Ndugu Waumini! Tukumbushane kuifufua Sunnah ya kuleta Takbiyr kuanzia unapoandama mwezi wa Dhul-Hijjah mpaka mwisho wa Ayyaamut-Tashriyq (Yaani kuanzia tarehe 1 Dhul-Hijjah mpaka 13 Dhul-Hijjah) baada ya Swalaatul-'Asr ndio kumalizika kwake kutokana na dalili zifuatazo:
Allaah ('Azza wa Jalla) Anaamrisha:
لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ
((Ili washuhudie manufaa yao; na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kwa yale Aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo. [Al-Hajj 28]
Na pia:
كَانَ إبْن عَمَر وَأبُو هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّه عَنْهُما يَخْرُجَانِ إِلَى السُّوقِ فِي أَيَّامِ العَشْرِ يُكَبِّرَانِ، وَيُكَبِّرُ النَّاسُ بِتَكْبِيرِهِمَا .
Ibn 'Umar na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) walikuwa wakienda sokoni katika siku kumi (za Dhul-Hijjah) na kutamka Takbiyr kwa sauti na watu wakiwaigiza. [Al-Bukhaariy]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَاذْكُرُوا اللَّـهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ ۚ
Na mdhukuruni Allaah katika siku za kuhesabika. [Al-Baqarah: 203]
Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: Siku za kuhesabika ni siku za tashriyq (11, 12, 13 Dhul-Hijjah) na siku maalumu ni siku za kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah. [Al-Qurtwubiy: 3.3]
Takbiyr katika masiku haya matukufu ni aina mbili:
Takbiyr Al-Mutwlaq: Za Nyakati Zote:
Takbiyr wakati wote mchana na usiku tokea unapoingia mwezi wa Dhul-Hijjah na inaendelea mpaka siku ya mwisho ya Tashriyq (tarehe 13 Dhul-Hijjah) na kumalizika baada ya kuingia Magharibi.
Takbiyr Al-Muqayyad: Za Nyakati Maalumu Za Kukadirika:
Takbiyr baada ya kila Swalaah za fardhi na huanza baada ya Swalaah ya Alfajiri Siku ya 'Arafah mpaka inapoingia Magharibi ya siku ya mwisho ya Tashriyq (tarehe 13 Dhul-Hijjah).
Inavyopasa kufanya Takbiyr:
اللَّهُ أَكْبَرُ، اللَّهُ أَكْبَرُ، لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ، اللَّهُ أَكْبَرُ، اللَّهُ أَكْبَرُ، وَلِلَّهِ الْحَمْد
Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, laa Ilaaha illa Allaah, Allaahu Akbar Allaahu Akbar WaliLLaahil-Hamd
Takbiyr hizo za masiku haya matukufu zimetekelezwa na baadhi ya Maswahaba watukufu na ni Mustahabb (imependekezwa) na wengi katika Salaf wa madhehebu ya Hanbaliy, Ash-Shaafi’iyy, Hanafiy na wengineo kama ifuatavyo:
Imaam An-Nawawiy - Al-Majmuw’ (5/32).
Ibn Rajab - Fat-hul-Baariy (6/125, 130).
Ibn Taymiyyah - Majmuw’ Al-Fataawaa (24/220. 222).
Imaam Ibn Baaz - Fataawaa Nuwr ‘Alad-Darb (13/355).
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn - Ash-Sharh Al-Mumti’ (5/166), Majmuw’ Fataawaa wa Rasaail Al-‘Uthyamiyn (16/262, 265).
Post a Comment