Unaposubiri Mitihani Ya Mola Wako Ni Kheri Kwako

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

 ((وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوفْ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الأَمَوَالِ وَالأنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ))   ((الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُواْ إِنَّا لِلّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعونَ)) ((أُولَئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ)

((Hapana shaka Tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanaosubiri))  ((Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Allaah, na Kwake Yeye hakika tutarejea))  ((Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao na Rehma. Nao ndio wenye kuongoka)) [Al-Baqarah: 155:157]

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatujulisha kuwa Huwapa mitihani ya aina mbali mbali waja Wake kisha Huwatazama watapokea vipi mitihani hiyo; wataipokea na kushukuru au watashindwa kusubiri na badala yake watakufuru?  

 

Kwa hiyo Muumini anatakiwa arudi kwa Mola wake anapokumbwa na msiba wa aina yoyote na kusema ((Innaa Lillaahi  wa innaa Ilayhi raaji'uun)). Kauli njema nyingine ya kusema ni kama alivyotufundisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

((لَا يُصِيب أَحَدًا مِنْ الْمُسْلِمِينَ مُصِيبَة فَيَسْتَرْجِع عِنْد مُصِيبَته ثُمَّ يَقُول : اللَّهُمَّ أَجِرْنِي فِي مُصِيبَتِي وَاخْلُفْ لِي خَيْرًا مِنْهَا إِلَّا فُعِلَ ذَلِكَ بِهِ))

((Hakuna Muislamu yeyote ambaye atakayekumbwa na msiba akasema istirja'a  (Innaa Lillaahi wa innaa ilayhi raaji'uun)) [Hakika sisi ni wa Allaah, na Kwake Yeye hakika tutarejea] kisha akasema: "Allaahumma Ajirniy Fiy Muswiybatiy Wakhluf-liy khayram-minhaa" [Ee Allaah Nilipe (thawabu) kwa msiba wangu na nipe [badala yake] bora kuliko huo] basi Allaah Atamuitikia.

Mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhiya Allaahu 'anhaa] anasema, nilihifadhi maneno haya, na alipofariki Abu Salamah nilisema 'istirja’a, kisha nikasema "Allaahumma Ajirniy Fiy Muswiybati Wakhluf-liy khayram-minhaa", kisha nikawaza na kusema: "Nani atakayekuwa bora kuliko Abu Salamah?". Eda yangu ilipomalizika Mjumbe wa Allaah   (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba ruhusa kuniona wakati nilikuwa napaka rangi ngozi niliyokuwa nayo. Niliosha mikono nikamruhusu kuingia na nikampa mto akaukalia. Kisha akaniomba nifunge ndoa naye. Alipomaliza kauli yake, nilisema: "Ee Mjumbe wa Allaah, si kwamba sikutaki lakini mimi ni mwenye wivu sana na nakhofu usije ukaona tabia mbaya yangu ambayo Allaah Ataniadhibu kwayo. Mimi umri wangu mkubwa, pia nina watoto". Akasema: ((Ama kwa wivu uliotaja, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atauondosha kwako. Ama umri wako kuwa ni mkubwa kama ulivyotaja, mimi pia nimeshafikwa na uliyofikwa. Na ama kuwa na watoto, wao pia ni watoto wangu)). Akasema (Ummu Salamah). Nimejisilimisha kwa Mjumbe wa Allaah". Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuoa Ummu Salamah ambaye alisema baadaye: Allaah Amenilipa (mume) aliye bora kuliko Abu Salamah, naye ni Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Imaam Ahmad na Muslim kaisimulia kwa ufupi zaidi ya hivi].

 

Na hadiyth nyingine inasema:

 

((عجباً لأمر المؤمن إن أمره كله له خير إن أصابته سراء شكر فكان خيراً له وإن أصابته ضراء صبر فكان خيراً له وليس ذلك إلا للمؤمن )) مسلم

((Ajabu ya hali ya Muumini kuwa mambo yake yote ni kheri; anapofikwa na furaha hushukuru na huwa kheri kwake, na anapofika na matatizo husubiri na huwa ni kheri kwake, na haiwi hivyo (sifa hiyo) ila kwa Muumini)) [Muslim]

 

Kwa hivyo usihuzunike ndugu Muislamu unapokumbwa na msiba, maafa au madhara yoyote kwani ni kheri kwako na hata mja hufutiwa madhambi kama tulivyobashiriwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

  عائشة رضي الله عنها ، قالت: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((ما من مصيبة تصيب المسلم إلا كفَّر الله بها عنه، حتى الشوكة يُشاكها))

 

Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Hakuna Muislamu yeyote atakayefikwa na msiba ila Allaah Atamfutia dhambi kwayo japo kama ni kuchomwa na mwiba)) [Al-Bukhaariy]

0 Comments