Utapokea Kitabu Chako Kwa Mkono Gani?
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

((وَوُضِعَ الْكِتَابُ فَتَرَى الْمُجْرِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا فِيهِ وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلاَ كَبِيرَةً إِلاَّ أَحْصَاهَا وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا وَلاَ يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا))

 

((Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyoogopa kwa yale yaliomo humo. Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila huliandika? Na watayakuta yote waliyoyatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako Hamdhulumu yeyote(( [Al-Kahf: 49]

.

 

Aayah hii inatupa picha ya hali itakavyokuwa Siku ya Qiyaamah kwamba matendo yetu yote tutayaona yamerekodiwa katika kitabu. Siku hiyo, ni Siku isiyo na shaka, siku ya miadi, siku ya inayosubiriwa,  siku ya majuto, siku ya nyoyo kushituka na macho kukodoka, siku ya mashaka, siku ambayo hakuna budi kwa kila mmoja kuifikia. 

 

Ndugu Waislamu, hii ni siku ya kulipwa mema au mabaya, Siku watakayosimama watu wote na majini mbele ya Mola wa Ulimwengu, siku ambayo kafiri atasema:

 ((يَا لَيْتَنِي كُنتُ تُرَابًا))

((Laiti ningelikuwa udongo!)) [An-Nabaa: 40]

.

 

Je, Umefikiria na kuwaza hali yako itakavyokuwa siku hiyo utakaposimama mbele ya Mola wako Mtukufu na huku unasubiri hesabu upewe kitabu chako? Mmoja wetu anapoingia kufanya mtihani au anapokwenda mahakamani kuhukumiwa, moyo wake hudunda kwa nguvu kwa khofu ya kutaka kujua atafanyaje au kuwaza yatakayomkabili.  Itakuwaje hali ya moyo siku hiyo wakati matokeo yake yatakuwa ni aidha Pepo ya milele yenye maisha ya raha au moto wenye adhabu kali?  Hasa kiwa umeishi umri wako wote katika maasi au umezama katika starehe ya dunia bila kuchuma mema yoyote, vipi itakuwa hali yako siku hiyo? 

 

Amiyrul Muuminiyn amesema manenno ya busara kabisa:

"حاسبوا أنفسكم قبل أن تحاسبوا، وزنوها قبل أن توزنوا، فإن أهون عليكم في الحساب غدًا أن تحاسبوا أنفسكم اليوم، وتزينوا للعرض الأكبر،  ((يومئذ تعرضون لا تخفى منكم خافية))  

    

"Hesabuni nafsi zenu kabla ya kuhesabiwa, na zipimeni kabla ya kupimwa, kwani ni bora (wepesi) kwenu kupima (amali zenu) leo kabla ya (kupimwa) kesho kwenye Hesabu, na jipambieni kwa siku ya Hadhara kuu, ((Siku hiyo mtahudhuriwshwa haitafichika siri yoyote))" [Al-Haaqah: 18].

 

Jipime ndugu Muislamu na jiulize: Je, utakuwa miongoni mwa watakaopewa vitabu vyao mkono wa kulia ukakichukua kwa furaha kubwa na kukionyesha kwa wenzako kama unapopata shahada yako uliyofuzu vizuri sana ukatamani kila mmoja aione, uwaambie kwa furaha 'nimefuzu! nimefuzu vizuri sana! Mfano huo ni kama mfano wa kauli ya Allaah: 

 ((فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَيَقُولُ هَاؤُمُ اقْرَؤُوا كِتَابِيهْ)) ((إِنِّي ظَنَنتُ أَنِّي مُلَاقٍ حِسَابِيهْ))  ((فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ))  ((فِي جَنَّةٍ عَالِيَةٍ))  ((قُطُوفُهَا دَانِيَةٌ))  ((كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا أَسْلَفْتُمْ فِي الأََيَّامِ الْخَالِيَة))

((Basi ama atakayepewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, atasema: Haya someni kitabu changu!)) ((Hakika nilijua ya kuwa nitapokea hisabu yangu)) ((Basi yeye atakuwa katika maisha ya kupendeza)) ((Katika Bustani ya juu)) ((Matunda yake ya karibu)) ((Waambiwe: Kuleni na mnywe kwa furaha kwa sababu ya mlivyotanguliza katika siku zilizopita)) [Al-Haaqah: 19-24]

 

Au utakuwa miongoni mwa wale watakaopewa kitabu chao mkono wa kushoto ukawa na majuto makubwa usiyoyaweza kuyarekebisha tena? Kama Asemavyo Allaah (سبحانه وتعالى):

(( وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِشِمَالِهِ فَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُوتَ كِتَابِيهْ)) ((وَلَمْ أَدْرِ مَا حِسَابِيهْ))  

 

((Na ama atakayepewa kitabu chake katika mkono wake wa kushoto, basi yeye atasema: Laiti nisingelipewa kitabu changu!)) ((Wala nisingelijua nini hisabu yangu))

 

Majuto yatazidi kuwa makubwa hadi kwamba mtu atatamani mauti!  

