Umoja wa Mataifa waonya kuibuka tena machafuko Jamhuri ya Afrika ya Kati

Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na mataifa jirani kuchukua hatua za kupambana na kile ulichokitaja kuwa tishio la muda mrefu katika eneo hilo, hasa katika kipindi hiki cha miezi sita kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais.

Katika ripoti, kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaohusika na kuchunguza vikwazo vya silaha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati limebaini kuibuka tena kwa mapigano, hususan kaskazini mashariki mwa nchi hiyo yaliyochochewa na kuwasili kwa wapiganaji na silaha kutoka nje ya nchi hiyo.

Hii imedhihirika baada ya kukutwa kwa vitambulusho vya wapiganaji kutoka  mataifa ya Chad na Sudan waliouawa ambao ni kutokana kundi moja la waasi nchini humo.  Ripoti hiyo imetahadharisha kuwa, jambo lingine linalotia shaka ni biashara ya kikanda ya silaha kutoka  Sudan, Chad, lakini pia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo mwezi April mwaka jana vilikamatwa vifaa na zana nyingi  za kijeshi.Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati yalizuka mwaka 2013 baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Baada ya Rais Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi. Kwa sasa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanajitahidi kurejesha utulivu katika nchi hiyo ya kati kati mwa Afrika.

Mashirika mbalimbali ya misaada ya kibinadamu yameendelea kuonya kwamba, hali ya kibinadamu katika nchi hiyo inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku huku idadi ya wakimbizi ikiongezeka.

0 Comments