Swala ya ‘Iyd Al-Adhwhaa kote Misri itaswalia katika msikiti mmoja tu

Katika taarifa, serikali ya Misri imesema uamuzi huo umechukuliwa na Kamati Kuu ya Kukabiliana na Janga la COVID-19.

Katika kikao kilichofanyika Jumatano chini ya uwenyekiti wa Waziri Mkuu Moustafa Mabdouli, imeamuliwa kuwa Swala ya Iyd Al-Adhwhaa itaswaliwa kama ilivyokuwa katika Swala ya Idul Fitr. Mwaka huu kutokana na janga la COVID-19 Swala ya Idul Fitr Misri iliswaliwa tu katika Msikiti wa Sayyid Nafisa mjini Cairo na kutangazwa mubashara katika televisheni ya kitaifa. Swala ya Idul Adha mwaka huu pia itaswaliwa katika msikiti mmoja na idadi ya waumini itakuwa ndogo sana.

Kamati ya Maulamaa Misri, chini ya uwenyekiti wa Sheikh Ahmed el-Tayyib, Imamu Mkuu wa Al-Azhar, imesema inajuzu au inaruhusiwa kisheria kuswali swala ya Idi nyumbani mwaka huu kutokana na janga la COVID-19. Mwaka huu Swala ya Idul Adha inatazamiwa kuswaliwa Julai 31.

Hadi sasa kuna watu 90,413 waliambukizwa COVID-19 nchini Misri huku 4,480 wakiwa wamepoteza maisha.

0 Comments