Polisi ya Tanzania yamtia mbaroni Sheikh Ponda kwa tuhuma za uchochezi

Jeshi la Polisi la Tanzania limemtia mbaroni Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini humo, Sheikh Ponda Issa Ponda kwa madai ya uchochezi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amethibitisha habari hizo za kukamatwa Sheikh Issa Ponda. Katika kikao na waandishi wa habari, Mambosasa amesema, “tunaye sisi polisi, tumemkamata kwa mahojiano ya uchochezi walioutoa kwenye kitu walichokiita waraka. Tunamhoji kutokana na ule waraka."

Kamanda huyo wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ameeleza kuwa, kiongozi huyo wa Kiislamu binafsi amekubali kwamba waraka walioutoa ni wake na taasisi yake, lakini eti viongozi wote wa taasisi wameukana kupitia vituo mbalimbali vya radio na televisheni.  Amesema kwa msingi huo jeshi la polisi litaendelea kumshikilia msomi huyo wa Kiislamu.

Katibu huyo wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania hivi karibuni alitoa mwito wa kufanyika uchaguzi huru na wa haki mwezi Oktoba mwaka huu nchini humo.


Sheikh Ponda Issa Ponda alitoa mwito huo Alkhamisi iliyopita katika kikao na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa, vyombo husika vinapaswa kuhakikisha kuwa uchaguzi huo mkuu unafanyika katika mazingira ya amani, uhuru na haki.
Sheikh Ponda katika kikao na waandishi wa habari Alkhamisi iliyopita
Kuhusu sifa za wagombea wa uchaguzi mkuu, Sheikh Ponda amesema waraka uliotolewa na taasisi hiyo imeorodhesha baadhi ya sifa hizo kama ifuatavyo: mgombea awe mkweli na mwenye utu, awe mwenye kuheshimu kiapo, awe mwenye sifa ya kupiga vita ubaguzi wa aina zote na awe mwenye maarifa ya kutosha ya kuongoza watu na serikali. Aidha amewataka Watanzania wasiwachague watu madikteta na wadhalilishaji katika uchaguzi huo wa Oktoba.

Ameeleza bayana kuwa, Waislamu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki hawaoni usawa wowote katika madaraka na ajira za serikali, na kwamba mfumo wa elimu wa taifa hilo umeshindwa kutoa fursa sawa wala kutenda haki kwa wote.

0 Comments