Upotoshaji wa tiba za Kisunna

Moja ya majaribu makubwa ya Allah kwa waja wake ni ugonjwa ama maradhi, kama ambavyo pia afya njema ama uzima ni moja ya neema kubwa za Allah juu yao. Wenye hekima wamesema: “Uzima ni taji (medani) juu ya vichwa vya wazima; hawalioni ila wagonjwa.”

Afya haiuzwi dukani wala sokoni, bali ni neema itokayo kwa Allah. Pia, kamwe haipimiki na kitu chochote cha thamani. Hali ya uzima haifanani na ugonjwa. Mtu anapokuwa mgonjwa shughuli zake husimama, hudhoofu na kuishiwa na ari na nguvu ya hata kuwaza tu mambo ya maisha.

Si hayo tu, mgonjwa pia hupoteza hata ladha ya chakula. Vyakula vitamu huvihisi vichungu, vyenye harufu nzuri huvichukia na kuvikataa. Mara kadhaa tumeshuhudia matajiri wakubwa jinsi wanavyoziteketeza mali zao katika kujitibu na hata kuwa tayari kumaliza utajiri wote ili warejeshe afya zao.

Ni kutokana na umuhimu wa afya ndiyo maana Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alisema: “Atakayeamka miongoni mwenu akiwa na amani katika familia yake, salama katika mwili wake, na chakula cha siku yake; basi anakuwa kama kwamba amekusanyiwa dunia yote” [Tirmidhy].

Na katika Hadith nyengine, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Muombeni Allah msamaha na afya njema, kwani mtu hajapatapo kupewa kheri kubwa zaidi baada ya imani kuliko afya.” [Tirmidhy]. Na kweli, kila siku mtu hupenda awe mzima.

Licha ya kwamba kila siku watu hupenda wawe wazima, lakini ukweli ni kwamba, binadamu yuko karibu sana na maradhi ama kifo. Mwenyezi Mungu amesema katika Hadith al- Quds: “… enyi wanadamu, nyote ni wagonjwa ila nitakayemponyesha, basi niombeni ponyo nikuponyesheni..”

Kama ambavyo mgonjwa hupata taabu sana kwa maradhi yaliyompata, shida pia huwafika familia yake ambao huhangaika huku na huko kumtafutia tiba mnasaba na ya haraka ili jamaa yao apone na arudi katika hali ya kawaida. Na hapo tiba ndipo inapopata soko dunia nzima.

Binadamu akiumwa au anapokuwa hana namna ya kukwepa tiba. Kama hatokwenda hospitali na kukutana na waitwao madaktari, atawafuata waganga wa kienyeji.

Viwanda vya kutengeneza dawa vimejaa kote ulimwenguni . Makampuni ya usafirishaji na uuzaji madawa nayo yamejaa kila kona. Madaktari waliosomea fani mbalimbali za kuyatibu magonjwa lukuki nao wapo kila pembe. Kwa upande wa pili, watabibu (waganga) wa kienyeji nao takriban wamekuwepo kila zama na kila pahala.

Mgawiko wa tiba

Kama tulivyoashiria hapo juu, tiba hugawika kutegemea aina ya maradhi yanayompata mtu. Kuna magonjwa ya kibaioloji ambayo mgojwa anapokwenda hospitali na baada ya kufanyiwa vipimo, madaktari huyagundua na kumpatia tiba muafaka.

Lakini, pia kuna maradhi ya kiruhani (yasiyoonekana) ambayo mara nyingi husababishwa na mashetani, wasiwasi, husda na uchawi. Ni vigumu kwa madaktari kubaini maradhi ya aina hii; hivyo basi, mgonjwa hulazimikakutafuta waganga mitaani wanaoaminika kuwa ni ‘wataalamu’ ili atibiwe.

Uislamu na dhana ya magonjwa ya kiruhani

Uislamu unataka tuamini kwamba, kuna ulimwengu wa viumbe wasioonekana kama majini na Malaika. Malaika ni viumbe watakatifu hawafanyi makossa, lakini majini ni kama wanadamu yaani wamepewa hiyari ya kumtii Allah au kumuasi.

