Tujikumbushe adabu za kula

Kwa kila kitendo afanyacho muislamu, iwe ni kusali, kutawadha, kuoga, na hata kuongea, ana nafasi ya kuchuma thawabu kutoka kwa allah ta’ala. hata hivyo, thawabu hizi zinaweza kupatikana tu kwa wale ambao watafanya matendo wayafanyayo kwa kufuata Sunna na mfano wa alivyofanya mtume (rehema za allah na amani zimshukie) kwa lengo la kupata radhi za allah.

Watu wanaotafuta radhi za allah ta’ala, maisha yao yote ni ibada. Kila wafanyalo, ikiwemo kula na kunywa, mambo ambayo binadamu wote tunategemea kwa ajili ya uhai wetu, pia inaweza kuwa ibada – madhali tunanuia kuwa ni ibada na tunafuata sunna za mtume (rehema za allah na amani zimshukie) katika namna tunavyoyaendea.

Katika makala haya tutaangalia adabu za kula na kunywa ambazo zimegawanyika katika mafungu matatu. mafungu hayo matatu ni ni adabu kabla ya kuanza kula, adabu za wakati wa kula na adabu za baada ya kumaliza kula.

Adabu za kabla ya kuanza kula

Kunawa mikono yako: Mikono lazima ioshwe kabla Muislamu hajaanza kula. Kwa kufanya hivi, mtu hataathirika na uchafu ambao unaweza kuwa katika mikono yake. Katika hadithi sahihi iliyosahihishwa na Al- Albani, Bi. Aisha amesema:

“Mjumbe wa Allah, rehema na amani zimshukie, alipotaka kula na kunywa, aliosha mikono kwanza kisha ndio hula au kunywa.” [Sunan al-Nasā’ī ].

Kutaja jina la Allah kabla ya kuanza kula: Ni wajibu kutaja jina la Allah kabla ya kuanza kula kwa kusema : ‘Bismillah’ (kwa jina la Allah).

Katika hadithi iliyopokelewa na Umm Kalthoom kutoka kwa ‘Aa’ishah (Allah amridhie) Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Pindi yoyote miongoni mwenu anapokula, ataje jina la Allah. Akisahau kutaja jina la Allah mwanzo, basi If he forgets to aseme ‘Bismillaahi awwalahu wa aakhirahu (Kwa jina la Allah mwanzo na mwisho) – Tirmidhy.

Adabu wakati wa kula

Kula kwa mkono wa kulia: Ni wajibu Muislamu anapokula ale kwa mkono wake wa kulia, na kamwe asile kwa mkono w kushoto. Imesimuliwa kutoka kwa Ibn ‘Umar (Allah amuwie radhi) kwamba Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Asile mmoja wenu na mkono wa kushoto au kunywa (kwa mkono wa kushoto) kwa sababu Shetani anakula na kunywa kwa mkono wa kushoto – [Muslim] . Kanuni hii inafanya kazi kama hamna dharura inayomlazimisha mtu kula kwa mkono wa kushoto, ikiwemo ugonjwa.

Kula kutoka sehemu ya sahani inakuelekea: Ni Sunna kula sehemu ya chakula inayokuelekea moja kwa moja na sio kupeleka mkono eneo la sahani linalowaelekea wengine. Hii ni kwa mujibu wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye alimwambia ‘Umar ibn Abi Salamah,

“Ewe kijana sema ‘Bismillaah’, kula kwa mkono wa kulia na kula sehemu (ya sahani) inayokuelekea” – [Muslim].

Kula kwa vidole vitatu: Sunna ni kula kwa vidole vitatu. Inaelezwa kuwa kula kwa zaidi ya vidole vitatu ni alama ya ulafi na ni tabia mbaya kwa sababu hakuhitaji zaidi ya vidole vitatu kubeba tonge kwa aina nyingi za vyakula.

Kunawa mikono ukimaliza kula: Kama ilivyokuwa ni muhimu kunawa kabla ya kuanza kula, vilevile ni Sunna hii inatimia kwa kuosha kwa maji pekee lakini ni bora kuosha mikono kwa sabuni.

Kula mabaki yaliyodondoka chini. Inaelezwa kuwa ni Sunna kuokoteza punje au vipande vilivyondoka chini na kula. Muislamu anatakiwa aviokote, avisafishwe na kula. Mabaki hayo yasiachwe kwani Muislamu hujui baraka za chakula chake ziko wapi. Huenda ni katika mabaki hayo ndipo ilipo baraka ya chakula.

Ili kufanikisha hilo, ni muhimu kuweka kapeti safi chini ya sahani ili iwe rahisi kukokoteza mabaki na kula, bila kinyaa.

Baadhi ya adabu nyingine ni pamoja na kula kwa pamoja. Imependekezwa katika familia baba kula na mke na watoto ni jambo bora. Vilevile, ni Sunna kusukutua mdomo baada ya kula ili kuondoa mabaki ya chakula.Kadhalika, imehimizwa kumuombea dua aliyewafadhili chakula, au hata mpishi na kadhalika kumshukuru na kumsifu Allah Ta’ala.

Pia imekatazwa kuegama wakati wa kula, kutema mate au kumeka kamasi ila tu kama haina budi. Pia haifai kukikosoa chakula. Haifai kushiba sana. Haifai kula katika chombo cha dhahabu au fedha na haifai kuzungumza mambo ya haramu wakati wa kula.

0 Comments