Umoja wa Mataifa waleta maelewano baina ya Waislamu na Wakristo Bangui

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA umetekeleza mradi wa maji na kusaidia kuleta utangamano baina ya jamii kwenye manispaa moja ya mji mkuu wa nchi hiyo, Bangui.

MINUSCA imejenga visima vitatu vya maji kwenye manispaa ya 3 ya maeneo ya  Sara, Yakite na Castors ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa eneo hilo waliokuwa wanakumbwa na uhaba mkubwa wa maji.

Luteni Kanali Leila Zemzoumi kutoka MINUSCA anasema kuwa wamejenga visima hivyo vitatu katika maeneo hayo kwa sababu kulikuwepo na mizozo kupindukia ndani ya jamii na baina ya jamii. Ameongeza kuwa ukosefu wa maji ulichochea zaidi mapigano hayo baina ya jamii za Waislamu na za Wakristo.

Uchimbaji wa visima hivyo ni kupitia miradi ya matokeo ya haraka, au QIP inayotekelezwa na MINUSCA ambapo Adam Roufai ambaye ni Naibu Meya wa Manispaa ya 3 anasema wanashukuru sana mwa mradi huo wa maji kwa kuwa utasaidia katika usalama wa kiafya hususan wakati huu wa janga la virusi vya Corona au COVID-19.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakilinda doria mjini Bangui
Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati yalizuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya Rais Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi.

Hivi sasa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameweza kujitahidi kurejesha utulivu katika nchi hiyo ya kati kati mwa Afrika.

0 Comments