Waislamu Tanzania wataka uchaguzi huru na wa haki, wataja sifa za wagombea


Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania ametoa mwito wa kufanyika uchaguzi huru na wa haki mwezi Oktoba mwaka huu nchini humo.

Sheikh Ponda Issa Ponda ametoa mwito huo leo Alkhamisi katika kikao na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa, vyombo husika vinapaswa kuhakikisha kuwa uchaguzi huo mkuu unafanyika katika mazingira ya amani, uhuru na haki.

Kuhusu sifa za wagombea wa uchaguzi mkuu, Sheikh Ponda amesema waraka uliotolewa na taasisi hiyo imeorodhesha baadhi ya sifa hizo kama ifuatavyo: mgombea awe mkweli na mwenye utu, awe mwenye kuheshimu kiapo, awe mwenye sifa ya kupiga vita ubaguzi wa aina zote na awe mwenye maarifa ya kutosha ya kuongoza watu na serikali.

Sifa zingine zilizoainishwa kwenye waraka huo wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania ni mgombea awe mwenye kuheshimu uhuru na mawazo ya watu wengine,  mbali na kuzijua na kuziheshimu haki za binadamu. Kadhalika taasisi hiyo ya Waislamu wa Tanzania imetaka wananchi wasiwachague watu madikteta na wadhalilishaji katika uchaguzi huo wa Oktoba.
Sheikh Issa Ponda na viongozi wengine wa Kiislamu katika kikao na wanahabari Dar es Salaam
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania amesema Waislamu wa Tanzania wanataka haki na usawa na ndipo wamekuwa wakishiriki katika chaguzi mbali mbali za nchi hiyo. Amesema Waislamu wa Tanzania hivi sasa hawaoni nafuu katika uhuru wa kuabudu, uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe, usalama wa viongozi wao, Madrasa zao, Misikiti na watu wao.

Aidha ameeleza bayana kuwa, Waislamu katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki hawaoni usawa wowote katika madaraka na ajira za serikali, na kwamba mfumo wa elimu wa taifa hilo umeshindwa kutoa fursa sawa wala kutenda haki kwa wote.

0 Comments