Prof Assad asema yupo tayari kwa majukumu MUM

KUFUATIA kuenea kwa taarifa za kuteuliwa kwake kuwa Naibu Makamu Mkuu (Fedha na Utawala) katika Chuo cha Waislamu cha Morogoro (MUM), aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amesema yuko tayari kwa majukumu hayo mapya.

Akizungumza na Gazeti Imaan, Prof. Assad alisema kwamba, amejisikia faraja kuteuliwa kushika wadhifa huo na anaamini atafanya kazi na wenzake atakaowakuta kwa ushirikiano mkubwa.

“Tumefundishwa kusema Alhamdullah kwa kila jambo. Mimi nilisema niko tayari kufanya kazi yoyote nikitakiwa kufanya. Kwa uteuzi huu, ninachoweza kukwambia ni kuwa, ninashukuru na nitakwenda kuifanya kazi ya Waislamu,” alisema.

Alipoulizwa, je jamii ya MUM na Waislamu itegemee nini kutoka kwake, Prof Assad alisema anafahamu kuwa chuo hicho ambacho kilianzishwa mwaka 2004 kina mipango yake, mikakati yake; hivyo naye anakwenda kusaidia kuitekeleza.

Taarifa isiyo rasmi iliyovujishwa kutoka katika chuo hicho wiki hii, ilisema kwamba, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM) Dkt. Abdulrahman Al-Muhallaan alimteua Prof Mussa Assad kuwa Naibu Makamu Mkuu mpya wa Chuo cha Kiislamu Morogoro – Fedha na Utawala.

Taarifa hiyo pia inasema kwamba, Mwenyekiti huyo alimteua Prof. Hamza Njozi kushika nafasi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Machapisho. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huo ulianza Juni 29.

Profesa Njozi anarejea kwa mara nyingine katika uongozi wa juu wa chuo hicho kwani alishawahi kukamata nafasi ya Umakamu Mkuu wa chuo hicho kwa miaka 12 hadi alipojiuzulu mwaka jana.

Kwa sasa, nafasi ya Naibu Makamu Mkuu – Fedha na Utawala inashikiliwa na Dkt. Issa Malecela wakati nafasi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Machapisho inashikiliwa na Dkt. Salim Hamis.

Wateule hao wawili wapya watafanya kazi chini ya Makamu Mkuu wa chuo, Profesa Hassan Tolla.

Katika tarifa hiyo iliyosambaa mitandaoni inasema Mwenyekiti, Dkt Al-Muhallaan aliwasifu watendaji waliopita kwa kufanya kazi nzuri katika nyakati zao, na kwamba waliweza kujitoa kwa nguvu zao zote na kuhakikisha kazi zinakwenda. Jaribio la gazeti hili la kumtafuta Afisa Uhusiano wa MUM athibitishe, akanushe au afafanue habari hizi halikufanikiwa kwani simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa. Hata hivyo, wafanyakazi kadhaa waliohojiwa alisema habari hizo ni za kweli, kama alivyothibitisha pia Prof. Assad.

Wadau wapongeza uteuzi huo…
Wakitoa maoni mbalimbali kuhusu uteuzi huo, watu wengi wameelezea kufurahishwa kwao, na kusema Prof Assad ni mtu sahihi na atakisaidia chuo hicho kutokana na uzoefu wake mkubwa katika mambo ya utawala na fedha.

Mmoja wa waliotoa maoni yao waasisi wa Jumuiya ya wanataaluma wa Kiislamu Tanzania (TAMPRO), Pazi Mwinyimvua Semili, ambaye alisema kwamba, ujio wa Prof Assad katika chuo hicho cha MUM ni taarifa njema ukizingatia kuwa vyuo vingi vya binafsi vinachangamoto nyingi za kiutendaji.

Alisema ukiangalia wasifu wa Prof Assad, utaona kuwa ana uzoefu wa kutosha wa uongozi, toka alipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia, alisema Prof. Assad ana weledi wa hali ya juu, na hivyo ni rahisi kuona kuwa atakisaidia chuo kufikia malengo yake, inshaAllah.

Pazi anaamini kuwa, kazi kubwa anayoweza kwenda kufanya Prof. Assad ni kusimamia zoezi zima la kutafuta, kutunza na kuangalia matumizi ya fedha.

“Tunajua vyuo vingi vya binafsi hapa Tanzania bado ni vichanga ukilinganisha na vya serikali, lakini pia kiuchumi bado havina vyanzo vingi vya mapato bali vinategemea zaidi ada za wanafunzi. Kwa hiyo tunategemea kwa uzoefu na ubobezi wake katika mambo ya fedha na usimamizi wa miradi huko alikotoka; ataweza pia kukisaidia chuo.”

0 Comments