Kwa hiyo, majini wanaweza kutawaliwa na madhambi kama vile: unafiki, ukafiri, dhana potofu, husda, dhuluma, chuki, choyo na kadhalika kama walivyo wanadamu. Hawa ndiyo huitwa mashetani.

Shetani anaweza kumshambulia (kumuingia mwilini) mwanadamu na kumsababishia ugonjwa. Kadhalika, Uislamu unatutaka tuamini uwepo wa uchawi na wachawi ambao hutumia njia za gizani na za kiuadui na kuwasababishia wengine madhara. Matukio mbalimbali na uzoefu pia unathibitisha hilo.

Hebu turejee baadhi ya maandiko yanayogusia kadhia hii. Allah Ta’ala anasema : “Sema, najikinga na Bwana wa watu. Mfalme wa watu. Muabudiwa wa watu. Kutokana na shari za mtia wasiwasi arejeae nyuma. Ambaye huingiza wasiwasi katika vifua vya watu. Miongoni mwa majini na watu.”

Kimantiki, Mtume hawezi kutakiwa ajikinge na kitu kisichokuwepo. Aya hizi zinatufundisha kwamba, shetani anaweza kumuingia binad
amu, akamuyumbisha, akamuangusha chini na kumgaragaza bila ya kujielewa, au hata kumsababishia uwenda wazimu. Naudhu billah!

Katika kisa cha Nabii Musa, Allah Aliyetukuka amesema: “(Mussa) akawambia (wachawi), ‘Bwageni.’ Basi walipoweka chini (fimbo na kamba zao) waliyaroga macho ya watu na wakawaogopesha (wakaona nyoka badala ya fimbo na kamba), na walikuja na uchawi mkubwa.” [Qur’an, 7:116].

Kuna maandiko mengi yanayothibitisha uwepo wa maswali ya uchawi, ulogaji na husda ambayo huwapelekea watu kupatwa na maradhi, na ambayo vipimo vya hospitali hushindwa kuyagundua. Lakini tunadhani msomaji wetu mpendwa amepata picha kwa hoja tulizozirejea.

Hata baadhi ya madaktari husikika wakiwaambia wenye mgonjwa kuwa, hayo si maradhi ya hospitali na kuwashauri waende kwa waganga wa kienyeji wakusaidieni.

Msimamo wa Uislamu juu ya tiba

Uislamu, kama kawaida yake, haujaacha jambo muhimu la kimaumbile kama hili. Uislamu wenyewe umejinadi kwamba ni dini inayoendana na maumbile ya watu. Na kwa vile kuumwa ama maradhi ni katika vipengele muhimu vya maisha, basi haukuliacha bila kulizungumza.

Uislamu umetoa muongozo safi kuanzia kwenye kinga dhidi ya maradhi, yawe ya kibaiolojia au ya kiruhania. Lakini pia umehimiza watu wanapofikwa na majaribu ya Allah ya maradhi, wajitibu. Pia, Uislamu haukuacha kutoa maelekezo tiba yenyewe iweje ili watu wasije kuchupa mipaka.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “ Jitibuni enyi waja wa Allah kwani Allah hakuweka ugonjwa ila ameweka pia na tiba yake.” [Abu Dawud].

Kutokana na unyeti wa suala lenyewe, na makosa makubwa wanayoyafanya baadhi ya waitwao ‘waganga’ mitaani huku wakihusisha wanayoyafanya na tiba ya kisunna, ndiyo tumeona ni vyema tuandike makala hizi ili tuzungumzie masharti ya tiba ya kisunna, sifa za tabibu na pia miiko yake.

Tunadhani kwa taufiq ya Allah Aliyetukuka tutakuwa tumechangia sana katika kuhakikisha watu wanabaki katika utiifu kwa Allah hata katika kipindi kama hiki kigumu.

0 Comments