Amnesty International: Polisi ya India ilishirikiana na magenge ya Wahindu kuwashambulia Waislamu


Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema jeshi la polisi la India lilifanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kwa kushirikiana na magenge ya Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mipaka kuwashambulia Waislamu katika mji mkuu New Delhi mapema mwaka huu.


Katika taarifa, shirika la Msamaha Duniani lenye makao yake mjini London Uingereza limesema, "polisi ya India ilihusika kivitendo katika ghasia zilizoibuka katika mji mkuu wa nchi hiyo mnamo Februari mwaka huu, ambapo watu 53 aghalabu wakiwa ni Waislamu waliuawa huku mamia ya wengine wakijeruhiwa."


Amnesty imebainisha kuwa, mongoni mwa ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na maafisa wa polisi wa India wakati huo ni kushirikiana na wafanya ghasia, kuwafanyia mateso Waislamu wakiwa korokoroni, kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, kuvunja maandamano ya amani, na kufumbia macho jinai zilizofanywa na Wahindu wafanya fujo. Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres aliikosoa serikali ya India kwa ubaguzi inaowafanyia Waislamu wa nchi hiyo, ikiwemo kunyimwa huduma zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya corona.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita zimeshuhudiwa hatua na maamuzi kadhaa yaliyochukuliwa na serikali ya India dhidi ya Waislamu, ambayo yamezusha malalamiko makubwa ndani na nje ya nchi hiyo.


Kuwapatia Wahindu ardhi ya msikiti wa kihistoria walioubomoa wa Babri, kufutwa mamlaka maalumu ya ndani ya kujiendeshea mambo yake liliyokuwa limepewa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India ambalo wakazi wake ni Waislamu, kubatilishwa uraia wa mamia ya maelfu ya Waislamu, kupitishwa sheria mpya ya uraia na kuwapatia uraia wa India raia wa kigeni kwa sharti la kutokuwa Waislamu, ni baadhi tu ya maamuzi ya kibaguzi yaliyochukuliwa na serikali ya chama tawala cha Kihindu cha Bharatiya Janata (BJP) nchini India dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.

0 Comments