkuu wa OIC amelitaka Baraza la Usalama liitishe mkutano wa dharura ili kuhuisha jitihada za kuipatiwa ufumbuzi wa kudumu kadhia ya Palestina kwa kutumia mchakato wa kisiasa chini ya uangalizi wa jamii ya kimataifa.

Hali kadhalika jumuiya hiyo imesema kuwa inapinga pendekezo lolote ambalo halitambui rasmi haki ya taifa la Palestina ya kujitawala. Hivi karibuni pia, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ilitahadharisha juu ya matokeo mabaya ya uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kutaka kuzipora na kuzikalia kwa mabavu ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kulaani vikali hatua hiyo.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa umepanga kwamba Jumatano iliyopita ya tarehe Mosi Julai ungeanza kutekeleza mpango wake haramu wa kupora na kuunganisha asilimia 30 ya ardhi za Ukingo wa Magharibi na ardhi nyingine za Palestina unazozikalia kwa mabavu. 

Hata hivyo umelazimika kuakhirisha tarehe ya utekelezaji wa mpango huo baada ya kushadidi mashinikizo ya upinzani ya Wapalestina na ya nchi mbalimbali duniani. 

0 Comments