Shura ya Maimamu yautambua waraka uliosomwa na sheikh Ponda kuwa ni waraka halali wa Taasisi hiyo

baada ya kukamatwa na kushikiliwa kwa Katibu wa Shura ya Maimamu nchini Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda, hatima ya kupata dhamana yake bado haijulikani, amesema msemaji wa Shura ya Maimamu.
Sheikh Ponda alikamatwa siku ya Jumapili baada yakuzungumza na waandishi wa habari juu ya waraka ulioandaliwa na Shura ya Maimamu Tanzania.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amenukuliwa na vyombo vya habari akisema wanamshikilia kwa mahojiano juu ya waraka huo.

"Tunaye sisi Polisi, tumemkamata kwa mahojiano ya uchochezi walioutoa kwenye kitu walichokiita waraka. Tunamhoji kutokana na ule waraka," amenukuliwa Kamanda Mambosasa akisema.

Msemaji wa Shura ya Maimamu Ibrahimu Mkondo ameaiambia BBC kwamba Shura ya Maimamu haijui kinachoondelea juu ya dhamana ya Sheikh Ponda.

"Hawajampeleka mahakamani na kimsingi hatujafahamu ni kituo gani wanachomshikilia kwa sababu tarehe 12 tulifatilia central hakuwepo pale na hadi leo hatujajua ni kituo gani anashikiliwa," amesema Mkondo.

Bwana Mkondo anasema polisi hawajasema ni kipengele gani hasa ambacho wanakiona kuwa ni hatari katika waraka huo wa Shura ya Maimamu lakini wanaamini suala la COVID-19 lililogusiwa katika waraka huo inawezekana likawa moja ya masuala yaliyosababishwa kukamatwa kwa Sheikh Ponda.

"Waraka ulishauri kwamba serikali iwaweke karantini wananchi badala ya kuwaaacha huru kama jinsi ambavyo ilikuwa.
Hili jambo polisi wanasema halijakaa vizuri. Pamoja na mambo mengine mengi ambayo wanasema waraka unachochea," amesema Mkondo.

Kuhusu umiliki wa waraka, Mkondo amekanusha kile alichokiita upotoshaji kwamba waraka ule ni wa Sheikh Ponda.
Amesema waraka ni wa Shura ya Maimamu na kwamba Sheikh Ponda aliusoma akiwa kama katibu wa Shura ya Maimamu.

BBC ilimtafuta msemaji wa jeshi la polisi Tanzania (SACP) David Misime lakini alisema yupo safarini na kushauri kumtafuta kamanda wa kanda maalumu ya polisi Dar es Salaam Mambosasa.

Hata hivyo simu ya Kamanda Mambosasa aidhahaikupokelewa ama ilikatishwa. Jitihada za kutafuta majibu ya polisi zinaendelea

0 Comments