((يَا لَيْتَهَا كَانَتِ الْقَاضِيَةَ)) ((مَا أَغْنَى عَنِّي مَالِيهْ)) ((هَلَكَ عَنِّي سُلْطَانِيهْ))

 

((Laiti mauti ndiyo yangelikuwa ya kunimaliza kabisa)) ((Mali yangu hayakunifaa kitu)) ((Madaraka yangu yamenipotea))

Wataamrishwa Malaika wamchukue mtu muovu huyo wamtupilie mbali motoni! 

 ((خُذُوهُ فَغُلُّوهُ)) ((ثُمَّ الْجَحِيمَ صَلُّوهُ)) ((ثُمَّ فِي سِلْسِلَةٍ ذَرْعُهَا سَبْعُونَ ذِرَاعًا فَاسْلُكُوهُ))

 

(([Pasemwe]: Mshikeni! Mtieni pingu!)) ((Kisha mtupeni Motoni!)) ((Tena mtatizeni katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini!))

 

Sababu ni kwa kuwa:

 ((إِنَّهُ كَانَ لاَ يُؤْمِنُ بِاللَّهِ الْعَظِيمِ))

 

((Kwani huyo hakika alikuwa hamuamini Allaah Mtukufu))

Hakuamini amri za Allaah (سبحانه وتعالى) na makatazo Yake pamoja na aliyokuja nayo Mtume Wake.

 

Na pia:

 

  ((وَلاَ يَحُضُّ عَلَى طَعَامِ الْمِسْكِينِ))

((Wala hahimizi kulisha masikini))

 

Ikiwa mtu alishughulishwa duniani na ndugu au jamaa au rafiki, basi Siku hiyo hakuna hata mmoja atakeyemfaa mwenziwe kwani kila mmoja atakuwa analo lake la kukhofia.

  (( فَلَيْسَ لَهُ الْيَوْمَ هَاهُنَا حَمِيمٌ))

 

((Basi leo hapa hana jamaa wa kumwonea uchungu))

 

Chakula cha humo motoni ni usaha unaotoka katika miili ya watu na mti wa Zakkuum ulio mchungu ajabu, ulio na miba na unaokirihisha kabisa!

 ((وَلاَ طَعَامٌ إِلاَّ مِنْ غِسْلِينٍ))  (( لاَ يَأْكُلُهُ إِلاَّ الْخَاطِؤُونَ))

 

((Wala hana chakula ila usaha wa watu wa Motoni)) ((Chakula hicho hawakili ila wakosefu)) [Al-Haaqah: 25-37]

.

 

Nani atakayeridhika kuwa katika hali hiyo? Kwanini basi mtu aache kuswali, kufunga Swawm na kutenda mema? Au kupoteza wakati kwa mambo ya upuuzi? Au kumuasi Mola Mtukufu na hali siku ya Qiyaamah mtu atasimama mbele Yake kujibu kila baya alilolitenda.

 

Anasema Allaah سبحانه وتعالى katika Hadiythil-Qudsiyy

((ياعبادي إنما هي أعمالكم  أحصيها لكم فمن وجد خيراً فليحمد الله ومن وجد غير ذلك فلا يلومن إلا نفسه)) مسلم

 

((Enyi waja Wangu, ni vitendo vyenu Ninavyovihesabu, kwa ajili yenu Nikakulipeni.  Kwa hivyo anayekuta wema amshukuru Allaah na yule anayekuta yasiokuwa mema (basi) ajilaumu mwenyewe)) [Muslim].

 

Tunamuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Atujaalie miongoni mwa watakaopokea vitabu vyao kuliani kama Anavyosema:

((فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ))   ((فَسَوْفَ يُحَاسَبُ حِسَابًا يَسِيرًا )) ((وَيَنقَلِبُ إِلَى أَهْلِهِ مَسْرُورًا))

((Ama atakayepewa daftari lakekwa mkono wa kulia)) ((Basi huyo atahisabiwa hisabu nyepesi)) ((Na arudi kwa ahli zake na furaha)) [Al-Inshiqaaq: 7-9]

.

 

Na Asitujaalie tukawa miongoni mwa wale watakaopewa vitabu vyao katika mkono wa kushoto au nyuma ya migongo yao:

 ((وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ وَرَاء ظَهْرِهِ))  ((فَسَوْفَ يَدْعُو ثُبُورًا ))    ((وَيَصْلَى سَعِيرًا)) 

 

((Na ama atakayepewa daftari lakekwa nyuma ya mgongo wake)) ((Basi huyo ataomba kuteketea)) ((Na ataingia Motoni))  [Al-Inshiqaaq: 10-12]

 

******************

0 Comments